MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewaasa viongozi wa siasa kutowagawa wananchi katika makundi ya siasa badala yake washirikaine ili kuleta maendeleo ndani ya jamii.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, wakati wa uzinduzi wa ofisi ya kisasa ya serikali ya mtaa wa Bwawani, Kata Mwananyamala, Kinondoni, alisema hakuna sababu ya viongozi hao kuingiza tofauti za kijinga ndani ya vyama vyao kwani hazitaleta maendeleo kwa Watanzania.
Pamoja na hilo, aliwataka viongozi hao kutotumia madaraka ya chama au rasilimali zake kwa maslahi yao, bali yatumike kwa manufaa ya wananchi kwa sababu kinachounganisha nchi ni wananchi wenyewe.
“Mosi, vyama vinakuja na kuondoka, awali kulikuwako na chama cha Tanu, Taa, na sasa CCM, hivyo kuweni makini na wananchi wenu katika kushirikiana ili asije ingia kidudu mtu baadaye na kuwachafulia au kuleta sifa mbaya kati yenu” alisema Hamad .
Mbali na hilo, aliwataka wanachi kushirikiana na viongozi wao pindi na baada kutoka madarakani kwa sababu ushirikaino na umoja wao utaleta mafanikio pamoja na maendeleo kwa Taifa, “sisi tunaamini kasi ya ushirikiano na maendeleo yataletwa na maelewano yenu wenyewe”.
Mwenyekiti wa eneo hilo, Mohamed Mkandu, alisema kuwa ofisi hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi wa eneo hilo, kwa kushirikiana na viongozi saba watatu kutoka chama cha CCM, na wane ni Cuf .
Aliongeza kuwa jengo hilo limegharimu Sh milioni 25, lakini bado linakabiliwa na changamoto ya lukuki ikiwemo ya miundombinu.
“Hadi sasa hakuna choo, barabara, wala mfereji wa kupitishia maji machafu, kijiografia eneo hili linapokea maji ya mvua mengi kutoka maeneo mbalimbali kutokana na mkondo wa maji, lakini hakuna eneo la kuyapitisha, hivyo kusababisha mafuriko mara kwa mara” alisema Mkandu.
Post a Comment