Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Mawakili 3 wahaha kumwokoa Lwakatare



JOPO la mawakili wanaomtetea Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare limelitaka Jeshi la Polisi kutoa dhamana kwa mshitakiwa huyo wakati akisubiri kufikishwa mahakamani.
Mawakili Tundu Lissu, Profesa Abdallah Safari na Peter
Kibatala walisema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya mshitakiwa huyo kutofikishwa kusomewa mashitaka yanayomkabili.

Akizungumza nje ya Mahakama, Lissu alisema tangu asubuhi jopo hilo lilikuwa linamsubiri Lwakatare, lakini hadi saa 9 alasiri hakuwa amefikishwa mahakamani hapo, kitendo ambacho walidai ni kinyume cha sheria kwa kuwa alitakiwa kufikishwa mahakamani saa 24 baada ya kukamatwa.

Lwakatare aliyekamatwa Machi 13 akituhumiwa kupanga mikakati ya kuteka na kutesa baadhi ya watu wakiwamo waandishi wa habari nchini, alitarajia kupandishwa kizimbani jana na kusomewa mashitaka.

Lissu alisema walitarajia Polisi watakuwa wameandaa hati ya mashitaka dhidi ya Lwakatare, ili wananchi wajue anakabiliwa na mashitaka gani, hata hivyo alisema sheria imekiukwa, kwa kuwa ndani ya saa 24 tangu akamatwe, alitakiwa kufikishwa mahakamani.

“Kutokana na kushindwa kumfikisha mahakamani, inaonesha wazi kuwa polisi hawajui kwa nini wanamshikilia Lwakatare na hawajui wanamshitaki kwa kosa gani, kwa kuwa mpaka sasa hawajamfungulia mashitaka ya kumshikilia Polisi,” alisema Lissu.


Alisema walijaribu kufuatilia kwa mpelelezi wa kesi hiyo ambaye aliwataka kumtafuta Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu ambaye awali alisema hana taarifa, kwa kuwa amesafiri na baadaye aliwaambia upelelezi haujakamilika.


Kwa upande wake, Profesa Safari alimwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuwaamuru askari watoe dhamana kwa Lwakatare, kwa kuwa anaumwa kisukari.
Lwakatare alikamatwa akituhumiwa kupanga mikakati mbalimbali, ikiwamo ya kuteka wanahabari na pia mbinu zinazotakiwa kutumiwa na vijana wa Chadema kujilinda.

Miongoni mwa watu ambao tayari wamevamiwa na kutekwa ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda ambaye amelazwa Afrika Kusini akipata matibabu baada ya kuvamiwa na kuumizwa na watu wasiojulikana.

Katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, anadaiwa kupanga mikakati ya kuteka Mhariri wa gazeti la Mwananchi, tukio ambalo halijatokea.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Polisi, Advera Senso, kigogo huyo wa Chadema anashikiliwa kutokana na picha hiyo iliyoko kwenye mtandao.

Katika picha hiyo, Lwakatare anaonekana akitoa maelekezo kwa mtu ambaye haonekani, namna ya kumfuatilia Mhariri wa Mwananchi anayedaiwa kuwa karibu na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto na ikiwezekana amdhuru, kwa vile anashiriki kuihujumu Chadema.

Hata hivyo, kwenye picha hiyo ya video mtu huyo anayedaiwa ni Lwakatare amejikita kutoa maelezo ya kufuatilia Mhariri huyo kama ana gari na mtu ambaye anapenda kuwa naye kwenye gari wakati anatoka kazini na hakuna sehemu anayotajwa Kibanda.

Senso akizungumzia hoja hiyo ya mawakili wa Lwakatare, alisema Polisi inafuata utaratibu na kuna vitu wanavikamilisha ambavyo vinazingatia taratibu za upelelezi za ndani ya Jeshi ambao hawawezi kuziweka hadharani.

“Hatuwezi kumwachia kabla ya upelelezi kukamilika, ukishakamilika tutamwachia akikamilisha masharti,” alisema Senso.

Wakati hayo yakiendelea Dar es Salaam, habari zilizopatikana jioni kutoka Iringa zilidai kuwa mtu mwingine ambaye jina lake linahifadhiwa alikamatwa jana mjini humo akihusishwa na harakati kama anazotuhumiwa nazo Lwakatare.

Hata hivyo, taarifa hizo zilikanushwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda akisema si kweli, ingawa alisema yuko safarini mkoani Kagera ambako anauguza ndugu yake.

“Huo ni uzushi tu, nimeletewa taarifa kutoka Iringa zikisema hakuna tukio kama hilo la mtu kukamatwa katika mazingira hayo,” alisema Kamanda Kamuhanda.


SOURCE::HABARILEO::

Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top