Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBIO za Urais Tanzania zinashika kasi baada ya sekeseke kubwa kuibuka katika Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA, kutokana na kudaiwa kuwa anayetajwa kuwania uongozi wa juu serikali, Edward Lowassa, kupewa Tuzo ya Amani.
Tuzo hiyo alikabidhiwa mwanasiasa huyo tishio hapa nchini, huku akidaiwa kuwa na mtandao wa aina yake, jambo linalomuwezesha kufanya kila anachotaka katika hali ya kumuweka juu kisiasa.
Tuzo hiyo ya Lowassa ilitolewa na Sheihke Mkoa wa Dar es Salaam, Shekhe Alhad Mussa Salum, huku akiitaja kama Tuzo ya Amani kutokana na mchango wa mwanasiasa huyo katika jamii.
Mchakato mzima juu ya tuzo hiyo, inaonyesha kuwa ni utaratibu wa kwanza kutolewa na viongozi hao wa dini, wakiwamo BAKWATA, huku ikiibua maswali lukuki kwa watu wanaofuatilia mambo ya siasa na wale wasiopenda dini zifungamane na siasa.
Wakati watu wakianza kujitafakari juu ya mbio za urais zinazoshika kasi siku hadi siku, Msemaji wa Kamati ya Vijana katika Baraza la Waislamu Tanzania BAKWATA, Sheikhe Said Mwaipopo alitangaza kujiuzulu wadhfa wake kwasababu ya suala la siasa kuingizwa kwenye mambo ya Mungu.
Kwa mujibu wa Mwaipopo, Tuzo ya Amani iliyotolewa kwa Lowassa ni ya kwanza katika maisha ya BAKWATA, jambo ambalo limetokana na kumsafisha yeye katika maisha yake ya siasa.
Gazeti la kila siku, lilichapisha habari hiyo likielezea kwa undani sakata la BAKWATA na Tuzo hiyo, ingawa Sheikhe Alhad mwenyewe alikanusha kumsafisha Lowassa kwa kumpa tuzo hiyo.
Aidha, habari za kujiuzulu Mwaipopo, Alhad mwenyewe alisema kuwa Msemaji huyo wa Vijana hajajiuzulu, bali alifukuzwa na Shekhe Mkuu wa Tanzania, Issa Shabaan Bin Simba.
Watu mbalimbali waliohojiwa juu ya sakata hilo, wengi wao walioonyesha kuwa na wasiwasi na tuzo hiyo, wakidai kulikuwa na haja gani ya kumpa Lowassa, mtu anayetajwa kuwa na lengo la kugombea Urais mwaka 2015.
Aidha, baada ya kupitia kwa undani suala hilo, limegundua kuwa kumekuwa na mzozo mkubwa ndani ya BAKWATA, huku baadhi yao wakishauri viongozi hao wa dini kujiweka pembeni na taasisi hiyo, kama wanataka kuvaa mavazi ya kisiasa na kupigia debe watu wanaowataka.
“Mimi ni Muislamu na ambaye naifuatilia kwa karibu mno taasisi hiyo ya Waislamu, jambo lililonifanya nibaini kuwa kulikuwa na sababu ya kisiasa iliyowafanya waibuni tuzo hiyo.
“Hata ukiangalia siku yenyewe ya kukabidhiana tuzo, tayari ilishapita kama walivyosema wenyewe kuzaliwa na Mtume Mohamed, ambaye kwa kawaida huadhimishwa kila Mfunguo Sita,” alisema mtu huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake gazetini.
Habari za kujiuzulu kwa Shekhe Mwaipopo, hazikupewa mkazo, licha ya kuzungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuhabarisha umma masuala yanayoendelea ndani ya taasisi hiyo wa Waislamu BAKWATA.
Kitendo hicho kilionyesha picha nyingine ya ndani kuwa kuna jambo lililojificha nyuma ya pazia, juu ya mambo yanayoendelea katika Taifa hili, hasa kwa wale wanaotaka Urais, hali inayowasumbua kuhaha katika nyumba za ibada au kwenye shughuli zinazohusisha mchanganyiko wa watu ili wafikishe hisia zao.
Sekeseke la kutajwa kuwania Urais kwa wanasiasa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), limewahusisha vigogo kadhaa, akiwamo Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli na Samuel Sitta, Waziri wa Afrika Mashariki na Spika wa Bunge aliyeenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Anne Makinda.
Wengine wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea Urais kwa tiketi ya CCM ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Dk Asha Rose Migiro na wengine wengi ambao kwa joto linaloendelea ndani yake.
Post a Comment