Ndugu zangu,
 
Hakuna wawili watembeao pamoja pasi na maelewano.
Ukiwaona wanadamu wawili wanatembea pamoja, basi, wana makubaliano. Ni watu waliopatana.

Kwenye kundi la watu wa mataifa tofauti ukimsikia Mtanzania anamtamkia Mtanzania mwenzake, tena kwa Kiswahili; ” E bwana inuka twende zetu!”, na Mtanzania huyo mwingine akabaki amekaa bila kushtuka, basi, utilie mashaka UTanzania wake.
Ndio, ” Inuka twende ni kwa waliogana”. Ni watu wenye kufahamiana. Ni ndugu.
Nimeanza kuingiwa na hofu kuwa Watanzania tumeanza kupoteana kama ndugu. ” Inuka twende’ yetu imeanza kuangaliwa kwa sura ya udini, ukabila na itikadi.
Hatujafika pabaya sana, lakini, tunakoelekea ni kubaya. Tumeshaziona ishara. Miongoni mwetu Watanzania tumeanza kuzisikia kaauli za ; ” Umewasikia jamaa zetu Wakrito? Umewasikia jamaa zetu Waislamu? Umewasikia jamaa zetu WaZanzibar? Umewasikia jamaa zetu wa Bara?……”
Hizi ni ishara za undugu unaosambaratika. Zamani sisi sote tulikuwa ni ndugu. Tulitembea pamoja, ishara ya watu tuliopatana.
Leo kuna Watanzania wanaoambiwa; ” E bwana wee, siku hizi nakuona unatembea na kuongea na wale jamaa zetu wa upande mwingine!”
Ndio, Watanzania tumeacha kuwa ndugu. Tunagawanyika kwenye mapande. Ni kwa kuzitazama tofauti za dini, kabila na itikadi.
Hatujafikia pabaya, lakini, tunakoelekea ni kubaya. Tukumbuke; ” Inuka twende ni kwa waliogana”. Watanzania tulishaagana. Tulishakubaliana. Tulijua tunakokwenda kama Taifa. Kama ndugu. Tumeanza sasa kusambaratika.
Tuinuke sasa twende kupambana na yote yenye kutugawa kama ndugu wa taifa moja. Tuna kila sababu, nia na uwezo wa kushinda mapambano haya dhidi ya ubaguzi wa aina zote.
Na hilo ni Neno La Leo.