TFF BADO YASISITIZA KUMUONA WAZIRI MUKANGARA
RAIS wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara kwa kukubali ombi la Shirikisho la
kutaka kukutana naye kwa mazungumzo na kumsihi asitishe hatua anazodhamiria
kuchukua hadi hapo kikao hicho kitakapofanyika.
Waziri Mukangara ameiagiza
TFF kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya katiba ifikapo tarehe 15 Aprili 2013
na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ifikapo tarehe 25 Mei 2013 na kwamba tamko la TFF
kutekeleza maagizo hayo liwe limetolewa katika muda wa siku tano zinazoishia
Jumatatu (Machi 11, 2013).
Katika barua pepe ambayo
amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, Rais Tenga ameeleza kuwa
alikwenda ofisini kwake tarehe 7 Machi 2013 kujaribu kumuona lakini akaambiwa
amesafiri, hivyo kuomba kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo
ofisini na hatimaye akakutana na Naibu Katibu Mkuu.
Katika barua hiyo pepe,
Rais Tenga ameeleza madhumuni ya kutaka kuonana na Waziri Mukangara kuwa ni
kwanza “kukushukuru kwa kukubali kuonana na ujumbe wa TFF ulioongozwa na mjumbe
wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw. Alex Mgongolwa, akiongozana na Katibu Mkuu wa
TFF, Bw. Angetile Osiah, jana tarehe 6 Machi 2013.
“Kukushukuru kwa kukubali
kukutana nasi tena siku ya tarehe 19 Machi, kwa ajili ya mazungumzo juu ya
maagizo yako.
“Kukuarifu
kuwa nimepokea maagizo yako uliyoyatoa jana kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya
Utendaji na kwa njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
Tenga, ambaye ni mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) aliondoka
jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda Marrakech, Morocco kuhudhuria kikao cha kamati
hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu
ukihusisha pia ajenda ya uchaguzi wa rais.
ROGASIAN Kaijage ameteuliwa
kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake, Twiga Stars
baada ya kocha wa zamani, Charles Boniface Mkwasa kujiuzulu katikati ya mwaka
jana.
Mkwasa, ambaye alikuwa
nyota wa Yanga na Taifa Stars, alijiengua kufundisha timu hiyo aliyoiongoza kwa
muda mrefu, baada ya Twiga Stars kuondolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania
tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika nchini
Equatorial Guinea.
Twiga ilipata bao muhimu
la ugenini jijini Addis Ababa ilipofungwa na wenyeji wao Ethiopia mabao 2-1,
lakini ikiwa na matumaini ya kutumia vyema bao la ugenini ilijikuta ikilala bao
1-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo wa marudiano na hivyo kukosa tiketi ya
kurudi tena kwenye fainali hizo.
Kaijage ambaye kwa sasa
anajihusisha na mradi wa vijana (grassroots) pamoja na programu nyingine za
kukuza vipaji zilizo chini ya TFF, aliteuliwa na Kamati ya Ufundi ya TFF kufanya
kazi hiyo na ameita kikosi cha Twiga Stars kwa mazoezi ya siku kumi kuanzia
Machi 10 hadi 23 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam.
Wachezaji walioitwa ni
Amina Ally (Lord Barden), Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini
(Zanzibar), Esther Chabruma (Sayari), Esther Mayalla (TSC Academy), Etoe Mlenzi
(JKT), Evelyn Sekikubo (Mbarahati Queens), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma
Mustafa (Sayari) na Fatuma Omari (Sayari).
Flora Kayanda (Tanzanite),
Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Maduka (Bujora), Hellen Peter (JKT),
Irene Ndibalema (TSC Academy), Maimuna Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite),
Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens), Mwanahamis Omari (Mburahati Queens) na
Mwapewa Mtumwa (Sayari).
Nabila Ahmed (Marsh
Academy), Nasiria Hashim (Zanzibar), Pulkeria Charaji (Sayari), Rukia Khamis
(Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida Boniface (Makongo Sekondari), Sophia
Mwasikili (Luleburgaz Gucu Spor, Uturuki), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia
Maarifa (Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati Queens).
YANGA, TOTO AFRICANS
KUUMANA DAR
MICHUANO ya Ligi Kuu ya
Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu)
kwa mechi mbili ambapo vinara Yanga watakuwa wenyeji wa Toto Africans kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi wa mechi hiyo
namba 135 atakuwa Andrew Shamba kutoka Pwani akisaidiwa na Abdallah Mkomwa na
Abdallah Rashid pia wote kutoka Pwani. Kamishna ni Salim Singano kutoka Tanga
wakati Mtathmini wa waamuzi ni Alfred Lwiza.
Nayo Polisi Morogoro
itakuwa mgeni wa Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es
Salaam. Azam katika mechi hiyo namba 136 na nyingine mbili zinazofuata itakuwa
bila kocha wake Steward John Hall ambaye Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu.
Charles Komba kutoka
Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 136 itakayochezeshwa na
mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani.
Ligi hiyo itaendelea tena
keshokutwa (Machi 10 mwaka huu) ambapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
utashuhudia mechi kati ya Simba na Coastal Union ya Tanga. Waamuzi wa mechi hiyo
ni Martin Saanya akisaidiwa na Jesse Erasmo na Vicent Mlabu wote kutoka
Morogoro.
RHINO, KANEMBWA ZASAKA
TIKETI VPL
KINDUMBWENDUMBWE cha Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) kinaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu) katika makundi yote
matatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu yakiwa kwenye
mechi za Rhino Rangers ya Tabora na Kanembwa JKT ya
Kigoma.
Timu hizo ndizo ziko
katika nafasi nzuri ya kupata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu
ujao kutoka kundi hilo la C. Tayari Mbeya City ya Mbeya na Ashanti United ya Dar
es Salaam zimeshapata tiketi za kucheza VPL msimu ujao kutoka kundi A na
B.
Rhino Rangers
itaikaribisha Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora,
wakati Kanembwa JKT itakuwa mgeni wa Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza.
Mechi nyingine za kundi C
ni Mwadui vs Polisi Tabora (Kambarage, Shinyanga), na Morani vs Polisi Mara
(Kiteto, Manyara). Mechi za kundi A ni Majimaji vs JKT Mlale (Majimaji, Songea),
Mkamba Rangers vs Mbeya City (Sokoine, Mbeya) na Polisi Iringa vs Burkina Faso
(Samora, Iringa).
Mshikeshike ya kundi B ni
Ndanda vs Ashanti United (Nangwanda Sijaona, Mtwara), Villa Squad vs Green
Warriors (Karume, Dar es Salaam), Polisi Dar vs Transit Camp (Mabatini,
Mlandizi) wakati Tessema na Moro United zitacheza Machi 10 mwaka huu Uwanja wa
Karume, Dar es Salaam.
Post a Comment