Daktari
bingwa wa macho kutoka China akimfanyia uchunguzi mtoto Fatuma juma
Mzee wa kijiji cha Uzini walipofika kutoa tiba na uchunguzi kwa wagonjwa
mbalimbali,huko katika kituo cha Afya Uzini Wilaya ya Kati Unguja.
Timu
ya Madaktari bingwa kutoka China wakiwa na wenzao wa Zanzibar wakiwa
katika picha ya pamoja,huko uzini Wilaya ya Kati Unguja. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Madaktari wa Kichina watoa huduma vijijini Zanzibar.Na Salum Vuai-Maelezo Zanzibar 16/03/2013.
WANANCHI wa
mbalimbali wa Wilaya ya Kati Unguja, wameelezea kuridhishwa kwao na
huduma za uchunguzi wa kiafya na tiba zinazotolewa na madaktari wa
kujitolea kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Wakizungumza na
gazeti hili jana wakati wataalamu sita wa magonjwa mbalimbali kutoka
China wakitoa huduma hizo katika kituo cha afya Uzini, wananchi hao
walisema, mpango huo ni mzuri kwani unawapunguzia mzigo wa kufuata
huduma mjini na kuchukua muda mrefu wakiwa nje ya vijiji vyao.
Hamad Juma,
mkaazi wa Mgenihaji, alisifu ubora wa huduma zinazotolewa na madaktari
hao, na kusema tiba zao ni mjarabu kwnai zimemsaidia sana kupata nafuu
matatizo ya macho yanayomkabili. “Kwa muda sasa
nimekuwa nikitibiwa na madaktari kutoka China katika hospitali kuu ya
Mnazimmoja badaa ya kuchomwa jichoni na kitu chenye ncha kali, na leo
wamekuja hapa nami nimefuata sawa zaidi”, alifahamisha.
Naye Mtumwa Jabu
Khamis, aliyempeleka mtoto wake mwenye matatizo ya kifua, alisema hatua
hiyo ni muhimu na inafaa ifanyike kila kipindi kifupi ili kuwafikia
wananchi walio wengi na ambao hawana uwezo wa kufuata huduma hizo mjini.
Akizungumzia ujio
wa madaktari hao, Sheha wa shehiya ya Uzini Vuai Mgeni Vuai, alisema
utaratibu unaofanywa na madaktari hao kupitia Wizara ya Afya, unawapa
faraja wananchi wa vijijini, kwa kuwaondoshea usumbufu wa maradhi
yaliyoficha na hatimaye kupatiwa tiba.
Alitoa wito kwa
wananchi wanapopata taarifa za kufikiwa na madaktari bingwa wa maradhi
mbalimbali, wasipuuze kwenda kufanyiwa uchunguzi, kwani huenda wakawa
wanaishi na maradhi ambayo hayajajitokeza.
“Siku hizi kuna
maradhi mengi, mengine hatuyajui mpaka tuchunguzwe, hivyo ni vyema
kunapokuwa na huduma kama hizi, wananchi wafike ili kuchunguzwa na
kuelezea matatizo ya kiafya waliyonayo ili yawahiwe mapema”, alisisitiza
Sheha huyo.
Mapema, kiongozi
wa timu ya madaktari hao Dk. Lu Jian Lin, alisema mpango huo
unaofadhiliwa na Serikali ya China, unalenga kuwasaidia wananchi wa
Zanzibar kuimarisha afya zao ili waweze kushiriki shughuli mbalimbali za
kiuchumi. Alieleza kuwa,
serikali ya nchi yake inatambua uhaba wa madaktari unaozikabili
hospitali na vituo vya afya vilivyoko vijijini, hivyo imeamua kwa
makusudi kuandaa programu hiyo ya kupeleka huduma katika maeneo hayo
Unguja na Pemba.
Aliwashauri
wananchi kuchukua tahadhari ili kujiepusha na maradhi mbalimbali, kwa
kula chakula bora, kufanya mazoezi ya mwili na kujenga utamaduni wa
kuchunguza afya zao kila baada ya kipindi maalum. Zaidi ya wananchi
250 kutoka shehia mbalimbali za Wilaya ya Kati, walipatiwa huduma hizo
kwa kupimwa na kutibiwa maradhi ya macho, pua, kifua, masikio magonjwa
ya akinamama na ya mifupa.
Post a Comment