MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26)
amekutwa amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business, iliyopo Mtaa
wa Jacaranda katikati ya Jiji la Arusha.
Benson Mollel wa
kwanza kushoto akiwa katika moja ya shughuli za UVCCM mkoani Arusha. Picha kwa
hisani ya Issa Michuzi
Mashuhuda wa tukio hilo walisema Mollel
alikutwa akiwa amekufa jana mchana na kwamba tukio hilo limezua hofu kwa wakazi
wa Jiji la Arusha, huku wakijiuliza chanzo cha kifo chake.
Kifo cha mwanasiasa huyo mchanga ambaye pia
alikuwa ni mfanyabiashara wa madini mkoani hapa, kimezusha maswali mengi wakati
wengine wakihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa na upande mwingine wakidai
ni masuala la kibiashara.
Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Arusha
ni jiji lenye hekaheka za kisiasa hasa ndani ya CCM ambapo Mollel alikuwa mmoja
wa vinara wake.
Polisi waliwasili hotelini hapo saa 8.00 mchana
na kuupakia mwili wa marehemu kwenye gari na kisha kuupeleka Hospitali ya Mount
Meru kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya wa Arusha (OCD),
Gilles Muruta akizungumza katika eneo la tukio alisema: “Tunachunguza tukio hili
ambalo ni la ghafla.”
Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM,
Martin Shigela alisema: "Tumepokea kwa masikitiko kifo cha Mollel japokuwa
sifahamu nini hasa kimejiri huko."
"Kuna rafiki yake alinipigia simu kuniarifu
kuhusu kifo hicho na nikawaambia kama UVCCM Taifa tupate maelezo kamili na tujue
nini cha kufanya. Iwapo familia itakuwa na mipango yoyote watutaarifu," alisema
Shigela.
Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa
madini mkoani Arusha walionekana nje ya hoteli hiyo baada ya taarifa za kifo
hicho kusambaa na wengine walishindwa kujizuia kisha kuangua vilio.
Miongoni mwao ni kada wa Chadema, James ole
Millya na diwani wa CCM Kata ya Mlangarini, Mathias Manga. Katibu Mwenezi wa CCM
wa Mkoa wa Arusha, Isaack Kadogoo ambaye pia alifika eneo hilo alisema kwamba
wamepokea taarifa za tukio hilo kwa mshtuko mkubwa.
Uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari
kulizungumzia kwa madai kwamba limefikishwa katika vyombo vya usalama.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya habari
ndani ya hoteli hiyo vilidai marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini
hapo akiongozana na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy na kuchukua chumba
namba 208.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment