By Basil Msongo, Nairobi
LEO ni leo, mamilioni ya Wakenya wanapiga kura kuamua hatma ya nchi yao.
Huu ni uchaguzi mkuu wa kwanza kufanyika tangu Kenya ipate Katiba
mpya. Wengi wao wanaamini kuwa machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi
wa mwaka 2007, hayatajirudia tena. Zaidi ya watu 1,000 walikufa katika machafuko hayo.
Uchaguzi huu ni wa kihistoria, si
tu kwa kuwa ni wa tano tangu
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi tangu nchi hii ipate Uhuru Desemba
12, 1963, bali kwa kuwa ni wa kwanza tangu Kenya ipate Katiba mpya na wa
kwanza baada ya machafuko yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Uchaguzi Mkuu wa Kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi nchini,
ulifanyika 1992, ukafuata 1997, 2002 na 2007 ambao uliendana na
machafuko ya kisiasa.
Wakenya sasa wanamchagua Rais wa Nne tangu Uhuru, ambapo Rais wa
Kwanza alikuwa Jomo Kenyatta, akafuatiwa na Daniel Arap Moi na kisha
Mwai Kibaki. Uchaguzi huu unakadiriwa kugharimu Sh bilioni 21.5 za Kenya na
kampeni za uchaguzi, zilimalizika juzi saa 12 jioni. Aidha shule zote za
Serikali zimefungwa kwa wiki moja kuanzia Alhamisi, ili kufanikisha
uchaguzi huo.
Kura sita
Wakenya wakiwemo wanaoishi Tanzania, Burundi, Uganda na Rwanda,
watapiga kura sita tofauti kwenye masanduku yenye kuonesha kilichopo
ndani tofauti na uchaguzi uliopita. Katika uchaguzi huo kwenye vituo 33,000 vya kupigia kura, wapiga kura
watamchagua Rais wa Kenya, magavana 47, maseneta 47, wawakilishi 47 wa
wanawake, wabunge 290 na wajumbe 1,450 wa mabaraza.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), vituo
vya kupigia kura vitakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi na vitafungwa saa
11 jioni. Kutakuwa na vituo 338 vya kujumlishia kura za majimbo, mabaraza na za
Rais. IEBC imesema kama hatapatikana mshindi wa nafasi ya Rais katika
uchaguzi wa leo, uchaguzi utarudiwa Aprili 10 mwaka huu na unatarajiwa
kugharimu Sh bilioni 6.
Jaji Mkuu wa Kenya, Willy Mutunga, amekaririwa akisema kuwa, maandalizi kwa ajili ya kumuapisha Rais mpya yamekamilika.
Kuna taarifa kwamba kama atapatikana mshindi wa nafasi ya urais
katika uchaguzi wa Machi 4, mrithi huyo wa Kibaki ataapishwa Machi 26
mwaka huu katika Uwanja wa Kasarani. Wakenya 14,352,545 wamejiandikisha
kupiga kura.
Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa,
watakaoruhusiwa kutumia haki hiyo
ya kidemokrasia ni raia wa nchi hiyo watakaokuwa Kenya siku ya uchaguzi.
Wenzao waliopo Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi watapiga kura katika
ofisi za balozi za Kenya kwenye nchi hizo.
Ulinzi waimarishwa
Jumatano iliyopita, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, David
Kimaiyo, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa polisi 99,000 watasambazwa
katika maeneo ya nchi hiyo kulinda amani wakati wa uchaguzi.
IEBC imesema hadi sasa waangalizi
2,400 wa kimataifa na wengine
20,000 wa nchini Kenya, wapo katika nchi hiyo kufuatilia uchaguzi.
Takribani waandishi wa habari 5,000 wa ndani na kutoka nje ya Kenya,
wapo nchini hapa kwa ajili ya uchaguzi huu.
Kuna wagombea wanane wa urais, lakini kwa mujibu wa mwenendo wa
kampeni, ushindani mkubwa upo baina ya Raila Odinga (68) wa Muungano wa
CORD na Uhuru Kenyatta (52) wa muungano wa Jubilee. Wagombea wengine wa urais ni Musalia Mudavadi (53) kupitia muungano
uitwao Amani, Martha Karua kupitia muungano wa NARC, Peter Kenneth (48)
wa muungano wa Eagle, Mohamed Abduba Dida (39) wa muungano wa Alliance
For Real Change (ARK), Paul Muite (68) wa Safina na Profesa James ole
Kiyiapi (52) kupitia Restore and Build Kenya.
Source: Mwananchi
Post a Comment