Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua) kimesema
kinaiburuza kortini Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu
(Sumatra), kwa madai kuwa hakikushirikishwa kwenye mchakato wa kuongeza nauli
za abiria.
Aidha, Chakua kimeitaka serikali kuuwajibisha uongozi
wa juu wa Sumatra kwa kuifuta na kuunda upya kwa madai kwamba
imeshindwa kusimamia maslahi ya wananchi wanyonge.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Mshauri wa chama hicho, Wilson Mashaka, alisema tangazo la kupandisha
nauli halikujengwa kwa dhana ya ushirikishwaji, kwani vikao vilivyofanyika kati
ya Septemba na Novemba, 2012, vilifanyika kwa kuwashirikisha wamiliki wa mabasi
lakini wadau muhimu kama Chakua hawakushirikishwa.
Alisema hata kigezo kilichotolewa na Sumatra kuwa
wamiliki wataleta mabasi mapya, hakina nguvu kwani hakuna uthibitisho wowote wa
mchakato wa kimkataba na hakuna taratibu zozote za awali zilizowahi kufanyika za
manunuzi ya mabasi husika ikiwa ni pamoja na muda wa kuwasili
kwake.
Mashaka aliongeza kuwa sababu nyingine iliyotolewa ya
kupandisha nauli kuwa mafuta yamepanda, hazina msingi kwani wananchi wa kawaida
hawatamudu gharama kubwa kwa mfano ya Sh. 75,000 kwa safari moja ya kwenda
mkoani Kigoma.
Alifafanua kuwa madai yanayotolewa na wamiliki wa
mabasi ya kupata hasara, hayana ukweli na kwamba yamekuwa yanaaminiwa na Sumatra
peke yake, kwani hakuna taarifa yoyote ya ukaguzi ya kimahesabu iliyowahi
kutolewa na wamiliki hao pamoja na kampuni zao ili
kuyathibitisha.
Mwenyekiti wa Bodi ya chama hicho, Hassan Mchanjama,
alisema mbali ya kuchukua hatua hiyo, pia chama chake kinakusudia kuzungumza na
baadhi ya wabunge ili wapeleke hoja binafsi bungeni kushinikiza kuvunjwa kwa
Sumatra.
Mchanjama alisema kupandishwa kwa nauli hizo kumekuja
kwa shinikizo la watu wachache ambao wamewarubuni viongozi wa Sumatra kwa
maslahi yao binafsi.
Mchanjama alimtaka Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison
Mwakyembe, kuingilia kati ili kuwanusuru wananchi wengi ambao hawana
uwezo.
SOURCE::NIPASHE::
Post a Comment