Picha juu na chini ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Makampuni ya Maji na Umeme { Botjheng Water na Megtron } ya Afrika Kusini pamoja Uongozi wa Wizara ya Ardhi , Makazi, Maji na Nishati aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mwakilishi wa Makampuni ya Botjheng Water na Megatron ya Afrika Kusini Bw. Dean Hiran akiwa pamoja na Viongozi wa Makampuni hayo wakizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na Uongozi wa Makampuni ya Maji na Umeme { Botjheng Water na Megatron } ya Afrika Kusini mara baada ya kumaliza mazungumzo yao. Picha nan Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Uongozi wa Makampuni yanayojishughulisha na masuala ya Maji Safi na salama ya Botjheng Water na Megatron kutoka Nchini Afrika Kusini umeamua kutoa fursa kwa Zanzibar katika uwekezaji wa miradi yao ya Maji na Umeme ili kuviwezesha Visiwa vya Zanzibar kutekeleza miradi yake ya Kiuchumi kwa ufanisi.
Mkurugenzi wa fedha wa Kampuni ya Maji Bw. Hardus Hattingh ameeleza hayo wakati ujumbe wao ulipokutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, makazi Maji na Nishati sambamba na idara zilizohusika na miradi hiyo chini ya uenyekiti wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bw. Hardus Hattingh amesema ujio wao Zanzibar ni kuangalia mahitaji halisi ya Huduma za maji pamoja na kufikiria mbinu zinazoweza kusaidia kitaalamu kupunguza tatizo hilo.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Maji ya Botjheng Water ya Afrika Kusini amefahamisha kwamba Kampuni yao imelenga kusaidia Mataifa yenye matatizo ya upungufu wa huduma hizo wakiangalia zaidi Nchi za Bara la Afrika.
Naye Mshauri wa Fedha katika Kampuni ya Umeme ya Megatron kutoka Nchi hiyo ya Afrika Kusini Bw. Johan Oelofse ameeleza kwamba Taasisi yao iko tayari kuwekeza Zanzibar wakati wowote kutegemea mahitaji watakayoelezwa.
Bw. Yohan ameeleza kuwa Kampuni ya Megatron iko tayari na uwezo kamili wa kuendeleza miradi ya umeme ambayo mengine imeshaanzishwa katika baadhi ya Mataifa Barani Afrika.
Nao kwa upande wao Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, makazi, Maji na Nishati Nd. Al- Khalil Mirza pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Dkt. Garu wamesema matumizi ya huduma ya maji yataendelea kuongezeka kufuatia kutanuka kwa sekta ya uwekezaji hapa Nchini hasa katika miradi ya Utalii.
Wamesema Mamlaka ya maji inahitaji kuwa na vianzio vingine zaidi vya maji ili huduma ya maji ifikie katika asilimia ya kiwango kinachohitajika hasa ndani ya eneo la Mji ambalo bado lina upungufu wa huduma hiyo.
“ Tunaangalia zaidi kuelekeza mipango yetu katika kuhakikisha eneo la Mji wa Zanzibar ambalo limekabiliwa na idadi kubwa ya wakazi wake linaondokana na upungufu huo wa huduma ya Maji safi na salama . Amefafanua Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Dkt.Garu.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema juhudi za ziada zinafaa kuchukuliwa katika kuona huduma za maji safi ndani ya manispaa ya Zanzibar zinapatikana kwa kiwango kinachoridhisha.
Balozi Seif amesema Mkoa wa Mjini Magharibi hivi sasa una idadi kubwa ya wakaazi wake inayofikia Laki 5.9 sawa na asilimia 46% ya wakaazi wote wa Visiwa vya Zanzibar wapatao Milioni 1.3.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuomba Ujumbe wa Makampuni hayo ya Maji na Umeme kutoka Nchini Afrika Kusini kuitumia fursa ya upungufu wa huduma hizo Zanzibar katika kuwekeza vitega uchumi vyao.
Post a Comment