Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Bw. Cosmas Mwaisobwa akisisitiza jambo mbele ya
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokua akitangaza kuhusu kuanza
kupokea maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuanzia 1 Mei,
2013.
---
Na Mwandishi wetu, Dar es
Salaam
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetangaza
kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa wafunzi wanaotarajiwa kujiunga na Vyuo Vikuu
pamoja na wanafunzi wanaoendelea kwa mwaka wa masomo 2013/2014 kuanzia Mei 1,
2013.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi hiyo Bw. Cosmas
Mwaisobwa amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa maombi
ya mikopo yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia anuani ya http://olas.heslb.go.tz
Amesema vipeperushi maalum vyenye maelezo ya jinsi ya
kuomba mkopo kwa njia ya mtandao vinapatikana kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu,
ofisi za Elimu za Wilaya,watoa huduma ya Intaneti, Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo
na Ofisi za Bodi ya Mikopo za Kanda.
Pia alisema maelezo haya ya mikopo yanapatikana kwenye
tovuti ya bodi ambayo ni: www.heslb.go.tz
Waombaji wapya wanatakiwa kulipa ada ya maombi ya
mikopo ya shilingi 30,000/- huku wanafunzi walio katika mwaka wa masomo wa tano
au wa sita wa masomo wataendelea kulipa ada ya maombi ya shilingi
10,000/-.
"Wanafunzi wa mwaka wa pili, tatu na nne ambao walilipa
ada ya maombi ya shilingi 30,000/- katika miaka ya masomo ya 2009/2010,
2010/2011 na 2011/2012 hawatakiwi kulipa tena ada hiyo ya maombi ya mikopo,"
alisema.
Bwana Mwaisobwa amesema mwombaji wa mkopo huo anapaswa
kuwa na sifa ambazo zimetajwa katika kifungu cha 17 cha Sheria Na 9 ya mwaka
2004 ambazo ni pamoja na na mwombaji kuwa raia wa
Tanzania.
Ametaja sifa nyingine kuwa ni kudahiliwa katika chuo
cha elimu ya juu, kutokuwa na njia nyingine ya kugharamia elimu ya juu, kufaulu
mitihani ya mwaka uliotangulia kwa waombaji wanaoendelea na masomo pamoja na
kuwa mhitaji.
"Bodi inasisitiza kwamba waombaji wa mikopo wazingatie
muda uliopangwa na pia kufuata kwa umakini taratibu zote zilizoainishwa katika
uombaji wa mikopo," alisema na kusisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa ziada baada
ya muda uliopangwa kupita.
Mwisho wa kupokea maombi hayo ya mikopo ni 30 Juni
2013.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu kwa mwaka wa masomo wa
2012/2013 iliwapatia mikopo wanafunzi wapatao 94,703
Post a Comment