WANASIASA wawili vijana
ambao wamekuwa katika vita ya maneno na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, kuhusu madai waliyoyatoa kuwa
anawindwa kuuawa, mwishoni mwa wiki iliyopita, walijitokeza katika ofisi za
Mtanzania Jumatano na kufunua siri na matukio ya utesaji raia na mauaji ya
kinyama ambayo yamekuwa yakitokea kwa nyakati tofauti kwenye shughuli za
kisiasa hapa nchini.
Wanasiasa hao, Juliana
Shonza na Mtela Mwampamba, ambao wamefanya mahojiano ya ana kwa ana na gazeti
hili, walisema madai waliyoyatoa awali kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod
Slaa, alitajwa na kada wa chama hicho, Ben Saanane, kuwa alimtuma amuwekee sumu
Zitto kwa lengo la kumuua ni ya kweli kwa sababu walimkamata akiwa nayo na
alikiri jambo hilo na kumuomba msamaha Zitto kwa kitendo
hicho.
Walidai, mbali na tukio hilo
ambalo baada ya kuliibua limegusa hisia za wengi na kuzua mijadala mikali, yapo
matukio mengine ya mauaji na majaribio ya kuua, ambayo yamekuwa yakiratibiwa na
Chadema kwa lengo la kuwagombanisha wananchi na Serikali.
Shonza na Mwampamba walisema kuwa wapo tayari
kutoa ushuhuda wa matukio hayo mahali popote watakapohitajika na walipoulizwa ni
kwa nini baada ya kubaini kuwepo kwa vitendo hivyo, hawakutoa taarifa kwa vyombo
vya sheria au taasisi za ulinzi na usalama, walisema mlengwa mkuu katika matukio
hayo ambayo yalikuwa yakisababisha madhara kwa watu wengine hakuwa tayari siri
hiyo kuanikwa.
Akizungumza mbele ya jopo la waandishi wa habari
wa gazeti la Mtanzania Jumatano, Shonza alidai kuwa, yeye na baadhi ya vijana
wenzake waliokuwa wakiunda kundi Patriotic Movement, walimnasa Saanane akiwa na
sumu hiyo katika Hotel ya Lunch Time iliyoko Ubungo, Dar es Salaam, ambao awali
alidai kuwa ni dawa ya Panya, lakini alipobanwa alieleza kuwa ilikuwa sumu
ambayo hakuitaja jina na kwamba alipewa na Dk. Slaa ili amuwekee Zitto kwa
sababu alikuwa akimsumbua sana.
Alisema, sumu ingewekwa kwenye kinywaji cha
Zitto akiwa katika kikao hicho, lakini hatua yake ya kutohudhuria ndiyo
iliyomuokoa.
Shonza alisema, baada ya Saanane kukiri kuwa
alitumwa na Dk. Slaa kumuwekea Zitto sumu, walimtaarifu wakati akiwa Marekani na
aliporudi alikutana na kuwataka jambo hilo wasilifikishe polisi kwa sababu
lingekivuruga chama na kwamba kwa sababu alikwishawajua wabaya wake
atajilinda.
Alimtuhumu Zitto kwa kuficha ukweli na kumwita
kiongozi mwoga, huku akimuonya kuwa iwapo ataendelea na tabia ya kukanusha
ukweli atamuumbua hadharani kwa sababu anamjua vizuri.
“Ameongea hayo kwa sababu ana tabia ya kushindwa
kuthibitisha kuwa ana uwezo wa kujiongoza yeye mwenyewe pamoja na wengine. Mtu
wa maslahi Zitto, anatafuta huruma ya Chadema baada ya kuona amepukutika kisiasa
kutokana na kukosa msimamo kiuongozi na hawezi tena kutetea wanyonge, ni mtu
mwoga.
Mnapokuwa kwenye mapambano yeye yuko tayari
kurudi nyuma, lakini huruma hiyo asitegemee kuipata Chadema, labda akubali
kushaurika na kubadilika kama kweli anataka kutetea maslahi ya wanyonge,”
alisema Shonza.
Aidha, Shonza alimshambulia pia Saanane kwa
kudai anakataa ukweli anaojua, kwa sababu tukio la kukamatwa kwake akiwa na sumu
lilitokea akiwa mbele ya zaidi ya mtu mmoja na kusisitiza kuwa kada huyo wa
Chadema anatumika na viongozi wa juu wa chama hicho kuwashughulikia baadhi ya
wanachama wasiotakiwa.
Katika hili, Shonza alidai zaidi kuwa Saanane ni
mtu hatari kwa sababu ndiye aliyeanzisha kundi la PM7, ambalo lilikuwa na lengo
la kumpindua Mbowe kutoka kwenye wadhfa wake wa uenyekiti, lakini baadaye
aliwageuka wenzake na kusababisha kufukuzwa katika chama.
“Saanane alikuwa anatumika kutuingiza mkenge.
Alianzisha kile alichokiita mapinduzi, Patriotic Movement (PM7), lengo lilikuwa
Pindua Mbowe, sisi hatukujua.
Tulikuwa saba katika PM7, Saanane alifanikiwa
kutuchezea akili na alikuja na 'nick names' (majina bandia) yake. Mimi akaniita
Benanzir Bhuto, Mchange akaitwa Mdude, Mwampamba- Joseph Kony, Zitto- Dogo kama
tulivyozoea kumuita na yeye mwenyewe akajiita Cobra, wapo na wengine sikumbuki
vizuri majina yao hapa.
Sisi vijana wakati mwingine tunatumika vibaya,
sisi hatukujua ana ajenda yake, tulivyoshtuka akatukana na ndiyo yakatokea hayo
yaliyotokea,” anazidi kueleza Shonza.
Mwampamba
Kwa upande wake Mwampamba ambaye aliandamana na
Shonza katika ofisi za Mtanzania Jumatano, alidai kushangazwa na hatua ya Zitto
kukanusha kauli ya Shonza iliyokuwa ikieleza namna Saanane alivyokamatwa akiwa
na sumu aliyokuwa ametumwa kumuwekea Zitto.
Alisisitiza kuwa, Zitto anajua mipango
inayopangwa ndani ya Chadema kwa ajili ya kummaliza na alimtaka aache tabia ya
kufunika kombe ili mwanaharamu apite, kwa sababu inaweza kuwa na athari mbaya
kwake.
“Zitto anajua mpango mzima wa kutaka kumalizwa
kwa sumu na Ben Saanane, baada ya kutumwa na Dk. Slaa kwa sababu tulimwambia na
alithibitisha mwenyewe pale Saanane alipomuomba msamaha, sisi ndiyo tulimbana
Saanane hadi akaeleza ukweli wa mipango yao ya mauaji.
“Leo namshangaa anavyojikomba eti haamini kuwa
anaweza kuuawa na hao jamaa. Lakini kwa Ben Saanane, namtaka atambue kuwa
Ludovick alipokamatwa alikanwa na Dk. Slaa wakati ndiye alikuwa kijana wake
mpenzi, sasa na yeye ipo siku atakimbiwa.
“Zitto anatakiwa aache tabia ya kufunika funika
mambo, ajue nimemwokoa sana katika mambo mengi, mfano mauaji ya Morogoro
yaliyopangwa na Chadema yalimlenga Zitto, alikuwa atolewe kafara. Yule muuza
magazeti aliyepigwa risasi Morogoro akafa, siku hiyo ilikuwa afe Zitto,” alidai
Mwampamba.
Alipoulizwa ni kwanini viongozi wa Chadema
wanataka kumuua Zitto, alisema ni kwa sababu ya uhusiano mbaya baina yake na
vigogo hao ambao chanzo chake ni hatua ya kutaka kugombea urais na kutomuunga
mkono Dk. Slaa katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2010.
“Zitto hana uhusiano mzuri na viongozi wa juu wa
Chadema. Nia yake ya kutaka kugombea urais hawaipendi, inawaudhi sana na amekuwa
akitofautiana nao kwa mambo mengi, anajua kuwa anawindwa ndiyo maana hata
oparesheni za M4C hashiriki.
“Mimi nilikuwa Chadema na nilikuwa karibu sana
na Zitto, najua nini kilikuwa kinaendelea juu yake na najua baadhi ya mambo ya
Chadema. Ninaijua mipango ya mauaji ya Chadema. Zitto aliwahi kuwekewa sumu
Bagamoyo wakati wabunge wa chama hicho walipokuwa kwenye mkutano wao
huko.
“Alinusurika kufa. Alipona baada ya sumu hiyo
kutolewa mwilini mwake. Waliiflashi.” Alidai Mwampamba.
Alidai kuwa Zitto alipata kunusurika katika
ajali ya gari wakati akitokea Bagamoyo kuelekea Iringa, baada ya gari alilokuwa
akitumia kulegezwa nati zinazofunga tairi. Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada
ya Zitto na Mbowe kutupiana maneno makali kwenye mkutano
Kauli ya Saanane
Akizungumza na Mtanzania Jumatano jana kupitia
simu yake ya kiganjani, Saanane alisema madai yaliyotolewa na Shonza na
Mwampamba dhidi yake siyo ya kweli, kwa sababu wanayodai kuwa walimkamata akiwa
na sumu, hakuwa nao.
Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu zake, siku ya
Desemba 5, mwaka jana, alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akikutana na
wanaharakati na baadaye jioni alikwenda harusini.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo alipata kukutana
na Shonza na Mwampamba katika Hotel ya Lunch Time, Saanane alisema amepata
kukutana nao mara kadhaa kwa ajili ya kupanga mikakati ya PM7, ambayo alishiriki
kuianzisha lakini aliachana nao baada ya kubaini walikuwa wakiitumia kwa malengo
mabaya.
Mtanzania Jumatano lilipombana Saanane aeleze
mikakati waliyokuwa wakiipanga yeye na wenzake katika PM7, alisema ilikuwa ya
siri na vikao vyao vilikuwa vya siri kutokana na hofu ya kufikiriwa vibaya na
viongozi wa chama iwapo wangebainika wanajihusisha na kundi hilo.
Alipoulizwa kama anafahamiana na Zitto na wapi
amekwishakutana naye, alisema anamfahamu na amekuwa akikutana mara kwa mara huku
akishangaa tamko lake kwenye mitandao ya kijamii lilikokuwa likieleza kuwa,
hamfahamu na hata akimuona anaweza kupishana naye.
Hata hivyo, baadaye Saanane aliomba anuani ya
barua pepe ya Mhariri wa gazeti hili na kumtumia barua ya kumtaka amuombe radhi
kwa kuandika habari ya uongo iliyokuwa ikieleza madai ya masharika wake
wanaomuhusisha na tuhuma za kutumwa kumuwekea sumu Zitto, pasipo kumtafuta Zitto
mwenyewe kuzungumza hata neno moja
Vituko vya Dk. Slaa
Dk. Slaa alipotafutwa kwa simu yake ya kiganjani
na kuulizwa kuhusu madai hayo, alianza kuporomosha matusi mazito huku
akilituhumu gazeti hili kutoa nafasi ya kuandika habari zinazowagusa viongozi wa
Chadema badala ya kuandika habari za maendeleo.
“Sina muda wa kujibu maswali hayo… hayana
msingi…tuhuma hizo hazijadiliwi kwenye magazeti……ni masuala ya kijinga…pumbavu
kabisa. Acheni upumbavu bwana. Nina mambo mengi ya msingi ya kitaifa ya
kushughulikia kuliko haya madai ya kipumbavu.” Aling’aka Dk. Slaa.
Hata gazeti hili lilipomsihi awe mtulivu ili
aweze kutoa ushirikiano, aliendelea kufoka huku akiporomosha matusi zaidi kabla
halijaagana naye na kukata simu.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe simu yake iliita muda wote bila majibu na hata
Zitto.
Post a Comment