Msaidizi wa zamani wa
Padri (Katekisita) katika Kigango cha Kanisa Katoliki Kijiji cha Mkwajuni,
Florian Mwamosi (70) amekufa baada ya kuzikwa akiwa hai katika kaburi moja na
mtu anayedaiwa kumuua kwa njia ya kishirikina.
Tukio hilo limetokea
katika Kitongoji cha Maweni kijijini hapo wilayani Chunya mkoani
Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mbeya Diwani Athumani alikiri kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa lilitokea
saa 9:00 mchana katika kijiji hicho cha Maweni Mkwajuni wilayani
Chunya.
"Marehemu aliuawa na
wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na mawe kwa tuhuma za kuhusika na uchawi
na kusababisha kifo cha Peter Robert," alisema.
Kamanda Athumani alisema
kuwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea na kwamba wahusika wote wa
tukio hilo wamekimbia na kuzihama nyumba zao, hivyo polisi wanaendelea na msako
wa kuwatia mbaroni watuhumiwa na kwamba tayari kaburi hilo limefukuliwa jana
kutenganisha maiti hizo.
Mashuhuda wa tukio hilo
walisema kuwa marehemu huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kwa ushirikina aliwahi
kuwa Katekista wa kigango hicho hadi mwaka 2007.
Wameeleza kuwa Mwamosi
alikwenda kuhudhuria mazishi ya Peter Robert (28) katika kitongoji hicho cha
Maweni, baada ya kufuatwa nyumbani kwake na watu wakitaka aende kwa sababu yeye
ni mmoja wa wazee wa mila katika kitongoji hicho.
"Bwana Mwamosi alikuwa
akituhumiwa kwa uchawi kwa muda mrefu na wenzie wawili, hivyo alipofika
makaburini ilianza minong'ono ya watu na huku wengine wakiguna na ndipo
alipoombwa aingie kaburini kwa ajili ya kupokea jeneza lililobeba mwili wa
marehemu Peter Robert," alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyejitambulisha
kwa jina moja la Joseph.
Alisema kuwa baada ya
kuingia kaburini akiwa na watu wengine watatu wenzake walitoka kwa haraka na
kumwacha Mwamosi peke yake ndipo kundi la watu waliokuwa eneo hilo la makaburi
walianza kumshambulia kwa kumpiga mawe huku wakimwamuru akae
chini.
Shuhuda huyo alisema
kuwa baada ya kukubali kukaa chini akiwa ndani ya kaburi hilo, walianza kumfukia
na alipofukiwa nusu ya mwili wake waliingiza jeneza la marehemu Peter na
kuliweka juu yake na kuanza kulifukia kaburi hilo.
"Baada ya kukaa chini
ndani ya kaburi hilo ndipo walianza kumfukia kwa udongo na baadaye wakachukua
jeneza la marehemu na kuliweka juu yake, kisha kumfukia na udongo na taratibu za
mazishi ziliendelea kwa ajili ya marehemu Peter,"alisema.
Alidokeza kuwa chanzo
cha tukio hilo ni marehemu Robert kuugua ghafla tumbo, ndipo ndugu zake
walipoamua kumpeleka kwa mganga wa jadi kwa ajili ya kupata matibabu na baada ya
siku tatu alifariki dunia.
:CHANZO
MWANANCHI
Post a Comment