Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa zaidi ya wiki nne umebaini
kwamba kazi ya kubomoa nyumba hizo inaweza kuanza wakati wowote ingawa
kuna changamoto kubwa kwani baadhi ya nyumba hizo ni za vigogo wenye
madaraka makubwa serikalini au ndani ya vyama vya siasa. Habari zaidi
zinadai kwamba baadhi ya vigogo hao wamekimbilia mahakamani kufungua
kesi ya kupinga nyumba zao zisiguswe wakati wengine wamekua wakitoa
vitisho kwa waliopewa mamlaka ya kuzibomoa.(Picha na GPL)
Wananchi hao wamemueleza waziri kwamba nyumba hizo zimeziba mkondo wa
maji katika baadhi ya mito inayoingia baharini, hivyo kusababisha maji
kuhama na kuelekea kwenye nyumba zao na daraja la eneo la Malecela
kusombwa na maji hivyo kusababisha magari kutopita. Walidai kuwa
nyumba nyingi zimejengwa katikati ya mto na wengine wamejaza vifusi
kando ya mto unaopita karibu na nyumba zao, hivyo kusababisha mkondo wa
maji kwenda kwa wananchi.
Vyanzo vyetu vya habari vinadai kwamba baadhi ya nyumba hizo zina hati
zilizopatikana serikalini wakati zingine wamiliki wao walivamia maeneo
hayo na kuporomosha maghorofa makubwa. Kutokana na ujenzi huo holela,
wakazi wa Kawe kwa Malecela waliamua kumwandikia barua Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakitoa
malalamiko juu ya ujenzi huo.Barua hiyo ambayo gazeti hili lina
nakala yake iliyoandikwa Februari 20, mwaka huu iliel eza kwamba ujenzi
wa nyumba hizo umekuwa ni kero kubwa kwani zimejengwa katika mkondo wa
maji hivyo mvua inaponyesha inasababisha mafuriko kwa wananchi wengine.
“Hivi sasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanashindwa kutembelea
ufukwe wa bahari kutokana na baadhi ya nyumba kuziba njia na mbaya zaidi
waliojenga kando ya mkondo wameharibu mikoko,” imesema sehemu ya barua
hiyo. Waliendelea kusema kwamba vigogo hao ambao ni wavamizi baadhi
yao wamekuwa wakitembea na bastola hadharani na kuwatishia maisha
wale wanaodiriki kuzungumzia ujenzi wanaoufanya katika maeneo hayo.
Wananchi
hao wametishia kuwa endapo hawatasikilizwa wataenda Ikulu kumuona Rais
Jakaya Kikwete. Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Hifadhi ya Mazingira
nchini (NEMC), Ignas Mchallo alisema: “Wote
waliojenga katika maeneo hayo watahamishwa kwa kufuata sheria kwani
kuna wengine waliojenga kabla ya sheria ya mazingira ambayo inataka
kuwepo kwa nafasi ya mita 60 toka mtoni au ufukweli,” alisema Mchallo.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka alisema kwamba nyumba 73 zilizojengwa kwenye fukwe za Bahari
ya Hindi, zitavunjwa na akazitaja kuwa ziko kwenye fukwe za Kawe, Mbezi
na Msasani na kwamba ingawa zilijengwa kihalali baada ya kupewa hati,
lakini sheria mpya hairuhusu nyumba hizo kuwepo.
Post a Comment