Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MBUNGE WA CHADEMA ASHUKIA BARAZA LA MAWAZIRI WA CCM.

 


Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, ameshangazwa na Baraza la Mawaziri kwa kushindwa kumshauri Rais Jakaya Kikwete, ambaye anahofiwa kudanganywa kuiruhusu Kampuni ya Kimarekani ya Mosanto inayozalisha mbegu za vyakula zinazosababisha watoto kuzaliwa taahira.
Amesema kampuni hiyo ambayo ilifukuzwa nchini India na kupigwa marufuku katika nchi za Ulaya, ikiwamo Ufaransa
na Marekani, imekwishaingia nchini na kupokelewa na serikali kwa mikono miwili na imekwishagawa mbegu za pamba.
“Baraza la mawaziri ndiyo washauri wa Rais, inawezekana Rais akaingizwa choo cha kike na hao mabeberu. Anadanganywa kwa maneno matamu matamu, kama Marekani wamemkataa mwenzao, Tanzania kwanini tunamkubali, tuna mpango gani wa kuwasaidia hawa wakulima?” alihoji Mdee.
Alisema mbali na kusababisha watoto kuzaliwa taahira, sababu nyingine ya kampuni hiyo kupigwa vita duniani kote, ni kuwafanya wakulima wadogo wadogo kuwa wategemezi wa mbegu za mabeberu.
“Naiomba serikali hawa mabeberu wana msingi wa kuingia katika system (mfumo) kwa njia ya rushwa kwa kutumia fedha walizo nazo kwa kuwarubuni viongozi walio madarakani. Nyie wengi wenu mko above fifty (zaidi ya miaka 50) yaani mmechoka mmenielewa, msiwaharibie kizazi hiki,” alisema Mdee.
Mdee alisema hayo bungeni jana wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2013/2014.
“Mimi nadhani kuwa kipindi cha kupigana fiksi fiksi hapa kina wakati wake. Wakulima wa Tanzania wamechoka ngonjera na serikali imekuja na mpango wa Sagot (Mpango wa Kukuza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania). Tunaambiwa kuwa mwaka jana serikali ilitenga Sh. bilioni 16, lakini zimetoka Sh. bilioni 1.7 tu,” alisema Mdee. Alisema katika Sagot kuna wadau mbalimbali, zikiwamo serikali za Marekani na Vietnam, lakini jambo linalotisha ni aina ya kampuni 17, ambazo zimeingia katika mpango huo kama wabia.
“Mimi naamini serikali mnasoma. Siamini kama hamfahamu kinachoendelea duniani. Hakuna mtu ambaye hafahamu kampuni kubwa ya kuzalisha mbegu ya Monsanto ambayo ni kampuni ya Marekani,” alisema Mdee na kuongeza:
“Mwaka jana kwenye mkutano wa G8 (mkutano wa nchi nane tajiri duniani), kampuni hii inaji-commit dola bilioni 50 kusaidia kufufua kilimo Afrika. Najaribu kufikiria katika fedha hizo ambazo tuna uwezo wa kuzitengeneza wenyewe Tanzania tutapata kiasi gani,” alisema.
Aliongeza: “Ukienda India leo huyu Monsanto, ambaye tangu mwaka 49, amefukuzwa kwa sababu amewafukarisha wakulima wadogo wadogo wa India wanaoitwa `untouchable'.”
“Ukisoma Sagot kwa kina, inamuangalia sana mkulima mkubwa halafu mkulima mdogo anawekwa pembezoni asaidiwe na huyu mkulima mkubwa. India wamewafukuzwa kwa sababu kwanza inamfanya mkulima kutokuwa na haki ya kurudia mbegu wakati wa upando ujao.”
Alisema Ufaransa inasema mbegu hizo husababisha sumu, ambayo inawafanya watoto wanaozaliwa kuwa taahira.
“Argentina amepigwa marufuku. Wala huhitaji kutumia nguvu kubwa. Una google tu. Utaona vielelezo kwenye Youtube,” alisema Mdee na kuongeza:
“Ukienda Peru Monsanto amefukuzwa kwa sababu mbegu za viini tete anazozalisha hazimsaidii mkulima. Mnakuja na maneno matamu matamu, lakini mnatuingiza kaburini.”
Alisema kuna taarifa kwamba wakulima wameanza kuzitumia mbegu hizo katika zao la pamba.
Mdee alisema wakulima wa pamba ambao sasa wamekuwa wakilia watakuja kulia zaidi.
“Mwekezaji ana eka 10,000, mkulima mdogo ana eka moja, unamuondoa umaskini ama unamzidishia umaskini? Hao ndiyo wawekezaji wakubwa. Wanakuja na mbegu za sumu zinasambaa kwa hao wakulima wadogo wadogo,” alisema Mdee na kuongeza:
Badala ya kutuletea mipango isiyokuwa na kichwa wala miguu, watuambie katika wilaya wameelekezaje mashamba kwa kujua wanawake wanastahiki ya kiasi gani? Watuambie wilaya fulani ina kitu gani ambacho kinashikika na si kututolea mifano hapa.”
Aidha, Mdee alisema serikali haiko makini na haina dhamira ya dhati kuhakikisha matatizo yaliyo katika kilimo ambacho kinawaajiri watu wengi, yanapatiwa suluhu.
Mdee alisema mwaka jana serikali ilitenga Sh. bilioni 120 kwa ajili ya maendeleo, lakini kwa kuonyesha kuwa haitembei katika maneno yake ni Sh. bilioni 14 tu ndiyo fedha za ndani na fedha za nje ni Sh. bilioni 106.
Alisema hadi kufikia Machi 19, mwaka huu, zimetolewa Sh. bilioni 22.9 sawa na asilimia 19 tu.
“Hapa tunapiga ngonjera kuwa tunamsaidia mkulima, lakini swali ni kwamba, kweli tunachokisema ndicho tunachokifanya?” Alihoji Mdee.
Alisema serikali ilisema bajeti ya kilimo itafikia asilimia 10 mwaka 2015, lakini sasa hivi kilimo kinachelea na kinakuwa kwa asilimia moja tu.
“Tunaambiwa uwekezaji unaongezeka, lakini kwa tafiti ambazo zimefanywa, zinaonyesha fedha nyingi ambazo zinaongezeka ni za matumizi ya kawaida, fedha za maendeleo hakuna ongezeko ambalo lina tija,” alisema.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliitaka serikali kuweka maji ya uhakika katika Chuo cha Kilimo kilichoko Kasulu, Mkoa wa Kigoma kwa kuwa wanachuo na walimu wanapata shida ya maji.
Pia alilalamikia utaratibu wa usambazaji wa mbegu za kupandia za Minjingu Mazao na kusema mbolea hiyo imekuwa ikisambazwa nje ya wakati.
Kutokana na hali hiyo, alisema kama serikali itaendelea kusambaza mbolea nje ya wakati, atawahamasisha wakulima wasiinunue kama alivyofanya mwaka jana ili wafanyabiashara waingie hasara kutokana na kuichelewesha.
Mbunge wa Viti Maalum, Munde Tambwe (CCM), alisema kuna haja kwa serikali kujenga maabara nyingi za kupima udongo ili kujua ardhi katika kila eneo inahitaji aina gani ya mbolea.
Pia alitaka serikali kujenga kiwanda cha tumbaku mjini Tabora ili kusaidia ajira kwa vijana mkoani humo.
Kwa mujibu wa Munde, kitendo cha serikali kujenga kiwanda cha tumbaku mjini Morogoro wakati tumbaku inalimwa mkoani Tabora, hakiwatendei haki vijana na wananchi wa Tabora kwa sababu nao wanahitaji ajira kupitia kiwanda hicho.
Mbunge wa Viti Maalum, Rita Kabati (CCM), alitaka kuwapo na mpango wa kuhifadhi maji yanayotokana na mvua ili kuyawezesha kutumika katika kilimo wakati wa kiangazi.
Mbunge wa Viti Maalum, Magreth Sakaya (CUF), alisema kuna watendaji ambao wameshirikiana na benki kukopa mikopo ambayo haikufika vyama vya ushirika na kuwafanya wakulima kulipa madeni ambayo hawakunufaika nayo.
Aliitaka serikali kueleza ni hatma ya benki hizo na watendaji ambao wamekopa mikopo hiyo na kuwabambikizia wakulima madeni kupitia vyama vyao vya ushirika.
Bajeti ya wizara hiyo ilipitishwa jana jioni.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top