Ludovick Utouh. |
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ameshauri kampuni za simu zinazotoa
huduma ya utumaji fedha na kumbi za harusi vitozwe kodi.
Sambamba na hilo
aliutaka uongozi wa Bunge, kurejesha Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu za Mashirika ya
Umma (POAC).
Alisema hayo
alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha taarifa yake bungeni
mjini hapa jana akisema uamuzi wa kufuta kamati hiyo na kazi zake kuunganishwa
na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), hautakidhi matarajio ya wadau wa
uwajibikaji.
Kwa upande wa kodi, alishauri kodi kutoka kwa
wafanyabiashara wadogo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ihusishe kikamilifu
makatibu kata kutambua walipa kodi wakiwamo wamiliki wa kumbi za harusi na
mikutano.
Akifafanua
kuhusu kodi kwenye kampuni za simu za mkononi alitaka zitozwe kodi ya zuio la
malipo ghafi ya kamisheni, inayolipwa kwa wanaofanya biashara hiyo ya kuhamisha
fedha kwa niaba ya kampuni.
Uhamishaji
fedha hizo unafanywa kwa kupitia mifumo ya M-pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na
Easy Pesa.
Alishauri kodi
hiyo ya zuio, ipunguzwe kutoka kodi ya mwisho inayotakiwa kulipwa na kampuni za
simu.
Utouh alisema
PAC itazidiwa na wingi na ukubwa wa majukumu na akatoa mfano, kuwa hata kabla ya
kamati hizo kuunganishwa, kamati hizo mbili zilikuwa
zinazidiwa.
Alisisitiza
kuwa ni jambo jema POAC irejeshwe kwa jina lolote, lakini kazi zake zibaki zile
zile.
“Kuna
mashirika 176, ukiweka na taasisi za Serikali mzigo unakuwa mkubwa na PAC hii ya
Zitto (Kabwe ambaye ni Mwenyekiti), kama atafanikiwa hata nusu ya kazi zake,
itakuwa ni muujiza.
“Hivyo
nashauri tuone uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama itakuwa na haja ya
kubadilisha jina, iitwe ya mashirika ya umma au ya uwekezaji, lakini ifanye kazi
za POAC,” alisema Utouh.
CAG pia
alisisitiza kuwa licha ya Serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya ukaguzi wa
umma, mabadiliko hayo hayajaingilia uhuru wa ofisi yake kutimiza wajibu
wake.
Hata hivyo,
Mwenyekiti wa PAC, alilalamikia sheria hiyo kuwa inawaziba midomo wabunge kwa
vile wanazuiwa kujadili ripoti ya CAG.
Zitto alisema
mfumo uliokuwapo wa kuwasilisha ripoti za kamati za Bunge, umefutwa na Serikali
baada ya kutunga sheria, na Serikali inachotaka ni Bunge kujadili ripoti hizo
kupitia kamati zake kabla ya kujadiliwa na Bunge
zima.
Makamu
Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema Serikali imetunga sheria hiyo kwa
vile haitaki kusimamiwa na Bunge, ila inataka Bunge kiwe chombo cha kujadili
tu.
Alisema hilo
halikubaliki na akasisitiza kuwa kamwe hawataruhusu ripoti za Kamati ya CAG
isijadiliwe bungeni.
“Tunatumia
miezi mitatu kuomba fedha za Watanzania, lakini linakuja suala la kuhoji
matumizi yake kwa sasa tunanyimwa fursa hii…hatuikubali ni lazima ripoti hizi
zijadiliwe na mwenye kuwajibika awajibike kama ilivyotokea mwaka jana,” alisema
Filikunjombe.
Mwenyekiti wa
PAC wa zamani John Cheyo alisema sheria hiyo mpya ya Ukaguzi wa Umma,
inaifedhehesha Serikali na akashauri marekebisho hayo yafutwe na Bunge ili kutoa
fursa ya ripoti ya CAG kujadiliwa.
“Tulikuwa
tunakwenda mbele sasa na mabunge mengine yalikuwa yanakuja hapa kujifunza namna
tunavyoshirikiana na CAG kusimamia fedha za umma, lakini sheria hii ya sasa
inaturudisha nyuma, tusikubali ni lazima ripoti hii ijadiliwe bungeni,”
alisema
Cheyo.
Wakati huo
huo, CAG alisema ataanza ukaguzi kwenye misamaha ya kodi kwa vile fedha ambazo
zingelipwa kutokana na misamaha, ni za Serikali ambazo zinatolewa kama ruzuku
kwa wanaopewa misamaha hiyo.
“Tumeamua
kuikagua kwa kina misamaha yote ya kodi kuanzia mwaka ujao wa fedha kwa
madhumuni ya kuangalia manufaa ya misamaha hiyo kwa uchumi wa Taifa,” alisema
Utouh.
Lakini CAG
alitaka hati za misamaha ya kodi, ziwekwe bayana kuwa msamaha wa kodi ni wa muda
gani, unaanza lini na kumalizika lini.
Alitaka
misamaha ya kodi iainishwe ikionesha malengo yanayokusudiwa na kuwa na utaratibu
wa Serikali kusimamia utekelezaji wa misamaha hiyo.
Ameshauri pia
mikataba yote yenye vipengele vya misamaha ya kodi, ipitiwe na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa ajili ya ushauri kabla ya kusainiwa na pande
husika.
Pia alishauri
mikataba ya kuchimba madini, ijadiliwe na Kamati ya Bunge inayoshughulikia
masuala ya madini, na ushauri utolewe kwa waziri husika kabla ya
kusainiwa.
Post a Comment