*Washirika wa Ludovick waanza
kubainika
*Teknolojia ya
mawasiliano yafichua siri zao
MTANDAO wa watu
wanaodhaniwa kuwa washirika wa karibu wa mtuhumiwa wa kupanga njama za
kutekeleza ugaidi, Joseph Ludovick, umeanza kufichuka.
Taarifa za
kufichuka kwa mtandao huo, zimekuja zikiwa zimepita siku tatu baada ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza orodha ya majina ya watu mbalimbali,
wakiwemo viongozi wa serikali, kiliodai kuwa ndio wanaopanga mipango ya
kishetani kisha kuwasingizia watu wengine.
Duru za habari
kutoka vyanzo mbalimbali vya MTANZANIA Jumatano zimeeleza kuwa, taarifa za awali
za kikachero zilizokusanywa katika mfumo wa mawasiliano ya simu ya kiganjani ya
Ludovick zimeonyesha kuwa amekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya
wanahabari waliopata kufanya kazi kwa karibu na Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri, Absalom Kibanda.
Mawasiliano hayo
yanadaiwa kuwa ni ya mazungumzo ya simu na ya kumtumia fedha kupitia mitandao ya
kifedha ya simu za kiganjani.
Kwa mujibu wa
taarifa hizo, mbali na wanahabari hao, pia uchunguzi umeonyesha kuwa Ludovick
amekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya wanasiasa wa Chadema, viongozi wa
juu serikalini na katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mmoja wa
makachero aliyezungumza na gazeti hili (jina lake tunalifahadhi) alieleza kuwa
taarifa za uchunguzi wa awali uliofanywa kwenye mfumo wa mawasiliano ya simu ya
Ludovick zimeonyesha kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akiwasiliana kwa karibu na
wahariri waandamizi wawili, waandishi wa habari na wachangiaji wa makala katika
magazeti mbalimbali nchini.
Kachero huyo
aliwataja wahariri wanaodaiwa kuwa na mawasiliano ya karibu na mtuhumiwa
Ludovick ambao ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile na
Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Ansbert
Ngurumo.
Balile na
Ngurumo, kwa nyakati tofauti wamepata kufanya kazi na Kibanda. Ngurumo na
Kibanda walifanya kazi pamoja katika Kampuni ya Habari Corporation Ltd, wakiwa
waandishi wa habari wa gazeti la kila wiki la Rai na baadaye walifanya kazi
pamoja katika Kampuni ya Free Media Ltd, inayochapisha gazeti la Tanzania Daima,
ambako Kibanda alikuwa Mhariri Mtendaji na Ngurumo akiwa Naibu Mhariri
Mtendaji.
Kwa upande wake
Balile, alipata kufanya kazi na Kibanda katika Kampuni ya Mwananchi
Communication Ltd na muda mrefu baadaye Kibanda alichukua nafasi ya Balile ya
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media, baada ya kuondoka kwenda masomoni
nchini Uingereza.
Taarifa za
uchunguzi wa kikachero zilizonaswa na MTANZANIA Jumatano zimeeleza kuwa,
Ngurumo, mara kadhaa, amepata kufanya mawasiliano ya mazungumzo na Ludovick
kupitia simu yake ya kiganjani na pia alipata kumtumia fedha kupitia simu yake
hiyo ya kiganjani.
Duru za
uchunguzi zinaonyesha kuwa baada ya tukio la Kibanda siku sita baadaye, Ngurumo
aliandika kupitia ukurasa wake wa facebook kuwa ameibiwa simu yake hiyo
aliyokuwa akiitumia kufanya mawasiliano na Ludovick.
Katika ujumbe
wake huo, Ngurumo aliandika kuwa; “Kuna mtu ameibia simu yangu yenye laini mbili
- Tigo (0719001001) na Airtel (0782172665) - tangu juzi na anatumia namba hizo
kutapeli pesa kwa watu ambao majina yao yamo kwenye contact list. Anawatumia
watu meseji, hapigi wala hapokei simu anapopigiwa. Anadai kwamba mimi nina shida
naomba msaada na anapendekeza kiwango cha pesa za kutumiwa.
“Wapo wachache
ambao wameibiwa tayari na wengine walitaka kuthibitisha kama ni mimi, wakapiga
simu hakupokea. Wanaojua namba zangu za simu wameniuliza kupitia simu yangu ya
Voda, wakagundua ni mtego wa tapeli. Kwa taarifa hii, nawajulisha wote
wanaonifahamu na wasionifahamu watakaoombwa pesa na mimi kutoka kwa yeyote,
wasitoe kabisa. Anayeomba pesa hizo si mimi, ni tapeli!”
Ujumbe wake huo
ulizua maswali kwa baadhi ya watu ambao walihoji ni kwa vipi matapeli hao
waliweza kufahamu mpaka namba ya siri ya M-pesa au Tigo-pesa yake kiasi cha
kufikia kupokea fedha kupitia namba zake hizo za simu?
Wengine
walionyesha shaka, wakimuuliza ni kwa nini hakuwahi kwenye kampuni za hizo simu
kwenda kuzifunga na badala yake akaziacha kuendelea
kutumika?
Mmoja wa watu
waliochangia katika ukurasa huo wa Facebook, France Rubian, aliandika akihoji;
“Da..! Muda wote huo kaka kwa nini ukae kimya? Achilia mbali kuibiwa, mbona
angeweza hata kukuharibia mambo mengine kama akiwa na nia hiyo? Hapa panazuka
mjadala mreeeefu usiokuwa na majibu sahihi. Simu imeibiwa, wewe kwa muda wa
siku2 hujachukua hatua, aliyeiba anaomba hela kupitia hizo namba zako, ‘password
zako pia anazo ndiyo maana anaweza kuchukua hela.... Mh! Kazi
kwelikweli.”
Tambo za
kiuchunguzi zilizofanywa na gazeti hili, zimebaini kuwa moja ya namba hizo za
Ngurumo, 0719 001 001 ambayo ndiyo imeandikwa kwenye safu ya bodi ya wahariri
kupitia gazeti analoliongoza la Tanzania Daima, hadi jana ilikuwa inaonyesha
kuwa imesajiliwa kwa jina la Subira Ramadhani.
Alipoulizwa
Ngurumo kupitia simu yake ya kiganjani na MTANZANIA Jumatano kuhusu uhusiano
wake na Ludovick na iwapo ana ushirika naye wowote wa kibiashara, alisema
anamfahamu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, lakini hana ukaribu naye sana wala
hashirikiani naye katika biashara yoyote.
Ngurumo alisema
alimfahamu Ludovick akiwa katika harakati zake za kisiasa mkoani Kagera, baada
ya kuunganishwa na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred
Lwakatare, aliyeeleza kuwa ni msaidizi wake wa kisiasa.
“Nilimfahamu
kijana huyu nikiwa katika harakati zangu za kisiasa mkoani Kagera na
nilifahamishwa kwake na Lwakatare, ni msaidizi wake. Alianza kunizoea taratibu
na baadaye aliniomba kunisaidia kazi za blog yangu kwa madai kuwa hana kazi na
alidai pia kuwa huwa anamsaidia Mjengwa kazi za blog yake, lakini kabla sijaanza
naye kazi akawa amekamatwa,” alisema Ngurumo.
Alipoulizwa
mazingira yaliyosababisha amtumie fedha kupitia simu yake ya kiganjani, Ngurumo
alisema Ludovick alipata kumuomba fedha za kumsaidia kuhama mahali alipokuwa
akiishi, lakini alishindwa kumsaidia kwa sababu hakuwa nazo na mara ya pili
alimuomba Sh 50,000 baada ya kupata wageni ghafla nyumbani.
“Aliniambia mama
mkwe wake amekuja na hana hela, akaniomba Sh 50,000, nikamwambia hizo nyingi
sana, basi nikatafuta kiasi kidogo nikamtumia, sikumbuki nilimtumia Sh ngapi,
lakini nadhani ni Sh 20,000 au 30,000.”
Aidha, taarifa
zaidi zinaeleza kuwa Balile, ambaye aliteuliwa na Jukwaa la Wahariri kuwa mmoja
wa wajumbe wa timu ya kuchunguza tukio la kuvamiwa na kuteswa kwa Kibanda,
amekuwa akifika ofisini kwa Ngurumo na kufanya mazungumzo naye kwa muda
mrefu.
Kwa upande wake
Balile, naye alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu uhusiano wake na
Ludovick, alisema alimfahamu kijana huyo kupitia mawasiliano ya mitandao ya
kijamii ambapo alianza kujenga naye ukaribu kabla hawajaanza kuwasiliana kwa
simu.
Balile alisema,
Ludovick alimueleza kuwa anavutiwa na uandishi wake wa makala na aliomba
amfundishe kazi ya uandishi wa habari, jambo ambalo hakuweza kulifanya kutokana
na majukumu yake mengi.
Hata hivyo,
alivyoulizwa iwapo amekuwa akimtumia fedha Ludovick, alisema hajawahi kumtumia
hata mara moja, licha ya kumuomba mara kadhaa na kutaja mara ya mwisho
aliyomuomba akiwa mkoani Iringa, kwa maelezo kuwa alikuwa amekwama nauli ya
kwenda Makambako, hivyo aliomba kutumiwa Sh 20,000 kwa ahadi ya kuzirudisha
baada ya kurejea Dar es Salaam.
Alieleza zaidi
Balile kuwa, alitafuta kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kumtumia, lakini kabla
hajatuma alipata taarifa kuwa amekamatwa na polisi.
Alipoulizwa
Balile iwapo amewahi kujadili mwenendo wa mwandishi yeyote wa habari na Ludovick
na hata kumpatia mawasiliano yake, alikiri jambo na kueleza kwa ufupi kuwa ni
kweli alipata kutoa mawasiliano ya namba za simu ya mmoja wa waandishi wa habari
kwa Ludovick, lakini baada ya kupata habari za kukamatwa kwa mkanda wa
Lwakatare, alishtuka na kuamua kujipeleka mwenyewe polisi kueleza namna
alivyotoa namba hiyo kwa Ludovick na mambo mengine anayoyajua kuhusu
Ludovick.
Vyanzo vingine
vya habari vya MTANZANIA Jumatano vimeeleza kuwa miezi michache kabla ya
Ludovick kutiwa nguvuni akituhumiwa kushiriki mipango ya kigaidi, alijaribu
pasipo mafanikio kujenga uhusiano wa karibu na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la
Mwananchi, Dennis Msaki.
Vyanzo hivyo vya
habari vinamtaja Balile kufanya kazi ya kuwaunganisha Ludovick na Msaki, vikidai
kuwa ni Balile ndiye aliyempigia simu Msaki kumtaarifu kuwa Ludovick ni kijana
wake na ana shida ambayo Msaki anaweza kuitatua, hivyo amempa namba yake ya simu
ya kiganjani ili awasiliane naye.
Kwamba siku
chache baada Msaki kupokea ujumbe wa Balile, alipigiwa simu na Ludovick ambaye
kwanza alimpongeza kwa uandishi mzuri wa makala, kisha akamuomba awe mwalimu
wake wa uandishi wa habari, jambo ambalo lilimshangaza Msaki, kwa sababu
haandiki makala magazetini na hivyo alimueleza kuwa taarifa alizopatiwa siyo
sahihi na kumkatia mawasiliano.
Mbali na Balile
na Ngurumo, taarifa za kikachero zinaeleza zaidi kuwa wapo pia baadhi ya
waandishi wa habari wanaotajwa kuwa na mawasiliano ya simu na Ludovick, jambo
linalozua hofu kuwa Mtandao ambao aliutaja Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema,
Mabere Marando ni mkubwa na si tu kwamba unaigusa serikali na CCM pekee, bali
pia wanahabari na baadhi ya wanasiasa.
Jumapili Aprili
14, Marando, alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza orodha ya
majina ya watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa chama na serikali kuwa ndio
wahusika wa mipango ya kishetani.
Miongoni mwa
viongozi wa juu wa CCM waliotajwa na Marando ni Naibu Katibu Mkuu wa chama
hicho, Mwigulu Nchemba, aliyedai kuwa uchunguzi wake ulibaini simu yake kufanya
mawasiliano ya mara kwa mara kwa watuhumiwa wa ugaidi. Hata hivyo, Mwigulu
amekwisha kaririwa akieleza kuwa yuko tayari kueleza kile anachokijua kuhusu
mtandao wa ugaidi mbinguni na duniani.
Marando
aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na uzoefu wa kazi yake ya
ushushushu, amechunguza na kubaini kuwa watu hao aliowataja ndio wahusika na
vitendo viovu na kuahidi kuwa ataongoza jopo la mawakili wa Chadema kumteteta
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Rwakatare, anayekabiliwa
na tuhuma za kushiriki kupanga ugaidi
mahakamani.
Post a Comment