Mwenyekiti wa Uvccm wilaya ya Arumeru mkoani
Arusha aliyesimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi,Boniphace Mungaya(picha na
moses mashalla)
SAKATA la kusimamishwa mwenyekiti wa
jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),wilaya ya Arumeru mkoani
Arusha,Boniphace Mungaya limeonekana kuvuta hisia mbalimbali kwa wanasiasa,
vyombo vya habari na viunga mbalimbali vya mkoa wa Arusha.
Mungaya,alisimamishwa mnamo oktoba
mwaka jana ili kupisha uchunguzi baada ya kuandikiwa barua na katibu wa CCM
mkoani Arusha,Mary Chatanda huku akituhumiwa kwamba ni mlinzi wa mwenyekiti wa
Chadema taifa,Freman Mbowe madai anayoyapinga vikali.
Hivi karibuni mwandishi wa gazeti
hili alikutana uso kwa uso na kada huyo wa CCM na kisha kufanya mahojiano naye
kuhusu sakata hilo.
SWALI.Je umepokeaje uamuzi wa
kusimamishwa ndani ya chama chako?
JIBU.(anavuta pumzi)…..Kwa kweli huu
ni unyanyasaji ndani ya chama sijui baya nililolifanya
waliniandikia barua ya kunisimamisha uongozi kwamba nimefanya usaliti ndani ya
chama kwamba mimi ni mlinzi wa Mbowe na nimeonekana naye mkoani Mtwara kwenye
M4C jambo ambalo si la kweli kabisa.
Hata siku moja sijawahi kuhudhuria
mkutano wa Chadema,na tena sijawahi kupata bahati ya kufika mkoani Mtwara,jambo
hili halina uhakika na hakuna hata ushahidi wa picha ukweli ni kwamba
nimefananishwa na mlinzi wa Mbowe aitwaye Zachariah Swai.
Mara nilivyopokea barua ya
kusimamishwa sikuchukua hatua yoyote kwani nasubiri uamuzi na
taratibu ndani ya chama hadi sasa kwani walinisimamisha tangu oktoba mwaka
jana.
Vijana wengi Arumeru walionichagua
hata wale ambao hawakunichagua ninajitahidi kuwatuliza hakika nawambiwa wasubiri
uamuzi wa chama kwa kuwa wengi kila siku wanauliza nini hatma yangu ndani ya
CCM.
Sisi tunaongozwa na kanuni na
taratibu ndani ya chama hizi ni changamoto tunazozipitia sisi vijana ndani ya
chama kama mimi kusimamishwa vijana wengi wamesononeshwa sana katika hili jambo
langu wengi wameona ni uonevu.
Hadi sasa nina imani kubwa na kamati
ya siasa mkoa wa Arusha kwamba itanirejeshea nafasi yangu ,nina imani hiyo
kwamba hivi punde watanirejesha madarakani na haki itatendeka pasi na
shaka.
SWALI.Endapo ikitokea kwamba
umevuliwa uongozi je utachukua hatua gani?
JIBU.Sitahama chama changu mimi si
kama wengine wanavyofanya pindi wanapovuliwa madaraka,nitaendelea kusimama ndani
ya chama change kama kada wa kawaida kwa kuwa sioni sababu ya
kuhama kwenda kwingine.
Unajua ndani ya chama change kuna
sera nzuri zinazotekelezeka ambazo huwezi kuzipata kwingine msimamo wangu ni
kwamba nitaendelea kubaki mwanachama hai wa CCM hata wakinivua
madaraka.
SWALI.Madai ya vijana ndani ya vyama
vya siasa nchini kutumika kama madaraja ya kupitisha wagombea
unayazungumziaje?
JIBU…..(anacheka kidogo)……sio vyema
kuwatumia vijana kama madaraja au mipira ya kiume(condoms),tabia ya kuwatumia
wakati wa uchaguzi au nyakati nyingine sio njema kabisa huu ni unyanyasaji na
uonevu mkubwa ni vyema kuwakumbuka vijana wakati kiongozi
unapopata madaraka.
Hii tabia ndiyo
imewacost(imewagharimu) baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wengi
walipiganiwa lakini mwisho wa siku wakajisahau na sasa wamewatupa
vijana baada ya kuwatumia hivyo ushauri wangu ni kwamba si vyema kuwatumia
vijana kama madaraja ya kupata nafasi na kisha kuwatupa.
SWALI.Je una mtizamo gani kwa vyama
vya upinzani hapa nchini?
JIBU.Upinzani kwangu hauna shida
yoyote kabisa,ila ninataka viongozi kutoka vyama vya upinzani watekeleze
majukumu ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwa wanasiasa wote tunahudumia
jamii zetu.
Upinzani sio vurugu,upinzani sio
matusi wala fujo ukiwa mpinzani ukatawala kwa vurugu haziwezi
kusaidia nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo lakini kwa hali ya
sasa naona upinzani umekuwa ni vurugu tu.
Kwa mfano kwetu Arumeru kuna baadhi
ya kata zimeshikiliwa na wapinzani lakini sasa hivi wananchi wanalalamika kwamba
hazifanyi vizuri kimaendelea kisa wananchi walipiga kura za chuki tu hivyo
upinzani sio vurugu ni maendeleo.
SWALI.Je unadhani CCM kitang”oka
madarakani mwaka 2015?
JIBU….(anacheka tena)…Hata siku moja
hakuna kitu kama hicho ,CCM ndiyo inazidi kushika chati ndiyo
inazidi kufanya kazi lakini pia ndiyo inazidi kung”aa .
Wote wanayoiombea ife watabaki kuomba
hadi kesho ifike lakini haitafika ,kwa kuwa sasa hivi CCM tuna umri wa kutosha
tangu kizaliwe na tuna sera zinazotekelezeka ambazo huwezi kuzipata mahali
kwingine,kwa kweli bado sijaona mbadala wa kuing”oa CCM hadi sasa.
SWALI.Je una matarajio gani ya
kisiasa hapo baadaye?
JIBU.Kwanza ni kukisimamia chama
changu na kushirikiana nacho bega kwa bega kutekeleza ilani yake kwa kuwa CCM
ndiyo tunasimamia serikali lakini pia kusimamia haki na wajibu
ndani ya chama changu siku zote.
Lakini kuwatumikia vijana wa CCM
Arumeru pamoja na wananchi wote bila itikadi zao,ninatarajia
kutowaangusha vijana wenzangu kwani nitaendelea kusimamia haki
ndani ya chama changu kwani nina imani nacho na vijana wasiogope kwani mimi
ndiye mwenyekiti wao hakuna mwingine.
SWALI.Mbali na nafasi ya uenyekiti je
umeshawahi kushika nafasi yoyote?
JIBU.Nimeshika nafasi mbalimbali tu
tangu nikiwa chipukizi ndani ya CCM mwaka 1994 nikiwa mwenyekiti wa chipukizi
kata ya Kiranyi na baadaye nikawa mwenyekiti wa tawi kisha baadaye
nikachaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la wilaya ya Arumeru mwaka 2005 hadi
2010.
Nimekuwa mwenyekiti wa Uvccm kata ya
Kiranyi hadi sasa,mwenyekiti wa mtaa wa Sakina , ni mjumbe wa
serikali ya kijiji cha Kiranyi lakini pia ni mjumbe wa
halmashauri kuu ya CCM wilaya.
Imechotwa: Libeneke la Kaskazini
Post a Comment