MBEYA: Polisi mkoani Mbeya wanatuhumiwa kumshushia kipigo Barnabas Kahemele akiwa mahabusu na kusababisha kifo chake.
Kufuatia tukio
hilo, ndugu wa marehemu Kahemele wamegoma kuuchukua mwili wa marehemu huyo
uliohifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa Mbeya wakidai
kwamba mazingira yanaonyesha kuwa kifo chake kimetokana na kipigo cha polisi
baada ya kumkamata.
Inadaiwa kuwa
marehemu na wenzake wawili walikamatwa usiku ya Jumatano wiki hii, baada ya
askari hao kufika nyumbani kwa marehemu, eneo la Uyole ya Kati. Mke wa marehemu
Sara Muhwanji, alidai kuwa wakiwa wamelala walisikia mtu akigonga hodi na ndipo
alipoamka na kutoka sebuleni.
“Nilitoka sebuleni
na kuuliza nani anayegonga, ndipo nikasikia sauti ya mtu anasema kuwa mimi
Mhagama, huyo ni jirani yetu pale nyumbani. Lakini sikufungua mlango na nikaenda
kumwamsha mume wangu, naye akauliza nani jibu likawa mimi Mhagama nina shida,
fungua mlango. Ndipo marehemu alipofungua mlango, polisi wanne wakaingia ndani
na kumwambia kuwa yupo chini ya ulinzi,” alisema Sara.
Alifafanua kuwa
baada ya hapo polisi hao waliondokana naye na kwamba alipojaribu kuhoji kosa
alijibiwa kuwa afike polisi asubuhi ataambiwa kosa la mume wake. “Nilipofika
asubuhi ambayo ni juzi Alhamisi nikauliza mapokezi na kuwaambia kuwa nimekuja
kumwona mume wangu, askari wa mapokezi wakatafuta jina lake lakini hawakuliona,”
alisema.
Alieleza kuwa
baada ya hapo askari walimfuata na kumchukua, kisha kumpeleka ofisi zilizo
ghorofani na wakamwingiza kwenye chumba cha mahojiano, ambapo alihojiwa na
askari wa kiume.
Alisimulia kwamba
baada ya kumaliza walimtaka aendelee kukaa kituoni hapo akisubiri taratibu
zinazoendelea kuhusu mume wake.
Alisema kuwa baada
ya muda mfupi majibu yakawa tofauti na kuambiwa kuwa imetokea bahati mbaya mume
wake amefariki dunia.Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki
alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo alisema kuwa hana
taarifa.
Post a Comment