• Asema imani ni
nafsi, hata kula chura sawa
RAIS mstaafu wa Awamu ya
Pili, Ali Hassan Mwinyi amerejea kauli yake kuhusu mgogoro wa udini akisema kila
mtu ana haki ya kuchinja kutokana na imani yake ilimradi tu asivunje sheria za
nchi.
Mwinyi alisema
anashangaa kuona watu wakigombania kitu kidogo kama kuchinja ilihali Tanzania
ina utamaduni wa amani siku zote na kwamba kila mtu ana imani yake ya dini
anayoiamini.
Kiongozi
huyo mstaafu alitoa msimamo huo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano juu
ya utamaduni wa Kiislamu Afrika Mashariki ambapo Tanzania imechaguliwa kuwa
mwenyeji.
“Imani ni nafsi ya mtu
na haitakiwi kumlazimisha kula nyama iliyochinjwa na mwenzie. Na kama unaona
aliyochinja mwenzio ni kibudu basi usile chinja yako, kula hata ukitaka kula
chura, mjusi, konokono, kula utakacho ruksa ilimradi tu usiingie katika jinai,”
alisema.
Mwinyi alikumbusha kuwa
hata wakati wa utawala wake majaribu kama hayo yaliwahi kumtokea, lakini
alijitahidi kuweka sawa kwa kumwambia kila mtu ale kile anachofikiri ni chakula
bila kumlazimisha mwenzake.
Alisema Watanzania
wamezaliwa ardhi moja na kwamba kinachotakiwa ni kuwa na misingi ya kuvumiliana,
na kwamba sifa ya Uislamu ni pamoja na kuwa na uvumilivu.
Aliongeza kuwa Uislamu
si kufanya vurugu kama inayotafsiriwa na makundi ya wanaotaka kuvunja amani ya
nchi kwa kutumia jina la dini ya Kiislamu.
Pia alimshukuru Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Ulimwengu wa Kiislamu Duniani (Rabita), Dk. Abdullah
Mohsin Al-Turki kwa kuichagua Tanzania katika kuhubiri amani.
Waziri wa Maji, Prof.
Jumanne Maghembe ambaye alimuwakilisha Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal katika
kongamano hilo, alisema kuwa utamaduni wa Kiislamu Afrika Mashariki na duniani
kwa ujumla ni kuvumiliana katika dini.
Pia aliwataka Waislamu
kujiendeleza katika elimu, akisema kuwa hata Mtume alihamasisha hayo, lakini
Waislamu wameshindwa kuyafuata.
Prof. Maghembe alitoa
mfano kuwa Waislamu wana Chuo Kikuu kimoja wakati dhehebu moja la Lutherani lina
vyuo vikuu 11, akisema ni vyema wakaungana na kujenga vyuo kwa ajili ya kusaidia
kuongeza wasomi katika taaluma mbalimbali.
“Suala la elimu ya dunia
pia ni muhimu, lakini mfano mzuri wa elimu kushuka ni katika mikoa ya Pwani
ambako ndiko ilipoanzia. Mathalani mwaka 1995 wanafunzi walioanza darasa la
kwanza walikuwa 35,000 lakini waliomaliza darasa la saba ni 9,000. Hapa
inaonesha Waislamu tunarudi nyuma,” alisema.
Akizungumza katika
kongamano hilo, Dk. Abdullah Mohsin Al-Turki alisema katika nchi ya Saudia
wanaishi watu tofauti, lakini wakiwa katika upendo huku akisisitiza kikubwa ni
kuheshimiana.
Alisema Rabita imekuwa
ikifanya kazi katika nchi mbalimbali za Nigeria, Gabon, Jamhuri ya Kongo na
baada ya ziara yake nchini hapa atahitimisha kwa kuitembelea
Sudan.
Kongamano hilo
limeandaliwa na Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania likiwa na
lengo la kusisitiza amani nchini.
NA TANZANIA
DAIMA
Post a Comment