Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (Elimu), Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa akijibu swali bungeni mjini Dodoma. (Picha na Maktaba).
Na Benedict Liwenga.
Serikali inakusudia kutumia shilingi bilioni 18.4 zilizotokana na fidia ya manunuzi ya Rada kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa Halmashauri zote nchini.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (Elimu), Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa amelifahamisha Bunge wakati akijibu swali la Mbunge wa viti Maalum, Mh. Sarah Msafiri Ally aliyetaka kujua mipango ya serikali kupunguza tatizo la upungufu wa madawati shule za Msingi nchini.
Mh. Majaliwa amesema serikali imekuwa inapeleka fedha kila mwaka katika halmashauri kwa ajili ya utengenezaji wa madawati.
Majaliwa ameainisha kuwa mwaka 2010/2011 serikali ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 3 katika halmashauri zote na mwaka 2012/13 shilingi bilioni 1 zilipelekwa katika halmashauri kwa ajili ya kutengeza madawati.
Aidha, serikali inahimiza Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutunza fedha katika mipango yao ya bajeti kwa ajili ya miundo mbinu mbalimbali ya shule ikiwemo madawati.
Pia serikali imetoa fursa ya uvunaji wa miti ya asili kupandwa kwa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa madawati kwa ajili ya shule.
Majaliwa amesema kuwa serikali inatambua umuhimu wa kuwa na madawati ya kutosha katika shule ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Hadi mwezi Machi 2013 shule za msingi za serikali zilikuwa na upungufu wa madawati 1,310,675.



Post a Comment