Ndugu zangu,
Februari 6 mwaka huu nilipata bahati ya kukutana na kuongea na wake wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini. Ilikuwa ni nyumbani kwa Balozi wa Sudan.
Kwenye mazungumzo yangu ( Pichani) niliongelea umuhimu wa Jumuiya hiyo ya wake wa Mabalozi kuendelea kuchangia elimu ya wasichana waliokatishwa masomo.
Kwamba ni haki kupata elimu na pia kumpa msichana nafasi ya pili katika maisha.
Kwamba ni haki kupata elimu na pia kumpa msichana nafasi ya pili katika maisha.
Nikakumbushia historia ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Jamii kwa kutolea mfano nchi ya Sweden. Kwamba kwa hapa nchini Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi vimetokana na urafiki wa kati ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere na Waziri Mkuu wa Sweden aliyeuawa, Olof Palme.
Kwamba ni kutokana na ziara ya Julius Nyerere Sweden iliyopelekea avione Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi vya huko na kuamua kuiga mfano huo. Hapa nchini Vyuo hivyo vilianzishwa katikati ya miaka ya 70. Idadi ya vyuo hivyo kwa sasa ni 53.
Niakaelezea pia umuhimu wa elimu na namna binadamu tunavyopata maarifa. Kwamba tunapata maarifa kutokana na milango mitatu; Uzoefu ( Fronesis) Shule ( Episteme) na Vipaji ( Tekne). Nilifafanua hayo kwa kutolea mifano hai.
Na kwamba , wasichana hao wanaokatishwa masomo yao wengine kwa kubakwa na walimu wao nao wana uzoefu ambao, ukichanganywa na elimu ya darasani na vipaji vyao, wanaweza kwenda mbele kimaisha na kutoa mchango katika ujenzi wa nchi yao.
Juzi, kupitia Shirika la Karibu Tanzania Association, wake hao wa Mabalozi wametoa mchango wa takribani shilingi milioni 4 kusaidia miradi ya kujitegemea ikiwamo ufugaji wa kuku wa kienyeji na bustani inayofanywa na wasichana hao kwenye Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi vya Njombe, Ilula na Ulembwe.
Tunawashukuru kwa mchango huo, na kubwa kabisa, ni kwa wao kufikisha ujumbe, kuwa kuna umuhimu kwa wasichana waliokatishwa masomo kwa sababu ya uja uzito kupewa nafasi ya pili maishani.
Post a Comment