Zaidi ya watu 30 usiku wa kuamkia jana walivamia na kuivunja nyumba ya Yasinta Malisa, iliyopo Kunduchi Ununio ,kando ya Bahari ya Hindi, huku wakimtishia kwa bastola mlinzi wa nyumba hiyo.
Kutokana tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela (Pichani), amemtaka mmiliki wa nyumba hiyo kuwasilisha vielelezo vya umiliki wa eneo hilo polisi.
Hatua hiyo inalenga katika kuwawezesha polisi kuvipitia na kumpa ushauri wa ama kwenda mahakamani au kumkamata anayeshukiwa kubomoa nyumba hiyo.
"Wanatakiwa kuwasilisha vilelezo vya umiliki wa eneo hilo, lakini pia inaonyesha kuwa kuna mgogoro katika eneo husika. Vielelezo ndivyo vitaonyesha kila kitu na tutajua wapi kuna tatizo," alisema Kenyela.
Mmoja wa walinzi wa nyumba hiyo, Saitoti Nang'oro na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ununio, Iddi Musa, walisema watu hao walivamia mtaa huo saa 9 usiku wakiwa na marungu, mapanga na bastola.
Akizungumzia na gazeti hili, Yasinta alisema baada ya kufiwa na mume wake mwaka jana, aliamua kuendeleza ujenzi wa nyumba hiyo, lakini siku tatu baada ya kuanza kazi, watu hao walivamia na kuivunja nyumba yake.
"Hili eneo tulilinunua kutoka kwa wazawa wa hapa Ununio na nina vilelezo halali, ila nashangaa kitendo kilichofanyika tena kimefanyika usiku, sasa kama wanamiliki eneo kihahali kwa nini waje usiku, mbona hakuna hata vilelelezo vyao katika ofisi za Serikali ya mtaa," alihoji.
Alisema alinunua eneo hilo miaka 20 iliyopita, huku akisisitiza kuwa eneo hilo halijapimwa na Serikali na wamiliki wake wanauza maeneo yao kama mashamba. Akisimulia alivyonusurika kuuawa Nang'oro alisema akiwa lindoni, aliona kundi la watu likija na wakati akijiandaa kuwahoji walimkamata na kumfunga kamba.
"Mmoja ndio alinishika na kunifunga kamba, wengine walikuwa wakibomoa nyumba kwa kutumia vyuma vikubwa. Yule aliyekuwa amenishika alikuwa pia ameshikilia bastola na aliniambia kuwa nisipokuwa mtulivu au nikikimbia atanipiga risasi," alisema Nang'oro.
Kwa upande wake, Musa alisema tangu achaguliwa kushika nafasi hiyo, vielelezo vilivyopo katika ofisi yake vinaonyesha kuwa mwenye eneo hilo ni Yasinta na siyo mtu mwingine.
CHANZO MWANANCHI
Post a Comment