Siku moja baada ya shirikisho la soka nchini TFF
kubadilisha ratiba ya baadhi ya mechi za ligi kuu ya Tanzania bara ili kuweza
kufanikisha mpango wa kuonyesha mechi hizo kupitia kituo cha Supersport, klabu
ya Yanga kupitia makamu wake mwenyekiti Clement Sanga imesema haikubaliani na
mpango huo kwasababu haujafuata utaratibu na pia utaziingizia hasara kubwa klabu
zinazohusika na mpango huo.
Akizungumza
na mtandao huu Sanga alisema kwamba mpango huo wa kuonyesha mechi za ligi
kuu bure kwenye Supersport haupo katika kuzinufaisha vilabu bali wahusika
wengine wa mpango huo.
"Kwanza jambo muhimu kuhusu suala hili kumekuwepo na
mfumo m'bovu wa mawasiliano baina ya TFF, Supersport na vilabu vyenyewe kama
Yanga. Sisi kwa upande wetu tunaona kabisa huu mpango unatuingizia hasara sana,
kwa mfano baada ya kubadilisha ratiba ya mechi zetu tutacheza mechi 3 ndani ya
siku 8 wakati ilitakiwa ndani ya wiki tucheze mechi mbili na bado ukumbuke bado
tunapaswa kusafiri kwenda Tanga hivyo kuna mambo ya gaharama na vitu vingine
vingi tu. Lakini pia mechi ambazo wanataka kuzionyesha bure ni zile ambazo sie
vilabu tunazitegemea sana kwenye suala zima la mapato na wao ndio wanataka
kuzionyesha bure - na watanzania wengi wanaposikia hivyo mahudhurio uwanjani
yanakuwa hafifu hivyo tunakosa mapato. Bora waonyeshaji wa mechi hizo wangekuwa
wanatoa fidia kiasi fulani kutokana na matangazo ya kibiashara wanayopata ili
kuweza kuzinufaisha klabu zetu, lakini si hivyo wanavyotaka wao. Nadhani kwenye
hili TFF wangeliangalia vizuri liweze kutunufaisha sote na sio watu wachache
kama ilivyo sasa," Aliongeza Sanga.
Alipoulizwa
kama wameshawasilisha msimamo wao kwa uongozi wa TFF na kamati ya ligi Clement
Sanga alisema, "Kwanza walipotuletea taarifa kuhusu jambo hilo kwa njia ya barua
pepe tuliwajibu na baadae ikaja barua ambayo katibu wetu alijibu kutoa msimamo
wetu juu ya suala hili, kinachojitokeza hapa TFF wanatumia mabavu yao kutupeleka
peleka, sie tumeshika makali wao mpini. Sie tusipokubali kucheza jumatano kama
wanavyotaka wao basi watachukua maamuzi ya kuigawia timu pinzani ushindi, la
msingi sie tutakalolifanya hatutokubali mechi zetu zionyeshwe kwenye TV bila
kupata fidia ya fedha. Sisi kama Yanga hatupo tayari kuona tunafanyishwa kazi
bure. Supersport imeshafanya majaribio sana, sasa haya ya sasa nini? Viongozi wa
soka tubadilike tuweke mbele maslahi ya soka letu kabla ya kujiridhisha nafasi
zetu, haiwezekani watu wawili watatu waamue tu kwamba mechi kesho hakuna bila
kujali hasara zitakazowagharimu wengine. Sie tulishajipanga kwamba Jumatano
tunacheza na Oljoro, then tunasafiri kwenda Tanga kucheza na Mgambo then turudi
Dar kwa ajili ya mchezo mwingine. Matayarisho ya mechi hizi tulishafanya wiki
mbili kabla, tukalipia hotel na gharama nyingine, sasa haiwezekani
ghafla kikundi cha watu fulani wenye nguvu za kimaamuzi kutubadilishia ratiba -
je zile fedha tulizolipa mahoteli watatulipaakina nani, kwa sababu ni dhahiri
unapolipia hotel unapewa na muda wa kuivitumia vyumba vile hivyo muda ule
unapoisha fedha yako inakuwa imeenda. Nadhani hili suala linahitaji kuangaliwa
vizuri, na viongozi wa vilabu tuwe na umoja kuweza kulipigania hili suala dhidi
yetu. Tusiwe viongozi wa kuburuzwa ovyo ovyo."
Akizungumzia
mahitaji wanayotaka ili wakubali mechi zao ziweze kuonyeshwa kwenye TV, Sanga
alisema kwamba hicho kituo cha TV kinachotaka kurusha matangazo ya moja kwa moja
ya mechi zao inabidi walete ofa ya kueleweka ambayo itaweza kufidia hasara ya
kwenye mapato na gharama nyingine ambazo timu wataziingia ili kuweza kwenda sawa
na ratiba zao. Pia akataka uwepo uwazi wa makubaliano yote ya kimsingi ili
kuepusha migogoro ya namna
hii.
Post a Comment