Gari aina ya Toyota Landcruiser
linalotumiwa na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa
Arusha, lilikamatwa juzi mjini Moshi likiwa limesheheni magunia 18 ya
bangi.
Habari za awali zilieleza kuwa gari hilo
lilikamatwa juzi saa 4:00 usiku katika Mji mdogo wa Himo, Moshi Vijijini
likisafirisha bangi hiyo kwenda Tarakea, Rombo.
Polisi wawili akiwamo dereva wa gari hilo wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Himo na gari lipo Makao Makuu ya FFU, Moshi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert
Boaz alithibitisha kukamatwa kwa askari hao: “Mchakato wa kuwafikisha
mahakama ya kijeshi unaandaliwa. Bangi hiyo ilikuwa inapelekwa kwa
mfanyabiashara mmoja huko Rombo na ndiye aliyewakodi.”
Hata hivyo, Kamanda Boaz alisema atatoa taarifa zaidi leo kwani uchunguzi bado unaendelea.
Bangi ilivyonaswa
Habari zimeeleza kuwa polisi waliokuwa doria
waliliona gari hilo likitengenezwa na waliamua kuwauliza wenzao
kulikoni? Wakajibiwa kuwa kuna kitu walikuwa wakirekebisha na lilikuwa
ni tatizo dogo tu.
“Walipoulizwa kwani mnaelekea wapi wakasema
wanapeleka mzigo wa bosi huko Tarakea mpakani na kwa taratibu zetu za
kijeshi huwezi kuuliza ni bosi gani,” kilidokeza chanzo kimoja ndani ya
polisi.
Hata hivyo, polisi hao wa doria walirudi katika
gari yao ili waendelee na doria lakini baadhi ya polisi wakamweleza
ofisa aliyekuwapo katika gari hilo kwamba wanashuku gari lile limebeba
bangi.
“Lilikuwa na harufu kali ya bangi na hilo ndilo
lililowafanya wale polisi kurudi tena kwa wenzao na kuwaambia wanataka
waone wamebeba nini ndipo wakakutana na magunia 18 ya bangi,” kilieleza
chanzo chetu.
Inadaiwa kuwa baada ya kukuta bangi hiyo, polisi
hao waliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi (RCO), Mkoa wa Kilimanjaro,
Ramadhan Ng’anzi ambaye naye alimjulisha Kamanda Boaz.
Ilielezwa kuwa Kamanda Boaz aliagiza kuwekwa mahabusu kwa polisi hao katika Kituo cha Himo na gari hilo lipelekwe FFU, Moshi.
Ofisa mmoja wa Polisi alidokeza kuwa baada ya kukamatwa, polisi
hao waliwasiliana na kigogo mmoja wa polisi Arusha ambaye inadaiwa
aliwafokea kwa kukamatwa kizembe.
“Inaonekana wanafanya sana biashara hiyo kwa
sababu karibu kila siku hili gari limekuwa likipita hapa. Hao jamaa
walitaka kuwahonga wale polisi Sh500,000 lakini walikataa,” alisema
ofisa huyo.
Arusha
Watanzania watatu wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro,
Arusha waliuawa kwa tuhuma za ujambazi huko Narok, Kenya Mei 2, mwaka
huu na kukutwa na bunduki aina ya ‘Sub Mashine Gun’ (SMG) ambayo
inasadikiwa kuwa ni mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Silaha hiyo ilitakiwa kuwa imehifadhiwa kwenye ghala la silaha katika Kituo cha Polisi Loliondo.
Kutokana na tukio hilo la aina yake, askari wawili
wa Kituo cha Loliondo, ambao majina yanahifadhiwa wanashikiliwa na
polisi wilayani Ngorongoro kwa uchunguzi kutokana na kupotea kwa silaha
hiyo hadi kukutwa mikononi mwa majambazi.
“Ni kweli tukio hili limetokea na kuna polisi
wanahojiwa kutokana na upotevu wa bunduki hiyo,” Mkuu wa Wilaya hiyo,
Elias Wawa Lali alisema.
Imeelezwa kuwa Watanzania hao waliuawa katika tukio la kuwateka wafanyabiashara wa Kenya waliokuwa wanatoka mnadani na kuwapora.
Lali alisema katika tukio hilo, majambazi hao
waliwaua wafanyabiashara wawili, lakini baadaye walizingirwa na wananchi
na wakauawa na kukutwa na bunduki hiyo.
Majambazi hao, waliouawa wametajwa kuwa ni Tigiki
Pasto, Steven Webo na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Kadogoo,
wote wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro.
Hata hivyo, alieleza kushangazwa na hatua ya ndugu
wa marehemu majambazi hao kushindwa kwenda Kenya kuchukua miili ya
ndugu zao kwa ajili ya mazishi hadi jana.
“Sisi kama Serikali tulijitahidi kuhakikisha miili
ya hawa waliouawa inaletwa nchini kuzikwa lakini hawa ndugu cha ajabu
wanataka polisi ndiyo wakawaletee miili,” alisema.
MWANANCHI
Mmoja wa ndugu wa marehemu hao, ambaye aliomba kutokutajwa jina
alisema wameshindwa kwenda kuchukua miili hiyo kwa sababu za kiusalama.
Alisema katika mazingira ya sasa ya Wilaya ya Narok kama wangekwenda huenda wangeuawa.
Hata hivyo, Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa
Jeshi la Polisi, Isaya Mngulu na Kamanda wa Polisi wa Arusha, Liberatus
Sabas walidai kuwa hawana taarifa ya tukio hilo.
Kuuawa kwa majambazi hao, pia kumekuja wakati
kukiwa na taarifa za muda mrefu za Polisi Wilaya ya Ngorongoro kuwasaka
majambazi hao kutokana na kuhusika katika matukio kadhaa ya ujambazi
katika maeneo ya Mji wa Wasson na Vijiji vya Soitsambu.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Mussa Juma na Boniface Meena.
Post a Comment