Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam
jana ilifuta kesi ya jinai iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Waziri wa Viwanda na
Biashara na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), Iddi
Simba, na wenzake watatu na kuwafungulia kesi mpya ya uhujumu
uchumi.
Washtakiwa
wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Uda na Diwani wa
Kata ya Sinza, Salim Mwaking’ida; Meneja Mkuu wa Uda, Victor Milanzi,
na
Mwenyekiti
Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena.
Washtakiwa hao
walisomewa mashtaka yao mapya ya uhujumu uchumi kesi namba tatu ya mwaka 2013
mbele ya Hakimu Ilvin Mgeta na Wakili wa Serikali, Oswald
Tibabyekomya.
Kubadilishwa kwa
kesi hiyo kumetokana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, kutumia
kifungu cha 12(3) cha sheria ya kudhibiti vitendo vya uhujumu uchumi cha mwaka
2002.
Wakili
Tibabyekomya alidai mahakamani kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita
ya kutumia vibaya madaraka na kulisababishia shirika hasara ya zaidi ya Sh.
bilioni nane.
Katika shitaka la kwanza, washitakiwa hao walidaiwa
kuwa, kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, katika maeneo yasiyojulikana jijini
Dar es Salaam, Simba akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uda, Milanzi, akiwa Meneja Mkuu
wa bodi hiyo na Kisena kama Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group
Limited, kwa pamoja walitenda kosa la kufanya manunuzi ya umma kinyume na
kifungu cha sheria cha 17 cha kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 cha mwaka
2007.
Katika shitaka
la pili, inadaiwa mshitakiwa Kisena, akiwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya
Simon Group ambayo ilikuwa na nia ya kununua hisa kwa Uda, alitoa kiasi cha Sh.
milioni 320 kwa Idd Simba na Victor Milanzi, kama kishawishi cha kuruhusiwa
kununua hisa hizo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za manunuzi ya
umma.
Wakili
Tibabyekomya, aliendelea kudai kuwa, katika kipindi hicho hicho, Idd Simba kama
mshitakiwa wa kwanza, na Victor Milanzi akiwa mshitakiwa wa tatu, kwa pamoja
wakiwa viongozi wa shirika hilo, walipokea kiasi cha Sh. milioni 320 kutoka kwa
Robert Kisena wa Kampuni ya Simon Group Ltd kama ushawishi wa kuuza hisa za Uda
kwa kampuni hiyo.
Katika shitaka
la nne, washitakiwa Simba, Mwaking’ida na Milanzi, walidaiwa kuwa kati ya
Septemba 2009 na Februari 2011, katika Makao Makuu ya Uda yaliyopo Mtaa wa
Bandari Kurasini Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, wakiwa viongozi wa
shirika hilo, kwa manufaa yao wenyewe walitumia vibaya madaraka kwa makusudi
kuuza hisa 7, 880, 330 mali ya Serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
kwa kampuni la Simon Group kwa kiasi cha Sh. 1,142, 643, 935 kinyume na sheria
za manunuzi ya umma ya kutangaza zabuni kwa umma.
Aidha, katika
shitaka la tano washitakiwa, Simba, Mwaking’ida na Milanzi, walidaiwa mahakamani
hapo kuwa wakiwa Makao Makuu ya Shirika hilo Kurasini jijini Dar es Salaam
walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa hisa 7,880,303 bila kibali cha Serikali
Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambao ni wamiliki wa Uda kwa Kampuni
ya Simon Group.
Katika shtaka la
mwisho, Tibabyekomya alidai kuwa washtakiwa Simba, Mwaking’ida na Milanzi kati
ya Februari 11, 2011 wakiwa Makao Makuu ya Uda kwa pamoja waliuza hisa 7,880,303
kwa kiasi cha Sh. 1,142,643,935 kwa kampuni ya Simon Group kinyume na utaratibu
wa sheria za manunuzi ya umma ya kutumia zabuni ili kuruhusu Watanzania wote
kununua na kusababishia hasara Shirika la Uda ya Sh. 8,422,076,940 iwapo
zingeuzwa kwa kufuata sheria ya manunuzi.
Hata hivyo,
washitakiwa wote walikana mashitaka hayo.
Hakimu Mgeta
aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 20, mwaka huu itakapoenda tena mahakamani hapo
kawa ajili ya kusomewa maelezo ya awali huku washtakiwa wote wakiendelea kuwa
nje kwa dhamana ya kesi ya mwanzo.
Pamoja na kesi
za uhujumu uchumi kutokuwa na dhamana, Hakimu Mgeta alisema kuwa wadhamini wa
washitakiwa hao wa kesi ya mwanzo iwapo hawatakuwa tayari kuendelea na kesi
mpya, washtakiwa wanaruhusiwa kwenda na wadhamini wengine.
Awali
washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na jumla ya mashitaka nane yakiwamo la
kula njama lililokuwa linawakabili Simba na Milanzi kinyume na kifungu cha 29
cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa ya mwaka 2007, na
kughushi.
Pia, kuhamisha
fedha kinyume na kifungu cha 29 cha Sheria ya kupambana na Rushwa, kwamba Simba
na Milanzi wakiwa viongozi wa Uda walishirikiana kuhamisha fedha kwa faida yao
binafsi Sh. 320,000,000, ikiwa ni malipo ya awali na ni sehemu ya malipo ya hisa
za Uda ambazo walizipokea wao binafsi kupitia nyadhifa zao .
Lingine ni lile
la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 302 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambalo lilikuwa linawakabili Simba na Milanzi kwamba
kati ya Septemba 3 mwaka 2009 na Machi 31 mwaka 2010 walijipatia Sh. 320,000,000
toka kwa Robert Simon Kisena wa Simon Group.
Shitaka la tano
ambalo lilikuwa linamkabili Simba na Milanzi ni la kuisababishia Uda hasara
kwamba kati ya Septemba 3 mwaka 2009 na Machi 31 mwaka 2010 kwa nia mbaya
walijihamishia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya matumizi yao binafsi, wakati
fedha hizo zilipaswa kuwa ni malipo ya awali ya ununuaji wa hisa za
Uda.
Mengine ni la
matumuzi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na
Kupamba na Rushwa, matumizi mabaya ya madaraka kwa kutenda kosa hilo kwa
makusudi kwa kuruhusu hisa hizo za Uda na la kuisababishia hasara kampuni
hiyo.
SOURCE:
NIPASHE
Post a Comment