JESHI
la Polisi mkoani Morogoro limeingia kwenye kashfa nzito baada ya askari
wake watatu na raia wanne kukamatwa wakiwa na kichwa cha binadamu.
Tukio hilo lilitokea Mei 7 mwaka huu katika eneo la Mgudeni- Dumila
wilayani Kilosa, linaandika gazeti la Mtanzania
Inaelezwa
kuwa polisi hao kwa kushirikiana na raia hao walikwenda nyumbani kwa
mfanyabiashara Samson Mura na kutaka kumbambikizia kesi ya mauaji.
Mbali ya kubambikizia
kesi hiyo, polisi hao wanadaiwa kuomba wapewe Sh milioni 25 na
mfanyabiashara huyo ili wasimpeleke kituoni.
Baadhi
ya wananchi walisema wameshangazwa na askari hao ambao wawili ni wa
Kituo cha Polisi Dumila na mmoja wa Kituo cha Polisi Mvomero.
Walisema siku ya tukio, polisi hao walifuatana na raia mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya masuala ya usalama.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgudeni,Zaituni Kifutu alisema walishangazwa na tukio hilo.
“Tumeshangazwa mno
na askari hawa… sijui walichukulia wapi mafunzo yao? Kama walibaini
kuwapo tukio hili kwa nini hawakutaka kulifikisha kituoni?
“Inasikitisha mno,
eti wao kwa kushirikiana na mfanyabiashara wanakwenda kudai kwa
mwanakijiji mwenzetu wapewe Sh milioni 25… haiingi akilini hata kidogo
wakamate mhalifu halafu washirikiane kwenda kuomba fedha.
“Tunaona na
mazingira ambayo askari na raia huyo ambao walifika kwenye nyumba ya
mfanyabiashara huyo, Samson Mura na kumtuhumu kukutwa na kichwa hicho si
mazuri ni ya kutaka kumbambikizia kesi tu. Yaani inasikitisha jeshi
kujaa uozo kiasi hiki,”alisema Kifutu.
Naye Musa Magisu alisema polisi hao walifika kwenye nyumba ya Mura na kufanya upekuzi ambao hata hivyo hawakuambulia kitu.
“Pamoja na kupekua kwa nguvu kubwa, hawakukuta kitu. Sisi tunamfahamu Mura ana silaha yake ambayo anamiliki kisheria,”alisema.
Alisema baada ya polisi hao kutoka nje ya nyumba walikwenda moja kwa moja kwenye gari lililokuwa limeegeshwa nje ya nyumba.
“Baada ya kufika
kwenye gari, yule raia na wale polisi waliona kuna mfuko wa rambo chini
na ghafla wakaanza kuuliza eti mfuko huu una nini na walipofungua
wakakuta kuna kichwa cha binadamu.
“Yaani baada ya
kukuta kichwa kile, walimuamuru mfanyabiashara yule atoe Sh milioni 25
lakini alikataa katakata akidai hajawahi kufanya tukio la aina
hiyo,”alisema.
Alisema mpaka sasa
hawajui kwa nini polisi ambao ni walinzi wa raia na mali zao, wamegeuka
watu wa kumbambikizia kesi wananchi wasio na hatia.
Ofisa Upelelezi
Msaidizi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Morogoro, Asifiwe Ulime alikiri
kutokea tukio hilo na kusema mpaka sasa polisi hao wanashikiliwa kwa
mahojiano zaidi.
Alisema hata yeye mwenyewe, alifika eneo la tukio na kushuhudia fuvu.
“Tunawashikilia polisi watatu na mwananchi mmoja kwa mahojiano ili watoe maelelezo ya kina juu ya tukio hili,”alisema.
Kutokana na hali hiyo, Ulime amewaomba wananchi wa Dumila kuwa watulivu wakati uchunguzi unaendelea.
Post a Comment