RAIS Jakaya
Kikwete ametangaza neema kwa wafanyakazi baada ya kuahidi kuwa Serikali
itawapunguzia makato ya kodi (Paye) na pia itawaongezea mishahara.
Akihutubia taifa katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei
Mosi) mjini Mbeya jana, Rais Kikwete alisema Serikali imeitikia kilio
cha muda mrefu cha wafanyakazi.
Aliahidi
kuwa Serikali itatangaza punguzo hilo la ongezeko la kodi na mishahara
kwa watumishi wa umma wakati Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa
atakapowasilisha Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2013/14.
Pia
alisema Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka atatangaza nyongeza ya
mshahara kwa sekta binafsi atakapowasilisha makadirio ya mapato na
matumizi ya wizara yake.
Hata
hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Serikali kupunguza kodi hiyo kwani
mwaka 2007, iliipunguza kutoka asilimia 18 hadi 15 na mwaka 2010
iliipunguza tena hadi asilimia 14.
Rais
Kikwete alisema mfumo wa makato ya kodi unatokana na kipato cha mtu
jambo ambalo limechangia wengine kukatwa kiasi kikubwa na wengine kidogo
lakini akasema anaamini kuwa makato hayo yataendelea kupungua bila ya
kuathiri uchumi wa nchi.
Mishahara
Rais
Kikwete alisema kuwa katika bajeti hiyo, Serikali itatangaza nyongeza ya
mishahara kwa watumishi wa umma na sekta binafsi huku akiahidi kuwa
italingana na hali halisi ya maisha.
Alisema
kutokana na hali hiyo, Serikali imetenga zaidi ya Sh4.76 trilioni katika
Bajeti ya Mwaka 2013/14 kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi wa umma.
Alisema
katika Bajeti hiyo, asilimia 44.9 ya fedha itakuwa kwa ajili ya
mishahara ya wafanyakazi, fedha ambazo zitatoka katika vyanzo vya mapato
vya ndani.
Alisema
katika kiasi hicho, zaidi ya asilimia 4.9 zinatoka kwenye mapato ya
Serikali na kilichobaki kitatoka kwenye vyanzo mbalimbali.
“Tunajua
kuwa, mishahara ya wafanyakazi ni midogo, lakini Serikali imekuwa
ikijitahidi kuongeza kila mwaka ili iweze kuendana na hali halisi ya
maisha,” alisema.
Alisema
mwaka juzi, kima cha chini kilikuwa Sh65,000 ambacho kiliongezwa hadi
kufikia Sh125,000 na kwamba mwaka huu wataongeza kiasi kikubwa ili
kiweze kukidhi mahitaji.
Mifuko ya Jamii
Akizungumzia
kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Rais Kikwete aliwaondoa hofu
wananchi na kusema iko hai na wafanyakazi watakaostaafu watalipwa mafao
yao kama kawaida.
Alisema
utafiti uliofanywa hivi karibuni na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA), umebaini kuwa mifuko hiyo haina matatizo
yoyote.
Alisema
Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), ulikuwa na matatizo
ambayo yalianza kabla ya mwaka 1999, jambo ambalo lilifanya uwe na
madeni ya zaidi ya Sh6 trilioni. Baada ya kuona hivyo, alisema Serikali
iliweka utaratibu wa kuuchangia kiasi cha Sh50 bilioni kila mwaka katika
mapato yake.
Alisema
kutokana na hali hiyo fedha hizo ndizo zinazotumika kulipa wafanyakazi
na wastaafu mafao yao na kwamba mpaka sasa hakuna aliyelalamika
kutolipwa mafao yake.
“Naomba
niwaondoe hofu Watanzania wenzangu. Hakuna mfanyakazi atakayekosa
kulipwa mafao yake pindi anapostaafu katika mifuko ya hifadhi ya jamii
ukiwemo PSPF,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa uwekezaji katika
mifuko hiyo unakua siku hadi siku. Rais Kikwete aliwashauri waajiri
kuwaacha wafanyakazi wajiunge na mfuko wowote wanaotaka ili waweze
kuhifadhi mafao yao.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz
Post a Comment