Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Joyce
Mapunjo, akifungua warsha ya kujadili mpango wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya
kuingizwa nchini (PVoC) uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es
Salaam.
Wadau mbalimbali wakifuatilia kwa umakini hotuba ya ufunguzi
wa Warsha ya kujadili Mpango wa Ukaguzi wa Bidhaa kabla ya kuingizwa nchini
(PVoC) uliofanyika kwenye Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau wakifanya usajili kabla ya kuingia kwenye warsha
ya kujadili mpango wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingizwa nchini (PVoC)
uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Mkutano huo
ulifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Joyce
Mapunjo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Joyce Mapunjo, akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kufungua warsha ya siku moja
iliyojadili mpango wa usalama na ubora wa bidhaa nchini (PVoC) pamoja
nae ni Meneja wa Bureau Veritas Tanzania, Bw. Cedric Serre.
---
Dar es Salaam, MEI 21, 2013
… Wakala wa
Kimataifa wa ukaguzi wa ubora na viwango vya bidhaa, Bureau Veritas (BV), kwa
kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wametoa tahadhali kwa
wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa nchini kuzingatia uzalishaji na
biashara zenye tija na viwango vya ubora kulingana na muktadha wa soko la leo
kimataifa, vinginevyo watashindwa kushindana.
Akizungumza kwenye warsha iliyojumuisha wafanyabiashara na
wazalishaji wa bidhaa mbalimbali katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam,
Makamu wa Rais wa Bureau Veritas, Jean-Michel Marnoto, alisema taifa
lolote linalozalisha bidhaa kwa kuzingatia ubora ni dhahiri hujisafishia njia
ya kufikia maendeleo kwa nyanja zote, hususan kiuchumi na kijamii.
“Ndio sababu tumekutana hapa ili kuelimishana na kubadilishana
mawazo ya namna ya kukidhi viwango na ubora kulingana na mahitaji ya soko. Na
kikubwa kinachotupa matumaini ni jinsi serikali ya Tanzania ilivyojitoa na
kuonesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha siku hadi siku inaweka mazingira
bora katika sekta ya viwanda na uzalishaji kwa maendeleo endelevu ya taifa na
watu wake,” alisema Marnoto
Marnoto
aliongeza kuwa BV kama wakala anayetambulika Kimataifa katika ukaguzi wa bidhaa
sanjari na kuthibitisha na kisha kutoa cheti cha ubora kwa bidhaa husika, kwa
kipindi kirefu imejijengea mwonekano mzuri na kukubalika kimataifa, huku
ikiamini hiyo ni fahari, heshima na jambo la kujivunia na la thamani
katika taswira ya dunia.
“Tunachukua fursa hii kuungana na wateja
wetu na watanzania kwa ujumla katika kubadilishana mazuri tuliyonayo kwa ustawi
na maendeleo, jambo la kuungana ndio hasa azma yetu kufikia dira ya kule
tunakokwenda,” alisema Marnoto
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Joyce Mapunjo, alisema kwa miaka
mingi sasa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, zimekuwa zikifanya jitihada
kuhakikisha zinakidhi vigezo vya uzalishaji wa bidhaa zake kulingana na
mahitaji ya soko, jitihada ambazo hata hivyo zimekuwa zikikwamishwa na
changamoto kadhaa zikiwemo rushwa na mifumo thabiti ya usimamizi.
Aliongeza kwa kuwahakikishia wadau wa sekta hiyo kuwa serikali kwa
kushirikiana na jumuiya za kimataifa na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs)
imeazimia kuboresha mazingira ya kiufanisi katika kufikia malengo, viwango na
vigezo vya ubora kulingana na uhalisia sambamba na mahitaji ya soko kwa bidhaa
husika.
Bureau Veritas ilianzishwa mwaka 1828, lengo likiwa ni
kushirikiana na taasisi za serikali ya nchi husika zinazotoa huduma ya ukaguzi
wa viwango na ubora wa bidhaa na kuthibitisha ubora wake, na kisha kutoa cheti
cha ubora kwa kampuni au taasisi husika iliyokidhi viwango na ubora,
kinachojulikana kama ‘Certificate of Conformity CoS’
Post a Comment