Na Mwandishi Wetu
******
Serikali imesema kwamba imebaini kuwa
baadhi ya wanasiasa na taasisi za kiraia wanahusika katika kuhamasisha
vurugu zinazoendelea mjini Mtwara.
Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana, kwa niaba
ya Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi
alirejea kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba Serikali itawasaka watu
wote wanaohusika na vurugu hizo ndani na nje ya nchi bila kujali
umaarufu na madaraka yao.
“Baadhi ya taasisi za kiraia na vyama vya siasa
kwa masilahi yao binafsi yasiyo na upeo mpana, vinaweza kudhani kuunga
mkono madai ya namna hii ni kuimarisha kukubalika kwao miongoni mwa
jamii,” alisema Dk Nchimbi: “Tunawakumbusha msemo wa wahenga usemao
‘tamaa mbele, mauti nyuma’... Tunaapa kuwasaka waasisi wa vurugu ndani
na nje ya Mtwara, ndani na nje ya nchi yetu.
Wote waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo hawataukwepa mkono wa sheria.”
Alisema Serikali inalaani vikali vurugu hizo
akisema wanaozihamasisha “wataipasua nchi, watasababisha vifo vya maelfu
ya watu, watajaza taifa vilema na majeruhi na hawatanufaika na matokeo
haya mabaya.”
Dk Nchimbi alisisitiza msimamo wa Serikali kwamba
maliasili hiyo ni ya Watanzania wote... “Tunalo taifa moja la Tanzania
ambalo maliasili zake ni za Watanzania wote. Tabia inayoanza kujengeka
ya kila eneo kutaka linufaike peke yake na mali za eneo hilo, italigawa
taifa letu vipandevipande.”
Alisema kiini cha vurugu hizo ni madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam.
Alisema Mei 15, mwaka huu kikundi cha watu
kilisambaza vipeperushi kuwataka wananchi wa huko Mei 17, saa 3:00
asubuhi kuacha shughuli na kusikiliza hotuba ya Bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini kujua mustakabali wa gesi kusafirishwa kutoka Mtwara
kwenda Dar es Salaam.
Alisema juzi, makundi ya vijana yalisikiliza
hotuba hiyo maeneo mbalimbali ya Mtwara kama vile sokoni, Magomeni,
Mkanaredi na baadaye kupanga mawe na magogo barabarani huku wakichoma
matairi.
“Hali hiyo iliendelea kusambaa maeneo mengine ya
mji kama vile Chuno, Chikongola, Mikindani na kutoka nje ya mji hadi
Mpapura, umbali wa kilomita 40 kutoka Mtwara mjini,” alisema.
Alisema polisi walikabiliana na vurugu hizo na hadi jana, watu 91 walikuwa wanashikiliwa.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment