Tumesikitishwa na kauli iliyotolewa bungeni na Mh. Zarina Madabida, mbunge wa viti maalum, mnamo Mei 8, 2013 akidai kwamba Sikika imekuwa ikiwakusanya wagonjwa ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) na kuwachochea waandamane kwenda ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM). Tumesikitishwa zaidi na kitendo cha Bunge kuruhusu baadhi ya wabunge kutumia muda wa Bunge kutetea maslahi yao binafsi badala ya taifa.
Mh. Madabida alitoa tuhuma hizo wakati wa kipindi cha Bunge alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2013/14. Mh. Madabida alinukuliwa akisema “…Sikika imekuwa inawakusanya wagonjwa ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI na kuwaleta mjini Dar-es-Salaam ili waandamane kwenda CCM… Lakini wamekuwa wakifanya uchochezi na kwenda ofisi moja hadi nyingine kwenda kufuata hizi habari…” Mh. Madabida ni mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI), ambacho hivi karibuni kimetuhumiwa kuzalisha ARVs bandia na kuiuzia MSD.
Hata hivyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh. Hussein Mwinyi aliliambia Bunge tarehe 9 Mei kwamba ana uhakika kabisa kuwa TPI haihusiki kutengeneza dawa hizo, ingawa taarifa rasmi ya uchunguzi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) haijatolewa kwa umma hadi leo. Awali, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliwasisitizia Watanzania kwa nyakati tofauti kwamba ina ushahidi kuwa dawa hizo bandia za ARVs zilitengenezwa na TPI. Kufuatia msisitizo huo, Wizara ilitoa amri ya kufunga kiwanda cha TPI.
Sikika inatamka wazi na kukanusha kwamba haijawahi hata mara moja kuomba kibali au kuratibu maandamano yoyote ambayo kwa njia moja au nyingine yaliwahusisha WAVIU na kuwapeleka kwenye ofisi za CCM kama alivyoeleza Mh. Zarina Madabida bungeni. Taarifa alizotoa Mh. Madabida si za kweli na zinalenga kuchonganisha na kuharibu muonekano wa Shirika kwa jamii ya watanzania wanaofaidika na shughuli au tafiti mbalimbali zinazofanywa na Sikika. Pia, hakuna mantiki wananchi kuandamana kwenda ofisi za CCM kwa kadhia ya ARVs bandia kwani wahusika wa kadhia hii ni Wizara ya Afya na Polisi. Kwa hiyo, kauli ya Madabida inatia shaka kuhusu ufahamu wake wa mambo labda kama alikusudia tu kuihusisha CCM ili apate huruma ya chama na ili kimtetee.
Sikika ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa nchini Tanzania kwa lengo la kufanya utetezi juu ya utawala na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watanzania wote ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa zenye ubora na viwango halali. Kwa hiyo, Sikika ingekiuka mojawapo ya malengo ya kuandikishwa kwake kama isingefuatilia sakata la ARVs bandia kwa sababu tu mojawapo ya wamiliki wa kiwanda kinachotuhumiwa ni Mbunge au kada wa chama cha siasa.
Kwa malengo hayo, Sikika itaendelea kutetea kwa kadri iwezavyo, bila upendeleo wala uonevu na kuhakikisha kuwa watanzania wote, wakiwemo WAVIU wanapata huduma bora za afya ikiwemo dawa na vifaa tiba ambavyo havina athari kwa afya zao. Kwa kuwa afya na uhai wa baadhi ya watanzania waliotumia hizo ARVs bandia zilihujumiwa, Sikika inaamini kwamba haki zao zilikiukwa. Hivyo tutafuatilia sakata hili hadi ukweli uwekwe wazi na wahusika wachukuliwe hatua. Hata kama itagundulika kuwa wahusika hao ni Wabunge, makada wa vyama au watendaji wa serikali.
Tunapendekeza Bunge letu liendelee kusimamia ukweli daima na kuhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa na mbunge yeyote ni za kweli na hazilengi kuchafua watu binafsi ama taasisi ambazo hazina fursa ya kujitetea ndani ya Bunge hilo. Hivyo basi, Sikika inamtaka Mh. Madabida kuthibitisha tuhuma hizo au sivyo aombe radhi kwa shirika.
Tunawakumbusha wabunge kwamba Bunge linaendeshwa kwa kodi za wananchi, hivyo litumike kutetea maslahi ya watanzania wote badala ya kutumika kama sehemu ya kulinda na kutetea maslahi binafsi. Michango yote ya kuongea ya Mh. Zarina Madabida Bungeni katika bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikuwa inalenga kutetea ama maslahi yake binafsi au maslahi ya kiwanda cha TPI ambacho yeye ni mmoja wa wamiliki.
Bw. Irenei Kiria
Mkurugenzi Mtendaji, Sikika, S. L. P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz


Post a Comment