Mikoa 18 kati ya 27 ya
kimpira tayari imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa
itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Timu tatu za juu katika
Ligi hiyo ya Mabingwa zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu
ujao (2013/2014). Ligi ya FDL ina jumla ya timu 24 ambapo tatu katika ligi hiyo
zilizoshuka daraja msimu huu ni Moro United ya Dar es Salaam, Small Kids ya
Rukwa na Morani FC ya Manyara.
Mabingwa waliopatikana
hadi sasa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo
FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi
Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC
(Kilimanjaro).
Wengine ni Magic Pressure
FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC
(Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC
(Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na
UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Kila klabu inatakiwa
kulipa ada ya ushiriki ambayo ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu
hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa
ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa
wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
MTANZANIA AOMBEWA ITC
ACHEZE NORWAY
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Norway (NFF) limetuma maombi ya kupatiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) kwa mchezaji Mtanzania Godfrey Mlowoka ili aweze kucheza mpira nchini
humo.
NFF inamuombea hati hiyo
Mlowoka ili aweze kujiunga na klabu ya Ekne IL kama mchezaji wa ridhaa ambapo
klabu yake ya zamani aliyokuwa akiichezea nchini imetajwa kuwa
Sadani.
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) linafanyia kazi maombi hayo na mara taratibu zote
zitakapokamilika hati hiyo ya uhamisho itatumwa nchini
Norway.
AZAM YAENDELEA KUJINOA
MOROCCO
Timu ya Azam ambayo iko
jijini Rabat kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la
Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabati ya huko inaendelea vizuri na
mazoezi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari
Msaidizi wa Azam FC, Jaffer Idd maandalizi yanakwenda vizuri kwa ajili ya mechi
hiyo itakayochezwa Jumamosi (Mei 4 mwaka huu). Jaffer Idd anapatikana kwa
namba+212671146092
Post a Comment