SHIRIKISHO la
Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limependekeza kima cha chini cha
mshahara kiwe sh 740,000 kutokana na gharama za maisha kuzidi kupanda.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Mbeya na
Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicolaus Mgaya wakati akisoma hotuba ya
wafanyakazi kwa Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi – Mei Mosi.
Alisema kuwa TUCTA iliiomba serikali ipandishe kima cha
mshahara kufikia sh 315,000 kwa kima cha chini tangu mwaka 2010, lakini haikuwezekana.
Mgaya alisema kuwa maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi yatakuwa na tija pale tu maagizo na makubaliano yatakapokuwa
yanatekelezwa.
Pia Mgaya aliishauri serikali kuangalia
uwezekano wa kupunguza kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi kutoka
asilimia 14 ya sasa hadi tatu.
Badala yake TUCTA, imeishauri serikali kutumia vyanzo vyake vingine kutafuta mapato kuliko kuendelea kuwabana wafanyakazi.
Mgaya alisema kuwa misamaha ya kodi
inayotolewa kiholela na serikali imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha
fedha ambazo zingesaidia kuboresha mishahara na mazingira mazuri ya kazi
kwa wafanyakazi.
Alisema kuwa takwimu zilizopo zinaonesha
kuwa uchumi unakua kwa asilimia 0.3, lakini hautakuwa na maana yoyote
kama misamaha ya kodi inatolewa bila kujali hali ya maisha ya
wafanyakazi.
Mgaya alisema kuwa serikali inapoteza
kiasi cha sh trilioni 1.3 katika misamaha hiyo, na hivyo
kuwanufaisha zaidi wawekezaji ambao pia ni waajiri.
“Mheshimiwa rais, nachukua fursa hii
kumpongeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoh kwa
kuweza kufichua wizi mkubwa wa fedha za umma unaofanywa na watumishi
wasiokuwa waaminifu na kuomba hatua kali zichukuliwe dhidi yao kwa kuwa
wanasababisha uchumi wa nchi uzidi kushuka,” alisema.
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Mgaya alisema izingatie haki kwa tabaka la wafanyakazi na mishahara iwe agenda ya kitaifa.
Pia aligusia hatua ya serikali kukopa
katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kutorudisha, akisema inazidi
kuwaongezea majonzi wastaafu.
Akihutubia katika kilele hicho, Rais
Kikwete aliahidi kuwa mishahara ya wafanyakazi itapanda katika bajeti ya
mwaka wa fedha ujao na kwamba Waziri wa Fedha atatoa mchanganuo huo.
Kuhusu kodi kupunguzwa kwenye mishahara ya
wafanyakazi, Rais Kikwete alisema suala hilo limeshazungumzwa kwenye
vikao vya pamoja na TUCTA na kwamba Waziri wa Fedha katika hotuba yake
ya bajeti atalitolea ufafanuzi.
Licha ya rais kutoa matumaini hayo, baadhi
ya wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili katika Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sokoine zilikofanyika sherehe hizo, walionesha kunung’unika.
Wafanyakazi hao wengi wao wakiwa walimu,
walisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete haina matumaini makubwa kutokana na
madeni makubwa wanayoidai serikali.
“Yaani hapa tumekaa tu hakuna jipya,
tulitegemea kuambiwa madeni yetu yatalipwa kabla ya bajeti mpya, lakini
mambo ni yale yale, hali ni ngumu. Huu uchumi unaokua mbona sisi
hatuuoni?” alihoji mmoja wa walimu.
Mbali na mafanikio mengi ya serikali yake
aliyoyaeleza, Rais Kikwete pia alisema kuwa kadiri uchumi utakavyozidi
kukua, serikali nayo itakuwa na uwezo wa kuongeza zaidi ajira za
watumishi wa umma.
“Tulifanya kosa mwanzo kutoa fedha bila
kutoa elimu ya ujasiriamali, kwa hiyo tunakusudia kutoa fedha kwa ajili
ya mafunzo kwenye vikundi vya vijana na wanawake ili waweze kupata
mikopo na kuweza kusimamia vizuri miradi yao,” alisema Rais Kikwete.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment