*******
Dar es Salaam. Idadi ya
watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati
ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya
marekebisho alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi
limebaini.
Habari ambazo gazeti hili
imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na
kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale
ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari kutoka
Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la
kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa
awali na huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao
82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa
wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo
mapya.
Kwa matokeo hayo, watahiniwa
wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa
225,126 sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo
walifaulu.
Msemaji wa Necta, John
Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua
kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili
watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema
Nchimbi.
Pia alisema usahihishaji wa
mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya
awali
Matokeo ya awali
yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha nne
mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa
126,847 sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa
na asilimia 28.1.
Katika matokeo hayo,
watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata sifuri, hesabu ambayo
imebadilika katika matokeo mapya ambayo yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja
hilo ni 158,100 ambayo ni asilimia 43.
Hata hivyo, habari kutoka
Necta zinasema kuwa licha ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya
kanuni mpya ya kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500
kushuka ufaulu ikilinganishwa na awali.
Maofisa mbalimbali wa Necta
pamoja na wale wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake,
walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita kukubaliana masuala mbalimbali juu ya
matokeo hayo pamoja na suala la matokeo ya wanafunzi hao 2,500 kabla ya
kutangazwa wiki hii.
“Baada ya wajumbe kujadili
suala lile, busara ilibidi itumike kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye alama yake
itashuka, kwa kawaida isingewezekana mtoto ambaye matokeo yalitoka akiwa
amefaulu leo umwambie ameshuka,” kilieleza chanzo
chetu.
MWANANCHI
Matokeo ya awali ndiyo
chimbuko la kupitiwa upya baada ya wadau kuyalalamikia na kumlazimisha Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume ya kuyachunguza Februari 23, mwaka
huu.
Kabla ya tume hiyo
kuhitimisha shughuli zake, ilitoa taarifa ya awali ambayo ilipendekeza kufutwa
kwa matokeo hayo kwa maelezo kwamba Necta ilitumia kanuni mpya ya kukokotoa
matokeo bila kushauriana na wadau.
Serikali ilitoa taarifa
bungeni kwamba imeamua kufuta matokeo ya 2012 na kuamuru yapangwe upya kwa
kufuata madaraja yaliyotumika mwaka 2011.
Ratiba ya
Bunge
Wakati hayo yakiendelea,
ratiba ya vikao vya Bunge la bajeti imefanyiwa marekebisho na kusogeza mbele
zamu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo awali, ilikuwa imepangwa
kusoma hotuba yake ya makadirio ya matumizi leo, badala yake nafasi hiyo imepewa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wizara ya Elimu sasa
imepangiwa kuwasilisha hotuba yake Juni 4 mwaka huu, hatua ambayo inatajwa
kwamba lengo ni kusubiri kutangazwa kwa matokeo hayo ya kidato cha nne na kidato
cha sita.
Wakati Mwenyekiti wa CCM,
Rais Jakaya Kikwete alipokutana na wabunge wa chama chake Mei 19, mwaka huu
mjini Dodoma, walisema hawako tayari kujadili hotuba ya wizara hiyo hadi matokeo
ya kidato cha nne na sita
yatakapotangazwa.
MWANANCHI
Post a Comment