MWENYEKITI wa Baraza la Wazee wilayani Kilolo,
Lunyiliko Nyaulingo amelazwa katika Hospitali ya mkoa Iringa na Mwenyekiti wa
CHADEMA Mgololo amelazwa Hospitali ya wilaya ya Mufindi baada ya kujeruhiwa
vibaya na watu wanaodaiwa ni wanachama wa CCM katika kampeni za mwisho za
kuwania nafasi ya udiwani.
Sambamba na hiyo Katibu wa CCM kata ya Ng’ang’ange
wilayani Kilolo, Wilhad Ngogo (40) na Yohana Mchafu anayedaiwa kuwa ni
mwanachama wa CCM wanashikiliwa na Polisi kwa kuhusika na matukio
hayo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi
alisema watu hao walikamatwa jana kufuatia
vurugu zilizojitokeza kwenye mikutano ya kampeni ya
mwisho katika wilaya hizo mbili.
Alisema kufuatia mzozo huo wanachama wa CHADEMA
walizuia barabara ya Iringa-Mbeya kwa kuweka magogo ili kuzuia magari kupita na
kuwa Polisi wanamtafuta Rabart Sam maarufu kwa jina la Kideri kwa kuongoza
vurugu hizo.
Kamanda Mungi alisema wanafanya uchunguzi wa kina juu
ya matukio hayo na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Aidha alitoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa
kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza
kutokea.
Leo Uchaguzi wa udiwani katika kata ya Ng’ang’ange
wilayani Kilolo na Mbalamaziwa wilayani Mufindi ulifanyika ambapo Zuberi
Nyomolelo (CCM) na Ezekiel Mlyuka (CHADEME) walipambana kwa kata ya Mbalamaziwa
na kwa upande wa Ng’ang’ange Kilolo Nafred Chahe (CHADEMA) na Namgalesi Msuva
(CCM) walipambana.
--
via Mjengwa
Post a Comment