Hatma ya kufikishwa mahakamani kwa Mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi ‘’Sugu”( Chadema), iko mikononi mwa Mwendesha Mashtaka wa
Serikali. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana kuwa
jeshi lake limekamilisha upelelezi kuhusu tuhuma zinazomuhusu Sugu na kwamba
wanasubiri maelekezo ya kumfikisha mahakamani. Mbilinyi alikamatwa juzi mchana
akiwa mjini Dodoma anakohudhuria vikao vya bunge na habari zilisema anatuhumiwa
kutoa maneno ya kashfa na uchochezi dhidi ya Waziri, Mkuu Mizengo Pinda. Inadaiwa kuwa mbunge huyo amefanya hivyo kupitia mtandao wa
kijamii. Kamanda huyo alisema jana Mbilinyi aliripoti katika Kituo cha Polisi
Kati kama alivyotakiwa na jeshi hilo na kuongezewa dhamana hadi leo anapotakiwa
kurudi tena kusikiliza hatma yake. Misime alisema “jeshi hilo liliamua kumkamata
mbunge huyo baada ya kugundulika kuandika maneno ya kumtukana Waziri Mkuu kuhusu
utendaji wake na kumdhalilisha katika siku ambayo hakuitaja.” Taarifa zisizo
rasmi zinaonyesha kuwa, mbunge huyo anatuhumiwa kuandika maneno hayo ya kashfa
kufuatia kauli ya Pinda hivi karibuni kuhusu kuwataka polisi kuwapiga raia
wasiotii sheria.
Alikuwa akijibu
swali la papo kwa papo ndani ya Bunge wiki iliyopita ambapo alisema Serikali
imechoshwa na vitendo vya watu kutotii sheria na kutoa mfano wa matukio ya
Mtwara na Arusha. Huko Mtwara polisi walitumia nguvu zaidi kuwadhibiti wananchi
waliokuwa wakikataa gesi isisafirishwe kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam,
wakati huko Arusha, walifanya hivyo katika kuwatawanya wafuasi wa Chadema,
waliokuwa wakishiriki katika tukio la kuaga maiti. Baadhi ya watu wakiwamo
wanaharakati walisema kauli hiyo inaweza kuleta chuki kati ya polisi na
wananchi.
Post a Comment