Chanzo cha vurugu kuhusu gesi zilizotokea hivi karibuni mkoani
Mtwara, kinaelezwa kuwa ni vuguvugu la kisiasa lililowaingia wananchi
kiasi cha kujenga chuki kubwa dhidi ya Serikali baada ya kupata mahubiri
ya wanasiasa.
Inaelezwa kuwa mzozo huo ulianza rasmi mwaka jana
baada ya Serikali kuituma kamati ya kuratibu Maoni ya Sera ya Gesi
ambayo ilifika mkoani Mtwara, Novemba 16, mwaka jana kukusanya maoni ya
wananchi.
Katika mikutano yake mjini Mtwara, inaelezwa kuwa
wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirisha gesi kwenda nje ya
Mtwara kwa njia ya bomba.
Hali hiyo ndiyo iliyowafanya viongozi wa vyama vya
NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, ADC, DP, APPT Maendeleo, Sau na Chauma,
kuungana na kuhamasisha wananchi kuhusu suala hilo.
Inaelezwa kuwa hilo lilifanyika Desemba 6, mwaka jana.
Katibu Mkuu wa Muungano huo, Selemani Litope
,alisema mikutano kati ya viongozi wa vyama hivyo na wananchi ilianza
Desemba 12. Mikutano hiyo iliyopewa vibali na Jeshi la Polisi ilifanyika
Desemba 12, 16, 19 na 22 na Desemba 27 yalifanyika maandamano makubwa.
“Tuliona kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu
suala gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, tukaona tuungane ili
tufikishe kilio cha wananchi serikalini, kwa sababu tunaamini kwamba,
kuisafirisha gesi hiyo ni kuwanyima wananchi fursa ya kufaidika,”
alisema Litope.
Alisema katika maandamano yaliyofanyika Desemba
27, Litope alisema walimwandikia Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Mstaafu Joseph
Simbakalia ombi la kutaka ayapokee lakini akakataa na kuwaita kuwa ni
wapuuzi, jambo lililozidisha chuki ya wananchi.
“Kitendo cha mkuu wa mkoa kutuita wapuuzi
,kimeibua chuki kubwa miongoni mwa wananchi, hata hivyo maandamano yetu
yalifanikiwa kwa sababu watu wengi walihudhuria na tukafanya mkutano
katika Uwanja wa Mashujaa,” alisema.
Hata hivyo, Simbakalia alishaomba radhi kwa kauli
yake hiyo Januari mwaka huu kupitia kikao cha majumuisho cha Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Nani anayetuma vipeperushi na meseji?
Kabla ya vurugu zilizotokea Mei 22 mwaka huu, kulikuwa na vipeperushi na ujumbe wa simu uliosambazwa mjini Mtwara.
MWANANCHI
Post a Comment