Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni kubwa taarifa
za shambulio la mlipuko lililotokea katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) mjini Arusha jioni ya leo, Jumamosi, Juni 15, 2013, tukio
ambalo limesababisha vifo vya watu wawili na majeruhi ya Watanzania
kadhaa.
Aidha, Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa
jamaa na ndugu wa wafiwa wote na pia ametuma pole nyingi kwa majeruhi ambao
wameumizwa na kujeruhiwa katika tukio hilo ovu na
katili.
Vile vile, Rais Kikwete amewatumia salamu za pole
viongozi wa CHADEMA kufuatia tukio hilo la woga mkubwa na pia kuviagiza vyombo
vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki za kuchunguza kwa haraka, kubaini,
kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika na tukio hilo, wawe
watu wa ndani ya nchi ama nje ya
nchi.
Katika salamu zake za rambirambi na za pole kwa Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Magesa Mulongo, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea
kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni kubwa shambulio la mlipuko lililotokea katika
mkutano wa CHADEMA mjini Arusha jioni ya leo, tukio ambalo limesababisha vifo na
majeruhi ya Watanzania wenzetu.”
Amesema Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mheshimiwa Magesa Mulongo salamu zangu za rambirambi kufuatia vifo na
pole nyingi kutokana na majeruhi katika tukio hilo na naomba kupitia kwako
unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa na pole
nyingi sana kwa majeruhi.”
“Kadhalika naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa
viongozi na wanachama wa CHADEMA kutokana na tukio hilo. Naomba uwajulishe kuwa
uchungu wao ni uchungu wetu sote na msiba wao ni msiba wetu pia.
Nataka wajue kuwa tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi na
huzuni mkubwa,” amesema Mheshimiwa Rais
Kikwete.
Rais Kikwete amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Arusha:
“Kadhalika, nimeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka
kuwasaka wahusika, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Aidha,
nawataka viongozi wa Serikali ngazi ya kitaifa, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya
Arusha mjini kuhakikisha kuwa majeruhi wote wanapata matibabu ya haraka na
huduma za tibabu stahiki.”
Aidha, Rais Kikwete ametoa wito maalum kwa wananchi
akisema: “Kwa wananchi wenzangu, Watanzania wenzangu, napenda kutoa wito wa
kuviachia vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi yao vizuri ili tuweze
kuwabaini waovu waliofanya kitendo
hiki.”
“ Natambua kuwa yatakuwepo maneno mengi na hisia mbali
mbali zitakazojaribu kulielezea tukio hilio ovu na katili kwa njia mbali mbali.
Nawasihi tujiepushe na kuchukua dhana na hisia zetu au maneno ya watu wengine
kuwa ni ukweli wa tukio hili. Tujipe nafasi ya kutafakari vizuri na kufanya
uamuzi ulio bora.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Mimi siamini kuwa Watanzania
au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya
unyama wa aina hii. Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia
mema nchi yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni
mwa raia ama makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko
makubwa.”
“Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, naomba tuzinduke,
ili tusiwape nafasi watu hawa waovu ya kuweza kutimiza malengo yao
ya kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu kwa kuleta mifarakano baina yetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Munfu Ibariki
Afrika.”
Credit to Father Kidevu
Post a Comment