*NI KWA KUMHUSISHA NA UJANGILI, BIASHARA YA PEMBE ZA
NDOVU
*ATAKA FIDIA SH. MILIONI 350
PETER MSIGWA |
DAR
ES SALAAM, Tanzania
KATIBU Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amefungua mashitaka katika
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) kufuatia mbunge huyo kumhusisha na
ujangili na biashara ya pembe za ndovu.
Amefungua
kesi hiyo kupitia Wakili wake, Eric Ng'mayo, kutokana na tuhuma alizozitoa
Mchungaji Msigwa, dhidi yake kuhusiana na ujangili na biashara haramu ya pembe
za ndovu.
Katibu mkuu huyo amefungua kesi hiyo kupitia kwa
wakili wake Eric Ng'mayo, baada ya mlalamikiwa huyo, kukataa kukanusha na
kumuomba radhi dhidi ya tuhuma hizo, hivyo Kinana ameiomba mahakama imwamuru
Msigwa kumlipa fidia ya sh. milioni 350.
“Naiomba mahakama imwamuru mlalamikiwa amlipe
fidia ya sh. milioni 350 kama hasara rasmi. Pia, fidia ya maudhi na fidia ya
hasara, mfano gharama za kesi.
“Mahakama imwamuru mlalamikiwa amlipe riba kwa
kiwango cha mahakama kwa tunzo ambayo atapewa na mahakama tangu tarehe ya hukumu
hadi malipo ya mwisho na kufuta tuhuma zake dhidi yangu na aniombe radhi kwa
kuchapisha katika magazeti mawili ya Kiingereza na mawili ya Kiswahili
yanayosambazwa nchini,” alidai Kinana kupitia hati yake ya madai.
Kupitia hati hiyo ya madai, Kinana anadai
mlalamikiwa aliendelea kurusha tuhuma hizo, hata baada ya kumtaka amuombe
radhi.
Mlalamikiwa huyo, ambaye ni Waziri Kivuli wa
Maliasili na Utalii, anadaiwa kuwa alitoa tuhuma dhidi ya Kinana kwa nyakati
tofauti nje na ndani ya Bunge.
Katika hati yake ya madai iliyowasilishwa
mahakamani hapo na Wakili Ng'mayo, Kinana anadai kwanza Mchungaji Msigwa, alitoa
tuhuma hizo Aprili 21, mwaka huu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Shule ya Msingi Mbugani, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Pia, inadaiwa mlalamikiwa huyo alirudia shutuma
hizo bungeni alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani katika Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa
fedha wa 2013/14.
Katika hati hiyo, amenukuu maneno yanayodaiwa
kutamkwa na Mchungaji Msingwa katika mkutano huo kuwa: "Kinana (naomba waandishi
wa habari mnisikie na nyie Usalama wa Taifa mkapeleke habari) hana sifa kupita
barabarani na kuwaambia Watanzania waiamini CCM. Kinana mikono yake si
misafi.
"Hata kwenye NASACO (Shirika la Wakala wa Meli
Tanzania) kuna harufu ya ufisadi ndani yake, ajibu hoja... Kinana meli zake
ndizo zinazohusika kubeba pembe nchi hii. Hajajibu hoja hizo. Kwa siku nchi hii
tembo 67 huuawa." Hao ndio wanaokifadhili Chama Cha Mapinduzi, kina Kinana
halafu wanakuja eti kuwashawishi Watanzania muwasikilize na kwamba Chama Cha
Mapinduzi eti ni kizuri.
"Halafu leo tukikaa ndani ya Bunge tunapojaribu
kuwatetea wananchi tumeacha majimbo yetu. Haya mambo ninayoongea ni hatari kwa
sababu haya yote ni majangili ni organized crime. Ni mtandao wa kimataifa, uko
duniani kote, unaweza ukatuua, lakini wabunge tumesimama tunawatetea..."
Mlalamikaji huyo anadai kutokana na kauli hizo,
ameharibiwa tabia yake na uaminifu na hadhi yake kitaaluma na weledi, hivyo
kumfanya achukiwe na kudharauliwa katika jamii.
Aidha, anadai jina lake zuri na heshima yake
alivyojijenga katika muda wote wa maisha yake vimeharibiwa na mlalamikiwa kwa
nia mbaya.
Kinana anadai tuhuma hizo ni za uongo, licha ya
kumsababishia maumivu ya kisaikolojia na hasara kubwa kifedha, kwani kabla ya
tuhuma hizo alikuwa katika hatua za mwisho za mchakato wa mazungumzo ya mradi wa
ubia wa kilimo cha mboga na mwekezaji wa kampuni kutoka nje.
Amedai kuwa kutokana na tuhuma hizo, kampuni
hiyo ilivunja majadiliano hayo, na kwamba sababu iliyotolewa ya kufanya hivyo ni
kutajwa kwake na mbunge huyo kuwa jangili anayejihusisha na biashara haramu ya
pembe za ndovu.
Kinana anadai mradi huo ulikuwa na thamani ya
dola za Marekani milioni nne, hisa zake za ushiriki zilikuwa asilimia 25 katika
kipindi cha miaka mitano, hivyo kupata hasara ya sh. milioni 350.
Aidha, mlalamikaji huyo anaiomba mahakama itoe
zuio la kudumu kumzuia mlalamikiwa au wakala wake kutoa ua kuchapisha taarifa
zozote dhidi yake.
Post a Comment