Na Hassan Hamad
OMKR
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim
Seif Sharif Hamad, amewatahadharisha wakaazi wa Arusha kuilinda na kuitunza
amani iliyopo ili kuuendeleza mji huo kiuchumi.
Katibu Mkuu wa CUF
Maalim Seif Sharif Hamad, akimtambulisha mgombea udiwani kata ya Themi mkoani
Arusha, Lobora Petro Ndarpoi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
relini kata ya Themi.
Amesema mji wa Arusha ni miongoni mwa miji
muhimu katika maendeleo ya Tanzania kutokana na umaarufu wake na kuwa mji wa
kitalii na biashara.
Maalim Seif ametoa tahadhari hiyo katika kata
za Themi na Kaloleni mjini Arusha, wakati akiwahutubia wakaazi wa maeneo hayo
kwenye mikutano ya kampeni za udiwani katika kata hizo.
Amefahamisha kuwa mji huo umeiletea sifa kubwa
Tanzania na kupelekea kuwa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kituo
muhimu cha mikutano ya kimataifa.
Ameongeza kuwa iwapo amani itatoweka katika
eneo hilo, itaupotezea sifa mji huo na kushuka kwa mvuto wake wa kitalii,
kibiashara na shughuli za kimataifa.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar amesema wakaazi wa Arusha wana kila sababu ya kujivunia maendeleo na
rasilimali zilizopo, yakiwemo madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Arusha
pekee duniani kote.
Akizungumzia kuhusu kampeni, Maalim Seif
amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu na kuvumiliana ili
kutunza na kulinda amani iliyopo ambayo ni rasilimali kubwa kwa maendeleo ya
nchi.
Amesema vyama vingi havikuja kwa lengo la
kuwagawa au kuwafitinisha Watanzania, bali kutoa fursa kwa wananchi kuchagua
chama au kiongozi wanayemtaka kwa uhuru.
Amewaomba viongozi wa vyama vya siasa
kushindana kwa hoja na kuachana na tabia ya kuwalazimisha na kuwanyanyasa
wananchi na kupelekea kuwakosesha haki na uhuru wao wa kuchagua na
kuchaguliwa.
Wagombea udiwani kwa kata za Themi na Kaloleni
kupitia Chama Cha CUF Lobora Petro Ndarpoi na Darwesh Abbass Ramadhan, kwa
upande wao wamewaahidi wakaazi wa maeneo hao kuwatatulia kero zinazowakabili kwa
muda mrefu zikiwemo upungufu wa ajira kwa vijana pamoja kuimarisha huduma za
elimu mashuleni.
Wamesema maeneo hayo yana utajiri mkubwa wa
viwanda lakini vingi kati ya hivyo havifanyi kazi vizuri, na hivyo kupoteza
fursa za ajira kwa vijana, na kwamba iwapo watachaguliwa watashirikiana na
halmashauri kuvifufua na kuviendeleza kwa maslahi ya wananchi wa Arusha.
Uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kata 26 nchini,
unatarajiwa kufanyika tarehe 16/06/2013, baada ya madiwani waliochaguliwa katika
kata hizo kupoteza sifa na wengine kufariki dunia.


Post a Comment