Bango la mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
Singida
Mratibu
wa mapambano dhidi ya UKIMWI wa halmashauri ya manispaa ya Singida,
Godson Charles Swai, amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Singida
mjini,kujibu tuhuma za makosa mbalimbali 21 yakiwemo ya kughushi kwa
lengo la kumwibia mwajiri wake.
Mshitakiwa
Swai alifikishwa mbele ya mahakama hiyo na TAKUKURU mkoa wa Singida na
kesi hiyo,inasimamiwa na mwendesha mashitaka mwanasheria wa TAKUKURU,
Antidus Rutayuga.Kati ya mashitaka hayo 21,18 ya kugushi na kujipatia
shilingi 1,260,000 mali ya mwajiri wake manispaa ya Singida.
Mapema
Rutayuga,alidai mbele ya hakimu Terrysphory Tesha,kuwa kati ya januari
saba mwaka 2008 na Desemba mwaka huo, mshitakiwa Swai aliandaa nyaraka
za matumizi ambazo ni za kumdanganya mwajiri wake,ili aweze kujinufaisha
binafsi.
Akifafanua, alisema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa na.11 cha mwaka 2007.
Katika
mashitaka 18,Rutayuga alisema mshitakiwa huyo aligushi kwa kuweka saini
yake kwenye hati za malipo ya posho za wanasemina wanaodaiwa kuwa ni
‘hewa’,kwa madai kuwa walihudhuria semina ya uhamasishaji wa mapambano
dhidi ya maambukizi mapya ya UKIMWI.Kati ya wanasemina hao,tisa hati
hizo zilionyesha kila mmoja alilipwa shilingi 90,000.
“Wanasemina
wengine watatu kila mmoja alilipwa shilingi 150,000 na wengine sita
walilipwa posho ya shilingi 300,000 kila mmoja”,alisema mwendesha
mashitaka huyo.
Rutayuga
alisema mshitakiwa Swai alitenda kosa hilo la kugushi na kujipatia
shilingi 1,260,000,huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na
kifungu 333,335 (d) kifungu kidogo (ii) 337 cha sheria ya kanuni ya
adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.
Mwanasheria
huyo wa TAKUKURU mkoa, alimsomea mshitakiwa shitaka jingine kuwa katika
kipindi hicho,Swai kwa makusudi alimsababishia mwajiri wake hasara ya
shilingi 1,260,000 huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na aya
ya 10 jedwali la kwanza kifungu 57 (i) kifungu 60 (ii),vyote vya sheria
ya uhujumu uchumi sura ya 200 ya marekebisho ya mwaka 2002.
Mshitakiwa Swai, alikana mashitaka yote hayo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai sita mwaka huu itakapotajwa tena.
Hadi
mwandishi wa habari hizi anaondoka mahakamani,mshitakiwa Swai alikuwa
hajapata wadhamini wawili kila mmoja mwenye mali isiyohamishika ya
thamani ya shilingi milioni mbili,kwa ajili ya kumdhamini.
Post a Comment