RAIS wa Marekani Barack Obama amewasili nchini Afrika kusini kuendelea na ziara yake ya nchi tatu katika bara la Afrika inayolenga kupanua uhusiano wa Marekani na bara hilo.
Ziara yake imekuja wakati kukiwa na wasiwasi wa afya ya kiongozi aliyepigania haki dhidi ya ubaguzi wa rangi, Nelson Mandela, ambaye yupo mahututi katika hospitali ya Pretoria.
Akizungumza na waandishi wa habari waliopanda ndege ya Rais ya Air Force One, Ijumaa bwana Obama alisema sio lazima kwake kumtembelea bwana Mandela katika hali yake ya sasa.
Maafisa wa White House walisema Alhamis kuwa ziara ya aina hiyo wanaiachia jukumu familia ya Mandela. Jumamosi Rais Obama anapanga kutembelea kisiwa cha Robben, gereza ambalo bwana Mandela alifungwa kwa miaka 27.
Rais Obama pia atakutana na kiongozi mwenzake wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Mshauri msaidizi wa usalama wa kitaifa nchini Marekani, Ben Rhodes aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba miongoni mwa masuala ambayo bwana Obama inaonekana atazungumzia ni suala la Zimbabwe ambayo inaelekea kufanya uchaguzi wa urais.
Rhodes alisema Marekani inataka kuona uchaguzi huru, sawa na wenye hadhi nchini Zimbabwe pamoja na nafasi ya uhuru wa vyombo vya habari na mambo mengine ya demokrasia nchini humo.
Marekani inamshutumu Rais Robert Mugabe kwa kutumia ukandamizaji na wizi kushinda uchaguzi wa urais uliopita ikiwemo ghasia na mzozo kwenye vituo vya kupiga kura mwaka 2008.Chanzo: voaswahili
Post a Comment