Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SERIKALI YASALIMU AMRI

 

Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia
*Yakubali hoja ya James Mbatia, yavunja Kamati ya EMAC

Serikali imeivunja Kamati ya Kuidhinisha Vitabu na Vifaa vya Elimu (EMAC), kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake inavyotakiwa. Badala yake itaunda chombo kingine kitakachokuwa na nguvu zaidi na kutekeleza kazi zake kwa ufanisi nzaidi.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, alipokuwa akishiriki kwenye mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Katika michango yao juzi na jana, wabunge wengi waliilaumu kamati hiyo kwa kuchangia kuvuruga na kudunisha elimu nchini.

Wabunge hao, walisema baadhi ya vitabu vya akida vilivyokuwa vikiidhinishwa na kamati hiyo kutumiwa shuleni vimekuwa vikipotosha wanafunzi kwa vile vilikuwa na makosa mengi.

Alisema baada ya kuundwa kikosi kazi kuichunguza EMAC, ilidhihirika kuwa kamati hiyo haikuwa na wataalamu wa kutosha.

Alisema hata baadhi ya vitabu vya ithibati, vilivyokuwa vikiidhinishwa na kamati hiyo vilikuwa na makosa.

Alisema chombo kitakachoundwa kitakuwa na meno na mamlaka zaidi kama lilivyo Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Chombo hicho, kitashughulikia ithibati na vifaa vya elimu na wajumbe wake watakuwa wanatembelea shule katika maktaba kuangalia vitabu na ambavyo vitakutwa na makosa vitafungiwa,” alisema.


Alisema vitabu vyote vyenye ithibati, vitapitiwa upya na vitakavyokutwa na makosa vitaondolewa.

Kuhusu fedha za ‘chenji ya rada’ zilizoidhinishwa kununulia vitabu, Mulugo alisema bado havijasambazwa.

Alisema vinatarajiwa kusambazwa mwishonki mwa mwaka huu.

Katika hatua nyingine, mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia amezidi kumkaba koo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, baada ya kudai kuna ufisadi katika matumizi ya zaidi ya Sh bilioni 52, ambazo ni sehemu ya ‘fedha za rada’ kununulia vitabu kwa ajili ya shule nchini.

Fedha hizo, ni sehemu ya zaidi ya Sh bilioni 70 ambazo zinajulikana kwa jina maarufu la ‘fedha za chenji ya rada’.

Alisema baadhi ya vitabu, vilivyonunuliwa kwa fedha hizo kwa ajili ya shule za msingi, havifai kwa vile vinawapotosha wanafunzi.

“Huu ni ufisadi kwa nini vinunuliwe vitabu vyenye makosa chungu nzima,” alisema.

Alitoa mfano wa vitabu kadhaa, vikiwamo vya Jiografia, Kiingereza na elimu ya uraia ambavyo alikuwa navyo bungeni na kusoma baadhi ya kurasa ambazo zinapotosha.

“Ndiyo maana nasema EMAC (Kamati ya Kuidhinisha Vitabu na Vifaa vya Elimu) ifutwe kwa sababu inalitumbukiza taifa katika janga la elimu,” alisema.

Alisema Watanzania hawana budi kukubali kwamba, elimu nchini kwa sasa ina matatizo makubwa na kinachotakiwa ni kuchukua uamuzi mgumu na kusonga mbele kuinusuru elimu nchini.

“Hakuna sababu ya kulaumiana kwa misingi ya itikadi, siasa au dini… hiki ndicho taifa tumevuna kwa kuivuruga elimu, kinachotakiwa ni tuchukue hatua tuinusuru elimu nchini,” alisema huku akikariri misemo mbalimbali ya dini za Kikristo na Kiislamu inayosisitiza umuhimu wa elimu.

Alisema elimu ndiyo moyo wa taifa lolote na akasema matatizo mengi yametokana na kutowekeza vya kutosha katika elimu kwa miaka mingi.

Mbatia alishauri angalau Sh trilioni 4.2, ziwekezwe katikka elimu kila mwaka na akampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutambua kuwa elimu ya nchi hii ina matatizo makubwa alipozungumza mkoani Mbeya Aprili mwaka huu.

Mbatia alimsifu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania, kuwa anafanya kazi nzuri.

Alishauri watu wanaohusika kuvuruga masuala ya elimu ndiyo wachukuliwe hatua kama watu binafsi.

Mbunge huyo alisema ili kuimarisha na kuboresha elimu nchini, hapana budi iundwe kamisheni ya elimu itakayoangalia masuala yote yanayozorotesha elimu nchini na kupendekeza hatua za kuchukua.

Susan Lyimo- Chadema (Viti Maalum) alisema ni muhimu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ajiuzulu.

Alisema kwa mfano wakati akitangaza kufutwa kwa matokeo ya mwaka 2012 ya kidato cha nne miezi ya mwanzo ya mwaka huu, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi alisema utaratibu ambao ungetumika katika kupatikana matokeo mapya ni kwa kutumia mtindo wa zamani wa usahihishaji (flexible grading).

“Lakini wakati Waziri Kawambwa anatangaza matokeo mapya hivi karibuni, alisema mtindo uliotumika ni uleule wa sasa (fixed grading),” alisema na kuongeza:

“Sasa kwa nini asiwajibike kwa sababu ni wizara yake ndiyo imehusika na ugatuaji wa elimu.”

Naye, Mwigulu Nchemba–CCM (Iramba Magharibi) alitumia muda mrefu kukishambulia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa kimechangia kuzorotesha elimu nchini.

Alisema kwa mfano Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amepiga marufuku wananchi katika jimbo lake kushiriki katika shughuli za ujenzi wa shule, nyumba za elimu na shughuli nyingine kama hizo.

Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, alisema wakati fulani Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alipounga mkono shule za kata “jioni Chadema ikamuweka kwenye kiti moto”.

Alisema mara nyingi mawaziri huangushwa na wataalamu na watendaji kwa sababu ndiyo ‘wapikaji’.

Mbunge huyo alitamka maneno hayo kumtetea Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ambaye wabunge wengi wa upinzani wamekuwa wakimtaka ajiuzulu na Naibu wake kutokana na matatizo mengi katika sekta ya elimu nchini hivi sasa.


    Na Revocatus Makaranga  MTANZANIA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top