Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue yaani
“dengue fever” hapa nchini. Ugonjwa huu
umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu
waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es salaam kupelekwa kwenye maabara
yetu iliyopo katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Dar es
salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo tarehe Juni 12,
2013. Utafiti huu uliongozwa na jopo la wataalamu kutoka Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ikishirikisha program ya mafunzo ya Epidemiolojia yaani
“Field Epidemiology and Laboratory Training Program” pamoja na manispaa
ya Ilala.
Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao waliogundulika kuwa
na dalili za ugonjwa huu ni 20 na hakuna mgonjwa yeyote
aliyepoteza maisha.
Homa ya
Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi
ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa,
maumivu ya viungo na uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia
kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya
dengue. Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza
kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati
wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua
la ili hatua stahiki zichukuliwe.
Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa kwa
binadamu baada ya kuumwa na mbu aina ya
“Aedes”. Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji
yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu
hawa huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili
na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma
wakati wa mchana.
Ugonjwa huu hauenezwi kutoka binadamu mmoja kwenda kwa
mwingine. Homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali
mapema na kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna tiba maalumu ya
ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili
zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu.
Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza
maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya
dengue
o
Kuangamiza mazalio ya mbu
ü
Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa
ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi
hayo
ü
Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile,
vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo,
nk.
ü
Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya
watu
ü
Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji
kutuama
ü
Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko
imara
ü
Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji
kutuama
o
Kujikinga na kuumwa na mbu
ü
Tumia dawa za kufukuza mbu “mosquito
repellants”
ü
Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
ü
Tumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira
ya mchana)
ü
Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za
kuishi
Hatua zinazochukuliwa na
Wizara
·
Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa
Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi.
·
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa
Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha uchunguzi wa ugonjwa huu
utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa
wenye homa.
·
Kutuma vipeperushi vya ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani ili
iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa
kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.
·
Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa
namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja
na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana.
·
Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika
hospitali 15 za mkoa wa Dar es salaam. Hospitali hizo ni pamoja na hospital ya
Taifa Muhimbili, Hospitali zote 3 za manispaa ya Dar es salaam, kituo cha afya
Kigamboni, Kituo cha afya cha Mbagala Rangi tatu, Dispensari ya Yombo Vituka,
Kituo cha afya cha Mnazi mmoja, Dispensari ya Tabata A, Kituo cha afya cha
Bochi, Kituo cha afya cha Mbweni, Hospital ya Mission Mikocheni, Hospitali ya
TMJ, Hospital ya Regency na Hospital ya Hindu Mandal
·
Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili kuweza
kuthibitisha ugonjwa huu
·
Kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa tatizo,
jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa
huu.
Ugonjwa huu si mpya. Mara ya kwanza kugundulika
kuwepo kwa ugonjwa huu nchini ilikuwa ni Juni 2010 mkoani Dar es
salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40 na hakuna
mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha.
Wananchi mnashauriwa kwenda katika vituo vya tiba mara
mnapoona dalili za ugonjwa huu.
Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote
vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara
itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa
huu.
Nsachris Mwamwaja
Msemaji
14 Juni 2013
Post a Comment