Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

TAMKO KUTOKA KWA KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA NA VIONGOZI WA MADEREVA WA BODABODA MJINI DODOMA 11/06/2013


 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma  David Misime
 --
TAMKO KUTOKA KWA KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA NA VIONGOZI WA MADEREVA WA BODABODA MJINI DODOMA 11/06/2013

Ndugu,

        Zangu Viongozi, Wawakilishi wa madereva wa Bodaboda na viongozi wengine mliopo hapa.

        Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutupa afya kuweza kukutana hapa leo.
        Pili niwashukuru kwa kuitikia wito na kukubali kuja ili msikilize ninachotaka tuzungumze ili wote tutoe maoni ili tuweze kuboresha zaidi utendaji wa kazi zetu za kila siku na kukabiliana na ajali zinazotuandama.         Kama mtakumbuka hiki ni kikao changu cha pili baina yangu nanyi. Kikao cha kwanza tulifanya tarehe 27/03/2013 na agenda zetu zilikuwa ni:-
  1. Kufahamiana na kujenga mtandao wa mashirikiano ili kuzuia uhalifu na ajali za barabarani.
  2. Kujadili mazingira ya kazi yenu
  3. Utii wa Sheria Bila Shuruti.

Baada ya majadiliano ya mada hizo baadhi yenu mliuliza maswali na kutoa maoni mbalimbali.

Kikao cha leo lengo lake ni kutaka tujadiliane pamoja tatizo linalotukabili hasa ninyi waendesha Bodaboda la 
AJALI ZA BARABARANI na lingine tutazungumzia nama ya kuendesha shughuli zenu kwa usalama zaidi kwa kushirikiana na Polisi na wadau wengine.

Ajali za barabarani zipo ambazo kwa namna yoyote ile zinapotokea, watu wanasema haiepukiki. Mfano, dereva amepatwa na ugonjwa wa ghafla na kushindwa kumudu chombo cha moto anachoendesha, kikakosa uelekeo na kupinduka ama kikagonga mtu au chombo kingine cha moto au watu walio pembezoni mwa barabara.

Nyingine inaweza ikawa chombo cha moto kimepata hitilafu katika mfumo wa umeme na ukasababisha ajali ikatokea, mifano inaweza kuwa zaidi ya hiyo.


Lakini ajali nyingi kulingana na utafiti uliofanyika asilimia 72 (72%) zinasababishwa na binadamu mwenyewe (aidha madereva au watumiaji wengine wa barabara).

Sababu zinazochangia ajali nyingi kutokea ambazo zinasababishwa na binadamu mwenyewe ni kama ifuatavyo:-

  1. Kutokuzingatia sheria za usalama barabarani.
  2. Mwendo kasi (hapo ndipo penye balaa).
  3. Kutokuzingatia alama za barabarani.
  4. Ulevi wa pombe na madawa ya kulevya.
  5. Dharau n.k.

Sababu hizo hapo juu ndizo zinazochangia ajali zote zinazotokea sehemu mbalimbali na hapa kwetu Dodoma kwa upande wa waendesha bodaboda.

Mfano hapa kwetu Dodoma kuanzia Januari hadi Juni 7/2013 ajali arobaini na nane (48) zilizohusisha bodaboda zimekwishatokea. Kati ya ajali hizo, zilizosababisha vifo ni kumi na saba (17) na waliokufa ni watu kumi na tisa (19). Zilizosababisha majeruhi ni ajali thelathini na moja (31) na waliojeruhiwa ni arobaini na saba (47). Katika ajali hizo zote arobaini na nane (48), zilizosababishwa na madereva wa bodaboda ni arobaini na mbili (42).

Ajali hizi kama madereva hawa wangekuwa makini na kufuata sheria na kuepuka yale niliyotaja hapo juu ambayo yanasababisha ajali, vifo hivi na majeruhi hawa, hatungekuwa tumekaa hapa tukizungumzia leo.

Mtu akisikia watu kumi na tisa (19) wamefariki kwa upeo wa kibinadamu anaweza kuona ni idadi ndogo lakini siyo hivyo ni kubwa sana tukizingatia zimesababishwa na uzembe na zimepunguza nguvu kazi ya taifa na kuwaacha wategemezi wengi na shida zaidi ya walizokuwanazo wakati walipokuwa na mtegemezi wao ambaye watakuwa wamempoteza kwa ajali.

Niwaombe nguvu ambazo huwa mnatumia na ushirikiano mnaoonyesha kwa misururu ya pikipiki mnapomsindikiza mwenzenu aliyekufa 
kwa ajali maana hao kumi na tisa (19) waliofariki miongoni mwao waendesha bodaboda wapo kumi na moja (11) mzitumie pia kuonyana nyinyi kwa nyinyi kuepuka mwendo kasi maana ndiyo unawaua zaidi. Kufuatia sheria na alama za barabarani na pale ambapo hakuna alama ujue ni nani umpe kipaumbele cha kupita kwanza (mfano sehemu ambayo haina taa za barabarani au alama yoyote unayotakiwa umpe nafasi aliye kulia kwako nafasi ya kupita kwanza).

Nguvu hizo na ushirikiano huo utumieni kukaa vikao vya kuonyana ili mjiepushe na ajali ambazo zinaepukika.


Jambo lingine napenda niwaombe muendelee kuimarisha vikundi vya Ulinzi Shirikishi vilivyopo na kuanzisha vingine ili kuzuia uhalifu usitokee dhidi yenu na katika maeneo yenu. Lipo tatizo pia la baadhi yenu kukaa kwenye vituo au kufanya biashara ya kubeba abiria hadi saa nane hata tisa usiku. Jambo hilo ni hatari kwa maisha yenu, onyaneni ili kuacha mtindo huu. Sisi Polisi tutaanza kuchukua hatua zinazostahili kadri sheria inavyotuelekeza.
Nisisitize tena kwenu tuzingatie UTII WA SHERIA BILA SHURUTI.

Fanya shughuli zako kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na hakuna atakayekubughudhi na itakusaidia kuepuka ajali zisizotarajiwa.

Pia naomba kila mmoja atambue kuwa Usalama unaanza na WEWE MWENYEWE, MIMI MWENYEWE NA SISI SOTE.                
 
DAVID .A. MISIME - ACP
KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA

POLISI MKOA WA DODOMA
DAWATI LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top