
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya akizungumza na waandishi wa habari jana (hawapo pichani)

Baadhi
ya maofisa wa TGNP wakiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Usu Mallya
wakizungumza na waandishi wa habari jana (hawapo pichani).
------------------------------------------------------------------
Na Thehabari.com
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), umetoa mrejesho
wa utafiti shirikishi uliofanywa na kikosi cha waraghbishi kutoka
mtandao huo katika baadhi ya vijiji kutoka mikoa ya Shinyanga, Mbeya na
Morogoro-huku matokeo yakionesha kuibuka kwa changamoto kadhaa katika
maeneo yote ya utafiti.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuelezea matokeo ya utafiti,
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema miongoni mwa masuala
makuu yaliyojitokeza katika utafiti huo shirikishi na uraghbishi ni
pamoja na changamoto za uwekezaji na mgawanyo mbaya wa ardhi kwa
wananchi hususan Kata ya Mshewe Mbeya Vijijini.
Mallya alisema masuala mengine ni pamoja na ugumu wa upatikanaji wa
huduma za maji safi na salama, Ukosefu wa huduma bora za afya, uongozi
mbovu na rushwa maeneo mbalimbali, pamoja na unyanyasaji wa wanawake na
wasichana karibu maeneo yote yaliofanyiwa utafiti.
Akifafanua zaidi alisema utafiti ulibani kuchukuliwa kwa maeneo ya ardhi
yenye rutuba Kijiji cha Mshewe mkoani Mbeya hali inayosababisha
wananchi kukosa ardhi ya kutosha kwa kilimo na makazi hivyo kulazimika
wao kuwa vibarua katika mashamba ya wawekezaji ili kujikimu kimaisha.
Hali hiyo pia imechangia wanaume kulazimika kutoa rushwa ya pesa ili
kupata kazi katika mashamba.
“Wanawake na wasichana wamekuwa wakifanya vibarua katika mashamba ya
wawekezaji kwa ujira mdogo kati ya shilingi (2,500/- na 3000/- tu kwa
siku). Wakati huo huo wanakumbana na ukatili katika ajira hiyo ikiwemo
rushwa ya ngono, hali ambayo inasababisha ongezeko la magonjwa
ambukizi yakiwemo VVU na Ukimwi.
Alisema licha ya Sera ya Taifa ya Maji kuweka lengo la kupatikana kwa
maji katika umbali kwa mita 400; bado maji safi na salama ni changamoto
kubwa kwa wakazi wa Kishapu na Mshewe kwani hakuna huduma za maji safi
na salama hali inayotishia maisha na afya zao.
“Mfano Kijiji cha Ilota- Mshewe, licha ya uhaba mkubwa wa maji
wananchi wanasaka maji katika eneo hatarishi huku wakichangia maji
kidogo yasiyo safi na salama pamoja na mifugo.
Cha kusikitisha wananchi
wamechanga pesa kwa ajili ya maji kwa muda mrefu bila mafanikio. Katika
vijiji vya Isoso na Lubaga Kata ya Kishapu, ukosefu wa maji
umesababisha wanawake na wasichana kutembea umbali mrefu na mazingira
hatarishi ambayo yamesababisha ongezeko la mimba za utotoni, ubakaji kwa
wanawake na wasichana na vipigo.”
Alisema tatizo hilo limeongeza umasikini wa kipato kutokana kutumia muda mwingi na rasilimali kusaka maji.
Kilio chao kikubwa ni kupata vyanzo mbadala vya maji hasa kutoka zi
wa Victoria.
Aidha aliongeza utafiti ulibainia huduma mbovu za afya
kwani katika Kijiji cha Ilota Mkoa wa Mbeya wananchi wamekiri kutokuwepo
na zahanati hali inayosababisha wanawake wajawazito kujifungulia
majumbani, huku Kata ya Kisaki Morogoro vijijini, tatizo kubwa likiwa ni
ukosefu wa dawa na wahudumu wa afya zahanati za vijiji vya Gomero,
Station na Nyarutanga licha ya uwepo wa majengo mazuri bila wahudumu,
dawa wala vifaa tiba kwa ajili ya uchunguzi. Eneo hilo pia wananchi
huchangia gharama kubwa za usafiri wa gari la wagonjwa (shs 70,000)
kwenda Morogoro hususan wanawake wanaokwenda kujifungua.
Alisema suala la viongozi kutowajibika na vitendo vya rushwa
limejitokeza karibu maeneo yote ya utafiti ikiwemo uwepo wa usiri wa
taarifa za mapato na matumizi, viongozi kutowashirikisha wananchi katika
masuala ya maendeleo, viongozi ngazi za vijiji kuruhusu video za ngono
kuoneshwa maeneo yao na kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.
“Unyanyasaji wa kijinsia umejitokeza kama suala mtambuka katika
maeneo yote. Mfano tatizo la maji linasababisha vipigo kwa wanawake,
ubakaji, elimu duni kwa wasichana, mimba za utotoni na ukosefu wa
kipato. Kwa upande wa uwekezaji/ardhi, wanawake na wasichana wamekumbana
na rushwa ya ngono, ajira isiyo na staha pamoja na kipato kidogo na kwa
upande wa afya, wanawake wamekuwa wakidaiwa fedha na vifaa wakati wa
kujifungua na hata kujifungulia katika mazingira hatarishi,” alisema
Mallya.
Aidha alisema lengo kuu la utafiti huo ilikuwa kujenga mifumo mbadala
dhidi ya mfumo dume, uliberali mamboleo na mifumo yote kandamizi, huku
akidai maafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuendeleza kampeni ya Haki
ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake Walioko Pembezoni ambayo
imewezesha kujenga nguvu za pamoja na kuongeza uelewa wa masuala ya
kijinsia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi mbalimbali
hapa nchini na hata nje ya nchi.



Post a Comment