Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA) inapenda kuufahamisha
umma kuwa kuanzia tarehe 1 Juni,
2013, SUMATRA ilianza kutoa leseni za
kusafirisha abiria kwa magari yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 7 hadi 14.
Hatua hii
imefikiwa na SUMATRA ili kuimarisha udhibiti katika sekta hii ya usafiri ambapo huduma ya usafirishaji
abiria kwa kutumia mabasi madogo yanayobeba abiria kuanzia 7 hadi 14 yanatoa
huduma bora, salama na yanakidhi viwango. Aidha hatua hii imekusudiwa kusaidia
wamiliki kufanya biashara ya usafirishaji kwa weledi na ufanisi zaidi na mdhibiti
kuwasimamia watoa huduma hao na hivyo kuimarisha shughuli za udhibiti ili kuwa
na usafiri bora na salama kwa wananchi wa Tanzania.
Ili kufanikisha utoaji leseni kwa ajili
ya usafirishaji wa abiria, wamiliki wa magari hayo ambayo yanajumuisha magari
aina ya NOAH wameelekezwa kuzingatia yafuatayo:
1)
Magari husika yawe na madirisha ya
kufunguka na kufunga kwa ajili ya kuingiza hewa ya kutosha.
2)
Mlango wa abiria uwe upande wa kushoto
tu na endapo gari lina mlango upande wa kulia, mlango huo uzibwe moja kwa moja kwa ajili ya usalama kama
ilivyobainishwa katika Kanuni za SUMATRA za Viwango vya Ufundi, Usalama na Ubora wa Huduma wa Magari ya Abiria, 2008.
3)
Magari hayo yawe na sehemu maalumu ya
watu kupita wakati wa dharura tofauti na mlango wa kuingilia abiria.
4)
Magari hayo yataruhusiwa kutoa huduma ya
usafirishaji abiria kwenye maeneo yenye upungufu wa huduma za usafiri na kwa umbali usiozidi kilometa hamsini
(50) .
5)
Magari hayo hayatapewa leseni kutoa huduma kwenye majiji ambayo Mamlaka tayari imeshachukua
hatua za kukataza matumizi ya magari ya
uwezo huo kwa ajili ya kuondoa msongamano.
6)
Magari yatakayopata leseni ya
kusafirisha abiria yatapaswa kupakwa rangi maalum kwa ajili ya utambulisho wa
gari la abiria na utambuzi wa njia kama itakavyoelekezwa na SUMATRA.
7)
Magari yatakayopewa leseni ya
kusafirisha abiria yatapaswa kutumia nauli zilizopitishwa na kutangazwa na SUMATRA.
SUMATRA
itatoa leseni ya usafirishaji wa abiria baada ya mmiliki wa gari husika
kukamilisha matakwa yote yaliyotolewa hapo juu.
Tungependa wananchi na wadau kwa
ujumla waelewe kwamba, leseni ni nyenzo muhimu ya udhibiti.
Faida za leseni ya usafirishaji ni
pamoja na:
1. Leseni humsaidia Mdhibiti kama
SUMATRA kuwa na taarifa sahihi za watoa huduma ikiwa ni pamoja na anuani zao
hivyo kuweza kuwafikia kiurahisi katika masuala kama
vile mafunzo n.k.
2. Leseni humsaidia Mdhibiti kuweka
utaratibu muafaka wa utoaji huduma kwa kuhakikisha unakuwa salama na bora.
3. Leseni husaidia katika kubaini
upatikanaji wa huduma katika maeneo mbalimbali.
4. Leseni ni utambulisho na hivyo
humsaidia mtoa huduma kutoa huduma bila bughudha.
5. Leseni husaidia umma kuwatambua watoa
huduma halali na hivyo kuwatumia.
6. Leseni husaidia katika masuala ya
fidia za bima.
7. Leseni ni uthibitisho kwamba chombo
cha usafiri ni salama na kinafaa kwa kutoa huduma ya usafiri.
Hivyo tunatoa wito kwa watoa huduma
kukata leseni ya usafirishaji ili waweze kufaidika na faida zilizotajwa hapo
juu.
SUMATRA imekuwa ikifanya kazi karibu sana na Jeshi la Polisi kama
msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Sheria hapa nchini. Pale ambapo taarifa za
Polisi zinapothibitisha ukiukwaji wa sheria, hatua za kisheria huchukuliwa na
mdhibiti (SUMATRA).
Kutokana na hali hii tunapenda
kuwafahamisha wamiliki wa mabasi madogo ya abiria 7 hadi 14 na umma kwa ujumla
kuwa SUMATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani
watafanya ukaguzi kwa magari yote yasiyo na leseni za usafirishaji ili
kuhakikisha mabasi yote yanayotoa huduma ya usafiri kwa umma yana leseni halali
ya usafirishaji abiria na kufuata Sheria, Kanuni na Masharti yote yaliyobainishwa
katika leseni hiyo.
Ni vyema
wamiliki wa vyombo vya usafiri hususan wa mabasi madogo kuzingatia na kufuata
Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo kwa ajili ya maslahi ya muda mrefu na yenye
tija kwao kama watoa huduma na kwa sekta ya usafirishaji abiria hapa nchini.
Kwa kushirikiana tunaweza kuwa na
usafiri bora na salama!
Imetolewa na:
Meneja
Mawasiliano
SUMATRA
Juni, 2013
Post a Comment