Na
Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA
Cha Muziki wa Hip Hop Tanzania (TUMA), kimetuma salamu ya rambirambi kufuatia
kifo cha msanii wake Langa Kileo, aliyefariki juzi katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili na kuibua machungu upya kwa wapenzi wa muziki huo nchini.
Marehemu
Langa Kileo enzi za uhai wake.
Wiki
iliyopita, wadau wa muziki wa Hip Hop walimpoteza Albert Mangweha ‘Ngwair’,
aliyezikwa katika makaburi ya Kihonda mjini Morogoro, huku mapema wiki hii
msanii wa filamu, Jaji Khamis Kash alifariki Dunia na kuleta hofu katika ulingo
wa sanaa hapa nchini.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tanzania Urban Music Association
(TUMA), Fredrick Mkoloni, alisema kuwa Tanzania imempoteza msanii mwingibne
mwenye uwezo wa juu katika uimbaji wa muziki wa Hip Hop.
Alisema
kwasababu hiyo, TUMA wapo mstari wa mbele katika kipindi hiki kigumu cha
mfululizo wa vifo vya wasanii Tanzania, ambapo pia wamewataka wadau, mashabiki
na wasanii kwa ujumla kumuombea marehemu ili akapumzike kwa amani.
“Huu
ni wakati mgumu kwa Watanzania wote baada ya Langa naye kufariki Dunia, hivyo
tunaomba ndugu zetu tushirikiane katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na
ndugu yetu, ikiwa ni siku chache baada ya kuzikwa Ngwair mkoani
Morogoro.
“TUMA
tutaendelea kushirikiana kwa namna moja ama nyingine katika kifo cha Langa, huku
tukiomba na wasanii wote tushirikiane katika msiba wa ndugu yetu Langa,”
alisema.
Wasanii
mbalimbali wameonyeshwa kupata mshtuko mwingine, akiwamo Kalapina, aliyeibuka na
kusema hofu imezidi kutawala na kumuombea marehemu aende akapumzike kwa
amani.
Kalapina
alisema kuwa Langa ni miongoni mwa wasanii wenye kutoa mashairi mazito, hivyo
Hip Hop imezidi kukumbwa na wasiwasi wa aina yake kwa kuwapoteza vijana wao
wenye makali ya hali ya juu katika ramani ya muziki huo nchini.
“Langa
ni msanii mzuri mwenye uwezo wa juu, hakika nitamkumbuka kwa mengi, maana kifo
chake ni pigo kwa Watanzania na wadau wote kwa ujumla,” alisema
Kalapina.
Naye
Kala Jeremia, alisema kuwa kifo cha Langa ni pigo zaidi katika muziki wa Hip Hop
hapa nchini, baada ya kurafiki katika Hospitali ya Muhimbili.
“Tutaendelea
kumkumbuka msanii mwenzetu Langa, maana wote safari ni moja,” alisema Kala
ambaye tuzo yake ya wimbo bora wa Hip Hop aliyposhinda ameamua kuipeleka katika
familia ya Ngwair kutokana na kuthamini mchango wake.
Ratiba
ya kifo cha Langa imepangwa kuwa msanii huyo ataagwa siku ya Jumatatu kuanzia
saa saba mchana, ambapo saa 10 alasiri atazikwa katika makaburi ya Kinondoni
jijini Dar es Salaam.
Post a Comment