Dar es Salaam. Miradi mbalimbali ya mashirika ya umma, nchini iliyopangwa kutekelezwa mwaka wa fedha 2013/14 huenda ikakwama kutokana na uamuzi wa Serikali kuagiza mashirika yote hayo yatoe asilimia 10 ya mapato yake kwa kuichangia Serikali.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumamosi umebaini kuwa tayari Serikali, imetuma waraka kwa mashirika hayo, ambayo hata hivyo baadhi yapo katika hali mbaya kwa sasa kutokana na kushindwa kuendeleza miradi kadhaa ya maendeleo.
Mbali na mashirika ya umma kutakiwa kuchangia fedha kwenye mfuko wa Serikali, Serikali pia haijapeleka fedha za ruzuku katika halmashauri mbalimbali nchini pamoja na kushindwa kuwalipa posho wafanyakazi wake maeneo mbalimbali.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya halmashauri kushindwa kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyomo kwenye bajeti.
Mtendaji wa moja ya halmashauri mkoani Pwani aliliambia gazeti hili; “Kwa sasa kweli hali ni mbaya, hakuna fedha iliyofika kutoka serikalini, hakuna shughuli inayohitaji fedha ambayo inafanyika.”
Taarifa za ndani kutoka Wizara ya Fedha zinasema kwamba Serikali haina fedha kwa sasa ambapo sasa inalazimika kukusanya fedha kutoka katika mashirika yake ili kuendesha shughuli zake.
Miongoni mwa mashirika ya umma yanayoguswa na uamuzi huo wa Serikali ni mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwamo NSSF, PSPF, Mamlaka Udhibiti wa Nishati na Maji(Ewura)Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa(Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na mengine kadhaa.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyakazi wa Idara za Fedha za mashirika hayo, walieleza kuwa kutokana uamuzi huo wa Serikali sasa wanalazimika kukaa ili kuandaa upya bajeti za mashirika hayo.
“Ukweli haya maagizo yana athiri kubwa kwetu kwani tayari tulikuwa tumepanga bajeti kutokana na mapato na kwa uamuzi huu ambao kimsingi hakuna mamlaka ya kuyapinga, itabidi tutoe, ila adhari zitakuwepo,”alisema ofisa mmoja wa juu wa moja ya mashirika ya umma.
Hata hivyo, alisema kuwa iwapo wangeshauriwa mapema basi walau wangetakiwa kuchangia asilimia tano kwa mwaka huu wa fedha na mwaka ujao ndipo ingeongezeka kufikia asilimia 10.
Ofisa mwingine wa shirika la umma aliyeomba kutotajwa jina alieleza kuwa uchangiaji huo, ulipaswa kutazama mashirika, kwani yapo yanayojiendesha kwa hasara, mengine yanapokea ruzuku na mengine yanajiendesha kwa fedha zake.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumamosi umebaini kwa Tanapa pekee inatakiwa kulipa Sh24 bilioni, zinazotakiwa kukatwa kutoka kwenye bajeti yao ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya shirika na jamii inayowazunguka. MWANANCHI
Post a Comment