Dar es Salaam. Biashara ya dawa za kulevya nchini inazidi kuchukua sura mpya ambapo sasa wanawake wanaouza vyakula, maarufu mama ntilie, hutumika kusambaza dawa hizo kwa wateja.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa biashara hiyo inafanyika katika maeneo ya Tandika, Manzese, Vingunguti, Temeke, Tandale, Mtongani na Keko.
Wanawake hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuuza chakula kama kinga yao, huku biashara yao kubwa ikiwa ni kuuza dawa za kulevya aina ya heroin, bangi na aina nyingine.
Mbinu hii mpya ya usambazaji wa dawa za kulevya kwa kutumia wanawake wanaouza vyakula imeelezwa kuwa inawasaidia wahusika wakuu, kuendesha biashara yao kwa ufanisi zaidi.
Uchunguzi umeonyesha kuwa wafanyabiashara wa dawa hizo wameamua kuwatumia mamalishe kutokana na kuwa waaminifu na kuhudumia wateja wengi, hivyo ni vigumu watu kuwashtukia wakiwamo askari polisi.
Imebainika kuwa dawa hizo huuzwa kulingana na maeneo, wakati maeneo ya watu wasiokuwa wa uwezo hupimwa kwa kutumia kipimo kidogo zaidi kwa bei ya chini ambayo watumiaji husika huweza kuimudu.
Aidha dawa hizo hufungwa katika mitindo miwili tofauti, ukiwa katika unga wa vidonge na wa kawaida ingawa bei zake hazitofautiani sana.
Uchunguzi unaonyesha kuwa vidoge huuzwa vikiwa vizima au vipande, huku unga wa kawaida ukiuzwa kwa kipimo maalumu.
Kwa kawaida ‘unga’ huo huuzwa kwa Sh1,000 kwa pointi huku kete moja ikiuzwa kwa Sh2,000, wakati vidonge, kizima huuzwa kwa Sh2,000, huku kipande huuzwa kwa Sh1,000 zikitofautiana kulingana na maeneo.
MWANANCHI



Post a Comment